IJUE HISTORIA YA KHADIJA MNOGA-KIMOBITEL

Khadija Mnoga alizaliwa Dar es Salaam maeneo ya Mwananyamala, na kuanza elimu ya msingi Shule ya Mwongozo iliyoko Kinondoni ambako alimaliza 1995, kisha akajiunga na shule ya sekondari Navy Kigamboni. Alipokuwa shuleni alikuwa mpenzi sana wa michezo na wala hakuwa na muonekano wowote wa  kipaji cha muziki. Lakini mwanzoni mwishoni mwa miaka ya 90 akajiunga na kikundi cha CCM cha Chipukizi Mwananyamala ambapo walianzisha kwaya na hapo ndipo kwa mara ya kwanza alijijua anauwezo wa kuimba alipoona watu wanaanza kumsifu. Diwani mmoja wa wakati huo, marehemu Ndege alikinunulia kikundi chake yunifomu na kikawa kikundi rasmi kwenye mikutano yako na ni toka wakati huo akaanza kufaidi kutuzwa  na hata ikafikia anatuzwa laki nzima katika onyesho. Wenzie katika vikundi hivyo vya chipukizi ndio walioanza kupandikiza mbegu ya kuanza kutamani kuimba kwenye jukwaa kubwa, hata Khadija mwenyewe akaenda kumwambia mama yake kuwa anajiona anauwezo wa kuimba kwenye bendi, mama yake hakumuunga mkono lakini pia hakumkataza, kwa maneno ya Khadija mwenyewe, 'Mama aliniangalia tu akacheka'. Jambo ambalo liko wazi Khadija alikuwa na ndoto kamili za nini anataka kufanya katika maisha. Kwanza alikuwa amepanga kuwa hataanza kupiga muziki mpaka atakapopata mtoto, kwani aliamini atakuwa 'busy' sana na akajikuta anazeeka bila mtoto, na hilo alimwambia pia mama yake. Na kama alivyopanga alipata mtoto wake wa kwanza na mtoto alipomaliza kunyonya tu, kama bahati mtu mmoja ambaye alikuwa mpiga ngoma wakati wako kwenye vikundi vya chipukizi, alimfuata na kumwambia kuna bendi inahitaji muimbaji wa kike. Alimkabidhi mama yake mtoto, na kwenda kwenye mazoezi ya bendi kwa mara ya kwanza katika maisha yake bila hata kujua ni bendi gani anayoenda. Alifika kwenye nyumba moja karibu na taa za Jangwani na kukuta bendi ya Shikamoo ndiyo iliyokuwa inahitaji muimbaji. Bendi ya Shikamoo ni bendi iliyoanzishwa mwaka 1994 kwa kukusanya wanamuziki wakongwe waliokuwa wamestaafu. Kwa hiyo Khadija alianza muziki akiwa na walimu kama Mzee Salum Zahoro wa enzi ya Kiko Kids, Capt John Simon wa NUTA Jazz, Mzee Majengo wa Maquis, na wote walikuwa wakifanya mazoezi nyumbani kwa Mzee Nyange aliyekuwa mpiga solo wa Salum Abdallah. Kikweli mwenyewe anasema walipoanza kumuimbisha nyimbo kama Wangu Ngaiye, alidhani wametunga wao kwani hakuwa anazijua kabisa, kwani baba yake wa Khadija alikuwa ni Shehe  ambaye aliiweka familia yake kwa misingi ya dini yake ya Kiislamu hivyo hakukuweko na nafasi ya kusikia nyimbo hizo nyumbani.
 Mababu hawa walimlea vizuri sana Khadija kwani pamoja na kujua kuwa hajawahi kupanda kwenye jukwaa waligundua anakipaji na hivyo kumpa nauli kila siku ya kuja kwenye mazoezi na pesa kidogo ya kujikimu. Wakati akiendelea na mazoezi mpiga bezi wa kundi la Young Star Taarab, wana Segere, alibahatika kumsikia akiimba na moja kwa moja akaenda kuwaeleza wenzie kuwa kuna binti mmoja mdogo lakini muimbaji mzuri ila yuko kwenye kundi la wazee, Segere wakaamua kufanya kila njia kumtoa kwa wazee na kumingiza katika kundi lao. Walimkaribisha awatembelee baada ya mazoezi yake, na Khadija alipokwenda huko akaambiwa kuwa kikundi hicho pia huimba nyimbo za Taarab, Khadija ambaye pia ana asili ya Zanzibar alijisikia nyumbani zaidi katika muziki wa Taarab maana huo hata kwa baba yake ulikuwa  unasikika. Khadija alipofika hapo haraka vyombo vilipangwa na wapigaji wakawa tayari, na akaulizwa anaweza kuimba wimbo gani wa taarab, akawambia kuwa yeye hajawahi hata kuwa jukwaani, lakini akaimba wimbo mmoja uliokuwa maarufu sana Zanzibar wakati huo uliokuwa na maneno haya,'Nafanya kwa raha zangu kwetu sigombwi, na nikigombwa napewa pipi, napewa pesa, na mobitel'. Siku hiyo hiyo wakamkubali na  wakamwambia usiku uleule atalazimu kupanda jukwaani kuanza kazi na kuimba wimbo huo mmoja. Kutokana na kuwa na wimbo huo mmoja tu wa mobitel na hapo ndipo alipopatia jina la Kimobitel......itaendelea

Comments