Wednesday, March 10, 2010

Mitindo ya Bendi Zetu

Kuwa na mitindo au staili ya muziki limekuwa jambo la kawaida kwa bendi zetu hapa Tanzania. Zamani mtindo mpya ulikuwa ni mapigo mapya ya muziki au hata uchezaji mpya. Hata bendi ikiwa mpya ulitegemea iwe na mapigo mapya na hivyo kuwa na maana ya kuwa na mtindo mpya. Hii ilifanya upenzi au unazi wa bendi kama ilivyojulikana wakati huo kuwa mkali na unaweza kuelezeka. Ilikuwa hata mwanamuziki akiwa mzuri vipi akiingia kwenye bendi alilazimika kujifunza kwanza mapigo ya bendi yake mpya kabla hajaruhusiwa kutoa nyimbo mpya, hii ilikuwa ni kuratibu mtindo wa bendi. Mitindo ilikuwa tofauti hata uchezaji wake. Wakati nikiwa Vijana Jazz tuliwahi kupiga pamoja na Msondo Ngoma, wakati huo OTTU. Wapenzi wa pande zote mbili walikuwa wanasema wanashindwa kucheza staili ya bendi pinzani. Utakubaliana na mimi kuwa wakati Vijana ikipiga mtindo wa Takatuka ni muziki tofauti na Pambamoto ya Mary Maria au Bujumbura, na ni tofauti na Saga Rhumba ya enzi ya VIP, kwa hiyo majina hayo hayakuja tu , kulikuwa na sababu ya kuyatafuta kuonyesha aina mpya ya mapigo. Majina ya mitindo hii, na uchezaji wake, ulitokana na mambo mbalimbali , mengine yalitungwa na wanamuziki au mengine wapenzi, na mengine vituko mbalimbali vilivyotokea wakati huo. Kwa mfano Bomoa Tutajenga Kesho ya Mambo Bado, ilitokana na sentensi ya tajiri mwenye baa ya Lango la Chuma kutamka sentensi hiyo, wakati wa matayarisho ya uzinduzi wa bendi ya Mambo Bado. hilo. Fimbo Lugoda ilitokana na mwanamuziki mmoja kutandikwa viboko na bibi yake baada ya kukutwa na picha ya mwanamke mzungu. Washawasha ya Maquis ni baada ya steji shoo mmoja aliyekaa chini ya mti kuangukiwa na mawashwasha na kuanza kujikuna. Wadau mna vyanzio vingine vya mitindo ya bendi zenu watu tujikumbushe?