Mitindo ya Bendi Zetu

Kuwa na mitindo au staili ya muziki limekuwa jambo la kawaida kwa bendi zetu hapa Tanzania. Zamani mtindo mpya ulikuwa ni mapigo mapya ya muziki au hata uchezaji mpya. Hata bendi ikiwa mpya ulitegemea iwe na mapigo mapya na hivyo kuwa na maana ya kuwa na mtindo mpya. Hii ilifanya upenzi au unazi wa bendi kama ilivyojulikana wakati huo kuwa mkali na unaweza kuelezeka. Ilikuwa hata mwanamuziki akiwa mzuri vipi akiingia kwenye bendi alilazimika kujifunza kwanza mapigo ya bendi yake mpya kabla hajaruhusiwa kutoa nyimbo mpya, hii ilikuwa ni kuratibu mtindo wa bendi. Mitindo ilikuwa tofauti hata uchezaji wake. Wakati nikiwa Vijana Jazz tuliwahi kupiga pamoja na Msondo Ngoma, wakati huo OTTU. Wapenzi wa pande zote mbili walikuwa wanasema wanashindwa kucheza staili ya bendi pinzani. Utakubaliana na mimi kuwa wakati Vijana ikipiga mtindo wa Takatuka ni muziki tofauti na Pambamoto ya Mary Maria au Bujumbura, na ni tofauti na Saga Rhumba ya enzi ya VIP, kwa hiyo majina hayo hayakuja tu , kulikuwa na sababu ya kuyatafuta kuonyesha aina mpya ya mapigo. Majina ya mitindo hii, na uchezaji wake, ulitokana na mambo mbalimbali , mengine yalitungwa na wanamuziki au mengine wapenzi, na mengine vituko mbalimbali vilivyotokea wakati huo. Kwa mfano Bomoa Tutajenga Kesho ya Mambo Bado, ilitokana na sentensi ya tajiri mwenye baa ya Lango la Chuma kutamka sentensi hiyo, wakati wa matayarisho ya uzinduzi wa bendi ya Mambo Bado. hilo. Fimbo Lugoda ilitokana na mwanamuziki mmoja kutandikwa viboko na bibi yake baada ya kukutwa na picha ya mwanamke mzungu. Washawasha ya Maquis ni baada ya steji shoo mmoja aliyekaa chini ya mti kuangukiwa na mawashwasha na kuanza kujikuna. Wadau mna vyanzio vingine vya mitindo ya bendi zenu watu tujikumbushe?

Comments

Anonymous said…
John
Nakumbuka hata majina ya bedi yalikuwa yanatafutwa kwa njia tofauti mfano tatu nane lilipatika wakati wakitafuta namba ya RTD wakati huo ilikuwa inaaza na 38 kitu fula namna hiyo siha hakika sana na mtindo waliokuwa unatumika maana mpaka band inasambaratika hapakuwata kusikika mtindo wao
mwananjenje said…
Tatunane nijuavyo mimi ni kuwa Kick Van Den Heuvel, yule Mholanzi aliyeisuka bendi hiyo baada ya kuvunjika kwa Watafiti alikuwa mpenzi sana wa UB40, hivyo akaona bendi yake iwe na jina kama UB40 ikawa 38
SIMON KITURURU said…
Hivi kama nakumbuka vizuri ule wimbo BOMOA tutajenga KESHO ulipigwa marufuku naserikali.

Hivi sikuhizi kuna udhibiti wa nini nyimbo zinasema Tanzania?
Swali langu mimi ni kuwa haya MAJINA ya bendi (achilia mbali mitindo) yaliakisi aina ya muziki pigwa?
Mfano Vijana JAZZ band ilikuwa inapiga Jazz? Ama Tancut Almasi ORCHESTRA ilikuwa ikipiga Orchestra ama?
Ni vipi waliamua kuziita bendi zao Orchestra ama Jazz na ni vipi waliweza kuakisi midundo yao kulingana na "jina" lao?
Asante
mwananjenje said…
Kwa kweli neno jazz na orchestra ni mapokeo kutokana na mfumo wa upigaji huu kutokea congo ambako walianza kutumia kiambatisho hicho.Japo Orchestra ni mkusanyiko wa wanamuziki wenye vyombo mbalimbali.
Anonymous said…
TOFAUTI YA JAZZ NA ORCHESTRA NI HII:-
JAZZ;NI MUZIKI UNAOIMBWA NA WAMERIKANI WEUSI TANGU KARNE YA 20.

ORCHESTRA; NI KUNDI LA WATU WAPIGAO MUZIKI PAMOJA
mwananjenje said…
Unaweza kuanzisha ubishi mkali kuhusu tafsiri yako ya jazz
Anonymous said…
John

Naona umesahau bendi zet za bara, Nakumbuka Mwanza kulikuwa na bendi ikiitwa Super Vea Revolution 69 na mtingo wao wa mbujdi, Tabora Jaz na segere matata, mara jazz and the likes. Can you provide an insight to these
Joe
mwananjenje said…
Itakuwa makosa makubwa kuzisahau bendi zote ulizozitaja, sijazisahau natafuta maelezo ambayo yatakuwa na maana kuandika hapa. Super Veya ilikuwa ni sehemu ya Fauvette ambapo iligawanyika makundi kadhaa baada ya kuingia hapa nchini. Super Veya walienda Mwanza na Zaire Success wakifanya makao Moshi. Nani asahau Super Veya na kibwagizo chao maarufu kilichotikisa Mwanza wakati huo....utalia pande zote mamayangu afe, babayangu afe............ au kesi ya Kitenge ya wana sensera toka Musoma