Wednesday, August 20, 2014

HAPPY BIRTHDAY MONALISA

HAPPY BIRTHDAY MONA LISA

G5 MODERN TAARAB LEO UKUMBIMMMOJA NA TWANGA

KUNDI la G5 Modern Taarab ambalo leo litavaana na Wakali wa Kisigino ‘Twaga Pepeta’, jana lilifanya shoo ya kujiweka sawa, kwenye ukumbi wa Flamingo Night Club, Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Pambano la leo kati ya wakali hao wa Dansi na Taarab, limepangwa kurindima kwenye ukumbi wa Equator Grill, Mtoni Kwa Azizi Ally, jijini Dar es Salaam, kuanzia majira ya saa 3:30 na kuendelea hadi majogoo.Blog hii itakayekuwapo kwenye ukumbi wa Equator baadae usiku kuwaletea kitakachojiri,  viongozi wa makundi hayo wote walionyesha kujiamini kwa kudai wamejiandaa kikamilifu.

MAPACHA WATATU NDANI YA MASAI CLUB

MWIMBAJI Januari Mavoko amerejea kwenye kundi la Mapacha Watatu kwa mbwembwe za mkwara mzito wa kutotaka kuajiriwa na badala yake sasa ameanza kufanya kazi kimkataba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwenye ukumbi wa Masai Club,Kinondoni jijini Dar es Salam ambako bendi hiyo ilikuwa ikitumbuiza, Mavoko alisema kuwa, amejifunza mengi kuhusiana na maisha ya kufanya kazi kwa kuajiriwa.
“Nimerudi kuongeza nguvu kwenye bendi yangu hii ya nyumbani, lakini kwa mkataba maalum, hivyo kama unaenda kuandika kaandike kuwa nimekuja kuzidisha mashambulizi,” alisema Mavoko.
Alipoulizwa kuhusu zawadi aliyowaletea mashabiki wa Mapacha, Mavoko alisema kuwa, amerudi na tungo kali atakayoifyatua hivi karibuni, ambayo itakuwamo ndani ya albamu ijayo ya Mapacha Watatu. Wakati huohuo Mapacha Watatu jana iliitumia fursa ya onesho lao la Masai Club, kutambulisha wimbo wao mpya unaokwenda kwa jina la ‘Kombe Uwanjani’, ambao ni makucha ya Mkurugenzi wa kundi hilo, Khalid Chokora.
Wimbo huo ulioko kwenye miondoko mchanganyiko ya Rhumba na Sebene, ulionekana kupokelewa vema na mashabiki ambao baadhi yao, ulipomalizika walikuwa wakishinikiza urudiwe.
Ndani ya ‘Kombe Uwanjani’ ambao kwa mujibu wa Chokoraa mwenyewe, tayari umesharekodiwa, kuna ujumbe wa mpenzi wa zamani anayepashwa kuwa wakati wake umeshapita hivyo amwache mwenzie atanue na mtu aliyenaye sasa.
“Kibao hicho ni hatua za awali kabisa za mchakato wa maandalizi ya albamu yetu ijayo tutakayoifyatua baadae mwaka huu,” alisema Chokoraa.
Ukumbi wa Masai,ulianza kuonekana mdogo tangu mishale ya saa 6:00 usiku , wakati bendi ya muziki wa Dansi, Mapacha Watatu ilipokuwa ikirindimisha muziki wa aina yake.
Mashabiki wengi walioingia kuanzia majira ya saa 5:30 na kuendelea, walionekana kusimama kwa muda wote kutokana na kukosa viti, jambo lililozidi kuufanya ukumbi huo kuonekana mdogo zaidi hapo jana.
Hakuna aliyejali ingawaje pia kulikuwa na hali ya joto la kiaina lililotokana na kuzidiwa nguvu kwa kiyoyozi humo ndani.
Muziki mtamu wa vijana wa Mapacha Watatu, uliokuwa ukinakshiwa na rapu za Issa Saad ‘Tulanongo’ na Khalid Chokora, uliwafanya mashabiki ‘kusahau shida zao’ kwa kuchizika katikati muda wote.
Waimbaji Jose Mara, Januari Mavoko, Cindy na wengineo, sambamba na wapiga ala wao, walitosha kabisa kuwafanya mashabiki kuiona burudani ya jana kuwa ni ya kipekee. Pata picha za shughuli hapa.........


MISAMBANO ALAUMU WENYE BENDI KWA KUSHUSHA HADHI YA MUZIKI WA DANSI

MWIMBAJI mahiri wa kundi la TOT, Abdul Misambano ‘Super Rocks’ yuko mbioni kuvirekodi upya baadhi ya vibao vyake vya Dansi, ili kutekeleza matakwa ya mashabiki wake wanaomuomba kufanya hivyo.
Akizungumza jijini Dar es Salam, Misambano alisema kuwa, hivi sasa anamalizia kutengeneza albamu yake binafsi ya mipasho ambapo baada ya hapo ndipo ataingia kwenye kuvirudia vibao vyake vya dansi.
“Nitakapovirudia vibao hivyo, nitahakikisha siharibu uhalisia ingawaje nitaviongezea ladha na vionjo ili kuvinogesha zaidi,” alisema Misambano.
Alisema kuwa, badhi ya wanamuziki atakaowashirikisha kwenye shughuli hiyo ni wale aliorekodi nao awali TOT, huku wengine wakiwa ni Wakongo wachache.
Baadhi ya vibao vitakavyokuwamo kwenye albamu yake hiyo, ni ‘Mpende Akupendae’, ‘Mnyonge Mnyongeni’, ‘Acha Waone Wivu’ pamoja na kile cha kwanza kukitunga alipojiunga na TOT, ‘Naachia Ngazi’.
Wakati huohuo  mwimbaji huyo, ‘Super Rocks’ amefunguka na kusema kuwa amevunja rasmi ndoa yake na muziki wa Dansi iliyodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Akizungumza na blog hii, Misambano alisema kuwa, kuanzia sasa atakuwa tu akijihusisha na miondoko ya muziki wa mipasho, huku akifanya shughuli zake nyingine.
“Sina muda tena kwenye Dansi hata nikifuatwa na bendi nyingine kwa dau lolote lile,” alisema Misambano.
Hata hivyo, Misambano alisema kuwa, deni pekee alilobakisha sasa kwenye dansi ni kuvirudia vibao vyake vya zamani alivyoviimba akiwa na TOT Plus Band.
Abdul Misambano  amesema  kuwa muziki wa Dansi umeshuka chati huku akishusha  shutuma nzito kwa wamiliki wa bendi kwa kudai wamechangia kwa kiasi kikubwa kuuporomosha muziki huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Misambano alisema kuwa, nafasi ya wamiliki wa bendi katika kuliporomosha Dansi ipo pale wanapohusika kuwahamisha ovyo wanamuziki na kuvuruga bendi nyingine.
Alisema kuwa, wanamuziki wengi wameshindwa kubaini walipokosea ili kusawazisha makosa yao na badala yake kuishia kutupia lawama kwa vyombo vya habari hapa nchini.
“Hata hivyo, Dansi linaweza kurudi kwenye hadhi yake wakati wowote kwasababu muziki ni mzunguuko, lakini ni vema pia wanamuziki wakajitoa kwenye utumwa wa kuyumbishwa na baadhi ya wamiliki,” alisema Misambano. Picha za misambano kazini hizi hapa.......MORO INTERNATIONAL BENDI YA WANAMUZIKI NDUGU

BENDI inayowakusanya wanandugu wengi pamoja, Moro International ya jijini Dar es Salaam, jana ilionekana kukitumia vema kiwanja chake cha nyumbani, Taxido Bar, Yombo Buza kwa kufanya shoo iliyowasisimua wengi.
Moro International inaongozwa na Marijani Muhumba pamoja na kaka yake, Shaibu Muhumba ambao ni baba wa kijana machachari katika gitaa la Solo, anayetamba na bendi ya Ruvu Stars hivi sasa, Sele Muhumba.
Katika onesho lao hilo la jana, Wana Muhumba walionekana kwenda sambamba na matakwa ya mashabiki wao kwa kumudu vema kupiga mzigo uliofaulu kukata na kumaliza kabisa kiu ya waliohudhuria.
Vibao vyao vikali pamoja na vile kadhaa vya kukopi walivyokuwa wakichanganya, vilikuwa vikichangia utamu na raha ya aina yake kwa mashabiki waliokuwa wamejazana ndani ya ukumbi huo kuwashuhudia.
Moro International hutumbuiza kwenye ukumbi huo kila wiki katika siku za Jumamosi , huku mahudhurio ya mashabiki yakionekana kuwa ni ya kuridhisha mno.MPIGA GITAA AKIMBIA KUNDI LA TAARABU NA KUJIUNGA NA BENDI KUKIMBIA TUHUMA NA KUTOKA NA MKE WA BOSI

TUHUMA ya kutoka kimapenzi na mke wa bosi wake, zimemfanya mcharazaji gitaa mahiri, kulikimbia kundi la Taarab alilokuwa kilipigia na kurejea kwenye bendi aliyokuwa zamani.
Akizungumza na mwandishi wa blogu hii, mpiga gitaa huyo alisema kuwa, amechoshwa na lawama za mara kwa mara kutoka kwa kiongozi wa kikundi cha Taarab  alichokuweko, akituhumiwa kumgeuka kwa mkewe.
“Kumbe kulianza kuwa na migogoro ya chini kwa chini baina yao, mke na mume, kabla ya kunikabili na kuniambia kuwa niachane na mke wake ili kuepuka kunitokea makubwa,” alisema mwanamuziki huyo ambaye pia ni mtunzi hodari anaechipukia.
Mpiga gitaa huyu anasema amerejea bendi yake ya zamani kiroho safi ambapo hivi sasa anapika kibao kikali kitakachokuwa zawadi kwa mashabiki wa bendi hiyo aliowatosa kwa kipindi kirefu.

TALENT BAND YA HUSSEIN JUMBE IKIBURUDISHA KISUMA SABASABA MBAGALA

BENDI ya Talent inayoongozwa na mwanamuziki nguli Hussein Jumbe, imeendelea kutesa kwenye kiwanja chake cha nyumbani, Kisuma Sabasaba, Mbagala, jijini Dar es Salaam walipokuwa wakitumbuiza, katika onesho lao la kawaida la kila wiki.
Mwandishi wa habari hizi aliyekuwamo ndani ya ukumbi huo wa Kisuma, alishuhudia namna mashabiki walivyokuwa wakivisusa viti vyao mara kwa mara na kujimwaga katikati kucheza, huku baadhi yao wakionekana kupagawa zaidi na kutuza.
Jumbe mwenyewe alikuwa akiwakosha zaidi mashabiki wake kwa kuwafyatulia vibao vyake vikali, huku vingine vikiwa ni vile alivyovirekodi alipokuwa katika bendi za Mlimani Park Sikinde na Msondo Ngoma Music.
Onesho hilo lilimalizika majira ya saa 7:00 usiku, huku wapenzi na mashabiki mashabiki wakipiga kelele wakiomba rhumba liendelee kutokana na kuwa bado wana hamu ya kuendelea kuusakata muziki wa Talent.


                           Picha za Wana Talent Band jukwaani Kisuma Bar Mbagala


MSONDO NA TALENT BAND JUKWAA MOJA AGOSTI26

WAKALI wa Dansi, Talent Band chini ya Mkurugenzi Hussein Jumbe, Alhamisi Agosti 26, mwaka huu, wanatarajiwa kukutana uso kwa uso na kaka zao, Msondo Ngoma Music, kwenye uzinduzi wa ukumbi wa Kisuma Mwembeyanga, jijini Dar es Salaam.
Onesho hilo ni la kawaida, ambapo bendi hizo zimealikwa kutoa burudani kwenye shughuli hiyo ya uzinduzi wa ukumbi huo, lakini hata hivyo tayari baadhi ya mashabiki wa Talent na Msondo wameanza kuligeuza kuwa pambano.
Katika onesho hilo lililopangwa kuanza kuunguruma majira ya saa 12:00 jioni, bendi hizo zimejipanga kukonga nyoyo za mashabiki wao kwa kuwaporomoshea nyundo zao kali; mpya pamoja na zile zamani zinazoendelea kutesa hadi sasa. 

JAHAZI MODERN TAARAB YATEKA NYOYO GADAFFI SQUARE

UKUMBI wa Gadaffi Square, jijini Dar es Salaam, jana uliwaka moto pale kundi mahiri la mipasho, Jahazi Modern Taarab linalotumia mtindo wa ‘Wana Nakshi Nakshi’, lilipokuwa likimwaga burudani ya aina yake.
Onesho hilo lililoonekana kujaa msisimko wa hali ya juu, lilianza kurindima majira ya saa 4:00 usiku na kuendelea hadi saa 9:00, huku mashabiki waliokuwa wamefurika wakijirusha kati kucheza karibu kila kibao kilichokuwa kikitumbuizwa.
Wakati mwingine, baadhi ya mashabiki walikuwa wakinengua hata pale magitaa na vinanda vilipokuwa vikidodoswa peke yake baada ya wimbo kumalizika na kabla ya mwingine kuanzishwa.
Baadhi ya wasanii walioonekana kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki, ni Kiongozi wa kundi hilo, ‘Mfalme’ Mzee Yussuf, Aboubakar Soud ‘Amigo’ na Khadija Yussuf ‘Sauti ya Chiriku’.
Kati ya vituko vya jukwaani vilivyokuwa vikisisimua wengi kwenye onesho hilo  ni mpapasa kinanda Rashid Yussuf kupiga kinanda kwa mbwembwe za upande upande na wakati mwingine kujifanya anasinzia.
Aidha, alipopanda Mzee Yussuf na baada ya kutumbuiza vibao vyake vitatu vya ‘Nani Kama Mama’, ‘Najiamini’ na ‘Wasiwasi Wako’, Mchiriku wa aina yake ulirindimishwa na kuwafanya mashabiki wajisahau na kuanza kunesa kitejateja.
Kwa ujumla onesho hilo lilikuwa zuri kutokana na kufana vilivyo, hasa kwa kuhudhuriwa na mamia ya mashabiki, ingawaje kulikuwa na dosari ndogondogo za fujo za hapa na pale kwa baadhi ya mashabiki waliokuwa wamekolea kinywaji.