Thursday, August 14, 2014

NEW ADEN MODER TAARAB YACHIZISHA MTU MONNIE JUNCTION

WAKATI mwingine burudani ya muziki wa kiingilio kinywaji una raha yake, kama ilivyoshuhudiwa  katika ukumbi wa ukumbi wa Monnie Junction, jijini Dar es Salaam.
Katika ukumbi huo jana, kundi la mipasho la New Aden Modern Taarab lilikuwa likitumbuiza na kuonekana kukonga zaidi nafsi za mashabiki waliokuwa wamehudhuria shoo hiyo.
Baadhi ya picha hapo chini, mwanadada ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja alionekana kucharuka zaidi kila pale Wana Aden walipokuwa wakiporomosha nyimbo.
Aden ni kati ya makundi ya mipasho yaliyotapakaa kwa wingi hivi sasa, yanayofanya maonyesho yake kwa kurindimisha zaidi vibao vya kukopi; vya zamani na vinavyotamba sasa ambavyo vimerekodiwa na makundi mengine.
Hata hivyo, kundi hilo lililo chini ya Mkurugenzi wa Salum Haji Chaurembo, lina nyimbo zake kadhaa ambazo hazijabahatika kupata umaarufu kwa mashabiki kama vile ‘Sikwa Cheketu Cheketu’....YALIYOJIRI...

UNAKUMBUKA KUNDI LA MASS MEDIA? BASI LINARUDI TENA

Zahir Ally Zorro
MASHABIKI wa muziki wa dansi nchini wameombwa kukaa mkao wa kula kusubiri ujio mpya wa bendi ya Mass Media iliyoanzishwa na kuwahi kutamba kwa mwaka mmoja pekee, 2000 kabla ya kuvunjika na wanamuziki wake kusambaratika. 
Ombi hilo limetolewa na aliyekuwa Kiongozi wa kundi hilo, Zahir Ally ‘Zorro’ aliyesema kuwa makao makuu ya Mass Media mpya yatakuwa nyumbani kwake Vijibweni, jijini Dar es Salaam ambako ameandaa sehemu maalum ya kufanyia mazoezi na wanamuziki kupumzika.
“Unajua, nimebakiza miaka isiyozidi 10 tu katika muziki kama Mungu atanijaalia, hivyo ni muhimu kuwaachia mashabiki wa dansi kitu cha ukumbusho kutoka kwa Zorro,” alisema.
Alisema, maandalizi ya Mass Media inayotarajiwa kuanza kambi mwezi ujao yamekamilika kwa asilimia 75, kutokana na kuwa tayari ana seti nzima ya vyombo, huku akitamba kuwa ana wanamuziki wake wa kudumu kutoka katika mikoa mbalimbali nchini.
Zorro alisema kuwa, ujio mpya wa Mass Media utakuwa ni uliojaa wanamuziki chipukizi lakini wenye vipaji na heshima ya hali ya juu, wasiovuta bangi wala kunywa pombe na ambao wataporomosha zaidi muziki wa Rhumba kuliko sebene.
KARIBU TENA MASS MEDIA (Picha kwa hisani ya http://abdallahmrisho.blogspot.com)

KUNDI LA TAARAB LA G5 LATANGAZA HALI YA HATARI

JINSI mambo yalivyokuwa kwenye shoo ya Jumamosi iliyopita ndani ya ukumbi wa Sisi Club, Msasani, Dar es Salaam limeipa kiburi G5 Modern Taarab kuijinasibu kuwa kundi bora linalochipukia kwenye miondoko ya mipasho.
Hamis Slim ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa G5 Modern ameweka wazi kuwa, wameamua kuvunja ukimya na kuchomoa makucha ili kuwadhihirishia mashabiki wa mipasho kuwa wamekuja kuwashika.
Slim alisema kuwa, wakiwa wanajianda na uzinduzi wa albamu yao ya kwanza baadae mwaka huu, watayatia shoti makundi kadhaa ya mipasho hapa nchini kwa kunyakua baadhi ya wasanii wake mahiri.
Slim alisema kuwa, watafanya hivyo kwa ajili ya kuiimarisha zaidi G5 inayozidi kushika chati kila uchao kwa kuzoa mashabiki kutoka pande mbalimbali hapa nchini.
Tayari wameshafanya mazungumzo na baadhi ya wasanii kutoka katika makundi kadhaa ya taarab yanayotamba sasa ambao wameonyesha kuafikiana nao.
“Ni mapema mno kutaja majina ya wasanii hao na makundi wanayotoka, lakini ukweli ni kuwa, kabla hatujazindua albamu yetu mpya, tutawanyakua wasanii kadhaa wakubwa ili kujiboresha zaidi,” alisema Slim.
Slim alisema, uzinduzi wa albamu yao hiyo mpya, inayokwenda kwa jina la ‘Kigodoro’ utafanyika kabla ya mwezi Oktoba, katika ukumbi utakaotangazwa hivi karibuni.
Baadhi ya wasanii waliopo sasa ndani ya G5 ni pamoja na Mwanahawa Ali, Ashura Machupa, Zena Mohammed, Abdul Misambano na Mwamvita Shaibu.

Yaliojiri Sisi Club
TWANGA PEPETA WAFANYA MAMBO SUNSET CLUB -JET LUMO

USIKU wa jana kuamkia leo ulikuwa ni uliojaa msisimko wa kipekee kwa wakazi wa Jeti Lumo, jijini Dar es Salaam pale wakali wa Kisigino, African Stars ‘Twanga Pepeta’ walipofanya shoo ya kufa mtu, kwenye ukumbi wa Sunset Club.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni ya ASET Entertainment inayomiliki bendi hiyo, Asha Baraka, shoo hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya utambulisho wa wanamuziki wao wapya, nyimbo pamoja na rapu zilizopangwa kuwamo kwenye albamu ijayo.
Ukumbi wa Sunset tangu kuanza kwa shoo hiyo, ulishuhudia namna mashabiki walivyokuwa mara kwa mara wakiviacha viti vyao vikiwa tupu na kujimwaga katikati kucheza kwa mzuka.
Baadhi yao walioonekana kupagawa zaidi walionekana kupigana vikumbo kupanda jukwaani kuwatuza baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiwavutia zaidi.
Vibao vya zamani kama vile; ‘Sumu ya Mapenzi’, ‘Password’ na ‘Safari 2005’ viliwakosha zaidi mashabiki waliokuwa wamefurika ukumbini humo, huku kile kipya kiitwacho ‘Mapenzi Yanauma’, nacho kikipokelewa vizuri kilipotumbuizwa.
Rapa Frank Kabatano aliyejiunga na bendi hiyo hivi karibuni akitokea TOT Plus, ni kati ya wanamuziki waliong’ara vilivyo usiku wa jana, huku pia ‘kiraka’ Kalala Junior ‘akivuruga’ akili za watu kwa kuchanganya rapa za Msaga Sumu kwenye sebeni ya baadhi ya vibao vyao.
Kwa upande wa rapu mpya, ndewe za wapenzi na mashabiki waliokuwamo kwenye ukumbi huo jana, ziliondoka na faida ya kusikia meseji za kisasa za ‘Kantangaze’, ‘Heshima Pesa’ na ‘Ahmada Umelewa’.

Picha za yaliyojiri