Friday, January 29, 2016

FILAMU YA SINGELI KUFWATIWA NA JICHO LA MCHAWI

IKIWA ni wiki tatu tangu iachiwe, muviya ‘Singeli’ imeonekana kufanya vema sokoni kiasi cha kufunika nyingine zilizotangulia.
Kwa mujibu wa waandaji wa filamu hiyo, Mmaka Film Production, kopi za awali zimemalizika na sasa wameanza kazi ya kudurufu nyingine ikiwa ni maombi maalum ya wateja wao.
“Tunashukuru kuona muvi hii ya ‘Singeli’ inaendelea kufanya vyema sokoni na mashabiki nchini wanaonekana kuipokea kwa mikono miwili,” alisema Mkurugenzi wa Mmaka Film, Omary Mmaka.
Mmaka alisema kuwa, hivi sasa wapo katika maandalizi ya kazi yao mpya inayokwenda kwa jina la ‘Jicho la Mchawi’, ambayo nayo itashirikisha nyota wengi wenye majina kama ilivyokuwa kwenye ‘Singeli’.

DISKO LEO DARLIVE WA MBAGALA MSIKOSE

DISKO la kukata na shoka linatarajiwa kuunguruma Ijumaa hii ndani ya Darlive, Mbagala Zakheem, Dar es Salaam katika shamrashamra za kuikaribisha wikiendi, imefahamika.
Mratibu wa Darlive, Juma Mbizo alisemajijini Dar es Salaam jana kuwa, disko hilo linaporomoshwa na Dj mahiri na maarufu kutoka kwenye moja ya radio zinazofanya vyema hivi sasa hapa nchini.
Mbizo alisema kuwa, kama ilivyo ada kwa siku za Ijumaa, wanawake wote watapenya bure, huku wanaume wakidondosha mlangoni mchango kiduchu wa buku tano.
“Nawaomba wapenda burudani wote wa Kitongoji cha Mbagala na Wilaya nzima ya Temeke kwa ujumla, kuhudhuria kwa wingi kwenye disko hilo, ili kufaidi raha isiyo na kifani,” alisema Mbizo, kati ya wadau wakubwa wa muziki hapa nchini.

WAPENZI WA KUNDI LA TAARAB LA WASHAWASHA CLASSIC WAMSAPRAIZ MPIGA KINANDA WAO

WADAU mbaimbali wa muziki, Jumapili iliyopita 24/1/2016, walilitumia jukwaa la bendi ya taarab ya Washawasha Classic, kumfanyia mwimbaji nyota wa bendi hiyo, Omary Sosha, sherehe ya kushitukiza ya siku yake ya kuzaliwa.
Tukio hilo la kusisimua na ambalo liliteka hisia za wengi, lilifanyika ndani ya ukumbi wa Centre Grill ‘Flamingo’ ambapo Washawasha Classic iliyo chini ya mpapasa kinanda mahiri, Amour Maguru, ilikuwa ikitumbuiza.
Wakati burudani ya muziki ikiendelea, ghafla liliibuka kundi la wadau kadhaa maarufu, wakiwemo ‘2po Dar Crew’, ‘Team Mombasa Raha’, ‘Mbaine Company Group’ wakiongozwa na wasanii Hummer Q na H Mbizo.
Walipoingia, wadau hao waliokuwa na keki kubwa na zawadi nyingine kemkemu, walikwenda moja kwa moja jukwaani ambako sosha alikuwa akipagawisha mashabiki kwa kuimba, wakamvamia na kuanza kumpongeza kwa wimbo wa ‘happy birth day’.
Alipohojiwa na mwandishi wetu baada ya tukio hilo, Sosha alisema anafurahi kuona wadau na wasanii wenzake wametambua umuhimu wa siku yake ya kuzaliwa, ambapo kwa upande mwingine ameahidi kuzidi kuwanao bega kwa bega kiburudani.

Tuesday, January 19, 2016

SIZONJE KAZI MPYA YA MRISHO MPOTO AKISHIRIKIANA NA BANANA ZOLLO

KIBAO KIPYA KABISA CHA MRISHO MPOTO  AMBACHO KASHIRIKIANA NA BANANA ZOLLO- SIZONJE, HEBU SIKILIZA SANAA HII

Sunday, January 3, 2016

Kundi la Muziki la Navy Kenzo Lashika Namba Nne Katika Video 50 Zilizobamba Zaidi MTV Base Mwaka 2015


Kundi la muziki la Navy Kenzo linaloundwa na Aika na Nahreel wamefanya vizuri baada ya video ya wimbo wao wa Game, waliomshirikisha Vanessa Mdee kushika Namba Nne katika chart ya Video 50 Bora za MTV Base Africa zilizofanya vizuri mwaka 2015..
Diamond Platnumz na wimbo wake wa Nana umeshika namba 5 katika chart hizo, wimbo huo wa Nana pia umetengenezwa na Producer Nahreel, kitu kinachomfanya aendelee kuwa producer bora zaidi kutoka Tanzania na Afrika ya Mashariki kwa ujumla,
Mwimbaji Wizkid wa Naigeria ameshika namba 6.
Pongezi ziende kwao @nahreel,@aikanavykenzo wanaounda Kundi la Navykenzo
Pia pongezi kwa Diamond Platnumz kwa kuwa namba 5 katika chart hiyo...

Friday, December 11, 2015

MWANAMUZIKI ROBERTO AMARULA KUTOKA ZAMBIA KUTUMBUIZA DAR ES SALAAM, DODOMA KATIKA TAMASHA LA INSTAGRAM WIKIENDI HII
Mwanamuziki na mtangazaji wa redio, Roberto Chindaba Banda 'maarufu Roberto Amarula kutoka nchini Zambia (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana , kuhusu onyesho lake atakalolifanya leo  katika fukwe za Escape One Mikocheni jijini Dar es Salaam na kesho ukumbi wa Ngalawa Pub mkoani Dodoma katika Tamasha la Instagram Party Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Freconic Ideaz, Fred Ngimba ambao wamemleta msanii huyo hapa nchini kwa kushirikiana na Kampuni ya C&G Solutions na kulia ni Mwanamuzi David Banda 'General Ozzy kutoka Zambia.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Freconic Ideaz, Fred Ngimba (kushoto), akizungumza katika mkutano huo.
Meneja Mawasiliano wa Freconic Ideaz, Krantz Mwantepele (kushoto), akizungumza katika mkutano huo ambapo alisema kampuni yao itaendelea kuleta wanamuziki wengine kutoka pande mbalimbali za dunia kama walivyofanya kwa Robarto Amarula. 

 Mwanamuzi David Banda 'General Ozzy kutoka Zambia (kulia), akizungumza na wanahabari.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo. 

 Mwanamuziki na mtangazaji wa Redio, Roberto Chindaba Banda 'maarufu Roberto Amarula kutoka nchini Zambia, akifanya vitu vyake mbele ya wanahabari.
  Mwanamuzi David Banda 'General Ozzy, akiimba mbele ya wanahabari. Mwanamuziki huyu atamsindikiza Roberto Amarula wakati wa shoo yao.
Mwanamuziki, Clinton Nyirongo kutoka Zambia naye atakuwepo kutoa burudani.
Na Dotto Mwaibale

MWANAMUZIKI wa Zambia anayetamba na wimbo maarufu wa Amarula, Robert Banda ‘Roberto Amarula’, kesho anatarajia kufanya shoo kubwa na ya aina yake katika Ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam kabla ya kufanya hivyo mjini Dodoma kesho kutwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Roberto Amarula, ameahidi kutoa burudanio ya aina yake kwa wakazi wa Dar es Salaam na Dodoma, akiwataka mashabiki wa muziki na burudani kujitokeza kwa wingi kwenye shoo zake hizo.

“Nimefurahia sana kuja Dar es Salaam na ninaahidi kutoa shoo ya aina yake kesho (leo) na Dodoma ili kuwaburudisha Watanzania, lakini pia nitatembelea vituo vya watoto yatima ili kuwafariji na kuwapa nguvu wajione nao ni sehemu ya jamii ya Watanzania na Afrika kwa ujumla,” alisema aliyeambatana na wasanii wenzake wa Zambia, David Banda ‘General Ozzy’ na Clinton Ntirongo ‘Mandela’.

Kwa upande wake, Mkugenzi wa Freconic Ideaz, Fred Ngimba, alisema kuwa shoo ya leo itawahusisha pia wasanii wa Tanzania kama Ben Pol, Roma Mkatoliki, Fred Swag, Msouth na wengine wengi na kwamba onyesho la Dodoma litafanyika kwenye ukumbi wa Ngalawa Pub, ikiwa ni sehemu ya tamasha la Instagram Party.  

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano wa Frecon Ideaz, Krantz Mwantepele, alisema: “Tunafahamu kiu ya Watanzania katika suala zima la burudani ndio maana tumewaletea msanii huyu ambaye kwa sasa ni maarufu mno Afrika na kwingineko tukiahidi kuwaleta wasanii zaidi wakubwa Afrika na hata Marekani ili kukata kiu ya mashabiki wa muziki hapa nchini.”

Ziara ya Roberto Amarula ambaye ni mshindi wa tuzo za uandishi bora, mwanamuziki, mtayarishaji muziki na mtangazaji wa redio, iliyoratibiwa kwa pamoja na Freconic Ideaz na C&G Solutions, imedhaminiwa na Millard Ayo, Morena Hotel, Shabiby Bus Service na Clouds FM.


Thursday, December 10, 2015

RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AUNDA WIZARA MPYA


Nape
Mhe Nape M Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo

 Rais John Pombe Magufuli ameunda Wizara mpya itakayoshughulikia pia wasanii. Katika kutangaza baraza jipya la mawaziri ambalo hakika litakuwa dogo kama alivyoahidi wakati wa kampeni, pia Ria amekuja na Wizara mpya. Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo. Waziri aliyeteuliwa ni Mheshimiwa Nape Moses Nnauye. Kwa wengine tuliomo katika Wizara hii hakika tunaona tunahitaji mabadiliko mengi, yakiwemo uongozi wenye uzalendo wa kupenda utamaduni wa Kitanzania, pia uongozi utakaotengeneza na kuheshimu mtiririko wa uongozi wa kiserikali wa shughuli za Utamaduni. Pia tungependa uongozi ambao unakubali kusikiliza pande zote za wadau wa tasnia ya sanaa. Uongozi ambao utaelewa tofauti kati ya Utamaduni, sanaa na burudani. Uongozi ambao utakuwa wa kwanza kuhakikisha sheria na taratibu zihusuzo sanaa zinafuatwa. Tuna uhakika Mheshimiwa Nape atayaweza haya na zaidi, hivyo kuweza kuweka kumbukumbu ya uwepo wake katika historia ya sanaa ya nchi hii. Bado jina la Wizara linaleta chemsha bongo katika kipengele cha wasanii, je Wizara itahusika na wasanii au Sanaa? Najua inawezekana likaonekana ni swali la ajabu lakini ukukikumbuka tu kuwa kuna wizara ya kilimo sio ya wakulima, au wizara ya biashara na si ya wafanyabiashara, kuna wizara ya uvuvi si ya wavuvi, ni mifano michache ya kuonyesha changamoto hii.