Friday, May 4, 2012

Muziki si kuimba tu ni zaidi ya hapo


Kwa kuangalia hali inayoendelea katika tasnia ya muziki hapa Tanzania, tafsiri ya muziki ni nini, jibu linaelekea kila siku kuwa  kwa Tanzania muziki ni kuimba. Fungua gazeti, sikiliza redio, angalia luninga, hiyo ndio picha inayoonekana na kusisitizwa.
Kwa kweli kuimba ni sehemu tu ya muziki. Sio siri kuwa katika nyimbo karibu zote ambazo waimbaji tu ndio wanaosifika au kuonekana, muziki uliopigwa na vyombo unachukua nafasi kubwa sana ya tungo hizo, kwa kweli ni jambo la ajabu kwanini waimbaji tu ndio wanaoonekana wanamuziki katika tungo hizo.
Pamoja na kuwa ni kweli kuwa kuna aina ya nyimbo ambao kazi ya kuutengeneza muziki wa ala hufanyika studio kwa kutumia vifaa vya studio, na kwa hiyo muimbaji ndie anakuwa na sifa kubwa zaidi, pia ni muhimu mbunifu aliyetengeneza hizo ala nae pia atambuliwe katika tungo hiyo. Kuna nyimbo nyingi ambazo zimekuwa maarufu kwa kuwa muziki wa ala ulikuwa mzuri, aidha umekuwa ukiwafanya wapenzi wasikilizaji watake kuucheza kila wanapousikia, tena bila kujali muimbaji yupo au hayupo, hivyo umaarufu wa nyimbo nyingine za aina hii hauna uhusiano na muimbaji japo sifa na tuzo zote huenda kwa muimbaji.
Katika muziki wa bendi au vikundi vya taarab, kazi hufanyika kwa umoja toka mwanzo wa tungo mpaka kazi kufika jukwaani. Utakuta utunzi wa maneno hufanyika na mtu mwingine, utunzi wa sauti ya uimbaji hufanyika na mtu mwingine, upangaji wa ala hufanyika na mtu mwingine, na hata uimbaji hufanyika na watu kadhaa. Asipofika mpiga bezi kazi haifanyiki, asipofika mpiga ngoma kazi haifanyiki, lakini bado vyombo vya utangazaji vinafanya kama vile hawa wanamuziki wengine na hata wale wengine ambao humsindikiza mwimbaji mkuu hawana maana, ila muimbaji kiongozi pekee ndie anastahili kutambuliwa!!!. Nyimbo nyingi za bendi au taarabu huimbwa na zaidi ya mtu mmoja ni kizunguzungu kuona  mmoja tu wa hao waimbaji na kuonekana ndie nguzo ya wimbo huo, na mara nyingine hata kuteuliwa kupewa tuzo.
 Umefika wakati sasa, hasa vyombo vya habari kuanza kuwatambua hata watendaji wengine katika tasnia ya muziki.
 Majina makubwa katika muziki zamani hayakutokana na uimbaji tu bali umahiri katika vyombo mbalimbali, kwa mfano Mafumu Bilali-Saxophone, Ally Jamwaka- Tumba, Shem Karenga-Solo, Mjusi Shemboza- Rhythm, Sadi Mnala- Drums, na kadhalika na  hata majina ya vyombo hivi yalikuwemo katika mazungumzo ya watu wa kawaida, jambo ambalo limepotea siku hizi. Kwa mfano ni lini mara ya mwisho uliona au kusikia chombo cha habari kikitaja gitaa la rhythm, au kumuhoji mpiga gitaa hilo? Si sikwamba halipo, wala si kwamba halipigwi, siku hizi  wakati muziki wa taarab ukiingia katika sehemu ambayo huchezesha sana ni mpiga solo kuchukua sehemu ya kupiga gitaa la rhythm, wakati akipiga gitaa hilo ndipo utaona watu wanavyopagawa kwa raha. Bendi  kama Fm Academia, Msondo Twanga, Extra Bongo na bendi karibu zote  zinatumia gitaa hilo, tunawajua wapigaji wake?
Waandishi wa mambo ya muziki wawatendee haki wanamuziki hawa na kuwatoa nyuma ya pazia ambako wametupwa. Pia katika vyombo ambavyo vinatoa tuzo kwa ajili ya muziki, ni muhimu kuangalia mfumo ambao utawapa haki stahili wanamuziki wote bila kujali fani zao.
Kuna kinachoitwa kusaka vipaji kinachoendelea kipindi hiki, mi naona ni shughuli ya kutafuta vipaji vya uimbaji tu , maana hata majaji niliyowaona ni mahiri katika fani ya muziki kutumia mdomo. Vipaji katika muziki ni zaidi ya kuimba.
Kuna vijana wengi ambao wanapenda na wanajifunza ala mbalimbali za muziki, na hapa nisisitize kuwa ninaposema muziki nina maana muziki wa kiasili na muziki huu wa mapokeo, japo ukisoma magazeti na kusikiliza vyombo vya habari utaweza kudhani vijana hawashughuliki tena na kujifunza ala za muziki, hili ni kosa. Binafsi nina wanafunzi wawili waliochini ya miaka kumi na tatu wanajifunza kupiga gitaa tena kwa kutaka wao wenyewe na kuwashikiza wazazi wao wawatafutie waalimu.
Ninachokiona ni vyombo vya habari kuegemea aina fulani ya muziki na kudhani ndio maendeleo au ndio unaoonyesha kuwa na wanamuziki wa nchi hii wanaweza kuvaa kucheza kama wa mataifa yaliyoendelea . Mtizamo huo pengine unatokana na malezi yao, kwa hiyo naona ni wakati sasa viongozi wa vyombo vya habari , ili kuwatendea haki wananchi wengi wengine, walio na kiu cha aina nyingine ya muziki, kufanya jitihada ya kuajiri waandishi na watangazaji wa ziada, ambao kwa malezi yao ni wapenzi wa aina tofauti ya muziki na wale waliopo, kwani ni wazi sioni uwezekano wa mtangazaji aliyebobea katika Bongoflava kuwa na hamu ya kufungua mdomo wake kuongelea utamu wa ngoma ya kabila la wazazi wake kwani hiyo haina swaga.Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo yapata mawaziri wapya

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Dr. Fenella E. Mukangara, Mb.,

Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Ndugu Amos Makala, Mb.,

Changia matibabu ya Sajuki

Waheshimiwa wabunge wametoa track inayoenda kwa jina la "Nimepoteza Mboni Yangu" kwa ajili ya kuhamasisha kumchangia pesa za matibabu msanii Sadiki Juma Kilowoko maarufu kama Sajuki wimbo huu utaanza kusikika katika kituo cha Clouds FM kuanzia kesho.
Watu wanahamasishwa kuchangia kwa kutuma pesa kwenye Account No. 050000003047 AKIBA BANK, jina la mwenye account ni Wastara Juma ambaye ndiye mke wa Sajuki au watume pesa kupitia MPESA No. 0762189592.
Wimbo huu ni maalum kwa Sajuki ambae anahitaji mchango wa hali na mali kuokoa maisha yake. Sajuki anasumbuliwa na uvimbe tumboni na mwezi huu anahitajika kusafiri kwenda nchini India kwa matibabu. Wimbo huu unatoka katika filamu aliyowahi kuifanya na mkewe ya ‘MBONI YANGU.’
Na wimbo huu upo ndani ya filamu hiyo aliuimba Wastara. Umeurekodiwa tena kuhamasishana kuchangia na utaanza kusikika kesho katika kituo cha Clouds FM na video ya tukio zima la kurekodi itaonekana Clouds TV.
Kesho hiyo hiyo Clouds watahakikisha wanakusanya angalau Tsh milioni 12 na wanawaomba sana Watanzania wengine kushiriki katika hili.
Baadhi ya wasanii na waheshimiwa walioshiriki katika "Nimepoteza Mboni Yangu" ni pamoja na Wastara mwenyewe na Vick Kamata, Amini, Barnaba, Peter Msechu, Madee, Rachel, Wema Sepetu, Mzee Yusuph, Pro Jay, Afande Sele, Fid Q, Chid Benz, Linex, Queen Darlin, Shilole, Ali Kiba, William Mtitu, Ester Bulaya, MwanaFA, Halima Mdee, January Makamba ,Zitto Kabwe na Khadija.

Mshindi wa Singeli Michano ya EFM Mwanza apatikana

> Watanzania jana waliadhimisha kumbukizi ya miaka 18 tangu kufariki dunia kwa mwasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Mwl.Julius Kambara...