Tuesday, February 21, 2012

Uchawi katika muziki

Imani ya uchawi ni utamaduni ambao umekuweko katika jamii zote za binaadamu kwa maelfu ya miaka. Historia na maandiko ya dini mbalimbali yanatukumbusha hilo na kulilaani. Huwa inategemewa kuwa kadri maendeleo na elimu yanavyoongezeka ndio imani hiyo inavyopungua na kupotea, lakini ni wazi safari bado ni ndefu kwani ukipita katika mitaa mingi utaona vibao vikiashiria waganga wanaoweza kutibu magonjwa mbalimbali, na hata kutangaza ‘kusafisha nyota’, ‘kuondoa majini’ na kadhalika.
Tasnia ya muziki kwa kuwa ni sehemu ya jamii, haijakwepa kuguswa na tatizo hilo. Kutokana na mimi mwenyewe kufanya kazi katika bendi mbalimbali niliona na kusikia vituko vingi vilivyohusishwa na imani ya uchawi. Mara ya kwanza kuanza kuona vitimbi hivi ‘live’ ni nilipojiunga na bendi moja ambayo ilikuja kuwa maarufu sana wakati wake. Kwa mara ya kwanza nilishuhudia kiongozi wa bendi yangu akiwa na katibu wake wakiwa wanafukiza kwenye radio majani fulani wakati kipindi cha Misakato kikiwa hewani. Misakato kilikuwa ni kipindi kilichokuwa hewani kila Jumanne saa tatu na robo asubuhi, katika redio ya RTD, kikiporomosha nyimbo mpya zilizorekodiwa na pia kutoa maelezo kuhusu wanamuziki walioshiriki. Siku hiyo vibao ambavyo tulikuwa tumerekodi vilikuwa vikirushwa hewani kwa mara ya kwanza, ndipo viongozi wangu hawa nikawakuta wakiwa katika shughuli ya kufukiza radio, kwa imani kuwa kwa kufanya hivyo, vibao hivyo vitatikisa wasikilizaji wake. Baada ya hapo vituko vingi viliendelea hatimae tulimzoea kiongozi wa bendi yetu kuwa ni mshirikina. Kuna wakati aliletwa mganga ambaye alidaiwa aliwahi kuifanya timu moja maarufu ya soka, ishinde kikombe na kuwa bingwa wa Taifa na alichukuliwa kwa mkataba na bendi na kazi yake ikawa ni kukaa mlangoni akijifanya ni muuza machungwa. Yeye alidai kila anapomenya chungwa kwa kuunganisha maganda basi na wateja nao wataingia katika ukumbi kwa kuunganika, huyu alikaa kiasi katika bendi na tukaweza hata kusafiri nae kwenda mikoani. Harakati za bendi kutafuta umaarufu kwa uchawi zilipeleka mpaka bendi ikasafiri hadi kwenda Mpanda, ambako viongozi wa bendi walikwenda kwa mganga na kufanya mambo yao yalioyohusisha na hata kumchinja mbuzi ambaye nadhani masharti yalikuwa ni sisi wanamuziki wote tule kipande cha mbuzi yule wa kafala. Sijajua hatima ya nyama ya mbuzi yule maana wanamuziki walifanya mgomo wa kumla yule mbuzi. Kiongozi wa bendi katika safari hiyo, alichanjwa shingo yote na akawa na mikrofon ambayo wengine wote tulikatazwa kuitumian na sikuona mtu akiigusa mpaka nilipoacha bendi. Ushirikina una matatizo ya kufanya watu wasiaminiane hata kwenye bendi yenyewe, haikuchukua muda mrefu bendi ilipoanza kupoteza umaarufu, Kiongozi wa bendi akaaitisha mkutano na kutuambia kuwa kuanguka kwa bendi kunatokana na mmoja wetu kuiloga bendi, hapo ikatolewa tishio kuwa mtuhumiwa asipojitaja mwenyewe na kuomba msamaha mganga atamfanya awe kichaa. Jambo ambalo liliungwa mkono na wote kuwa kama ni kweli kuna mtu namna hiyo basi apate uchizi. Hakuna aliyekumbwa na tatizo hilo mpaka leo.
Miezi michache baadae, wanamuziki wawili walioamua kuacha bendi walirudisha uniform zao shati zikiwa zimechanywa kwenye kwapa na suruali kuchanywa kwenye maungio ya miguu kwa imani kuwa hizo ndizo sehemu zenye jasho kwa hiyo zingeweza kutumiwa na bendi kiuchawi kuwaharibia maisha.
Katika mizunguko kwenye bendi mbalimbali, nilikuwa katika bendi ambapo siku kukiwa na mpambano wa kupiga bendi zaidi ya moja katika ukumbi mmoja, basi hapo mganga maalumu lazima atafutwe ili kuilinda bendi isimalizwe na wapinzani. Ilikuwa inaaminika kuwa katika mpambano wa bendi, uchawi hutumika kuimaliza bendi ambayo itakuwa haina kinga. Kwa siku hiyo ndani ya spika kuliwekwa tunguli na hirizi mbalimbali tayari kwa mpambano.
Kwa ukweli kabisa hata wanamuziki kutembeleana zamni ilikuwa ni vigumu, kwani ukionekana mwanamuziki wa bendi nyingine katika ukumbi, basi bendi iliyo jukwaani haina raha, anaweza hata akatumwa mtu kufuatilia kila utakachofanya. Na ilikuwa vigumu kuruhusiwa kugusa vyombo vya bendi nyingine kwa wasiwasi wa kuwa unaweza ukaloga kile chombo.
Kulikuwa na hadithi nyingi kuhusu ni kiasi gani bendi ziliweza kufanya ili kupata wateja. Kuna bendi ambayo ilisifika kuwa kila wakimaliza kupiga walipita katika kumbi na kuokota vizibo vya chupa, mifupa, na hata kupata maji toka chooni kwenda kuloga ili wale walioingia wasiingie bendi yoyote kasoro yao. Bendi nyingine zilidaiwa kuwa ziliweka mkataba ambapo zililazimika kutoa kafala ya mtu kila mwaka, hivyo viongozi wa bendi kufiwa na watoto, na hata wanamuziki wageni katika bendi hizo kukutwa na mauti ambayo, kwa chinichini yalidaiwa ni katika kutoa kafala.
Bendi mbili ambazo zilikuwa na upinzani mkubwa katika jiji la Dar es Salaam zilidaiwa hata kutaka kuweka uchawi katika chanzo cha maji Dar es Salaam , na kujikuta wakitaka kuumbuana hadharani kuhusu hilo.
Kama nilivyosema imani ya uchawi huleta kutokuaminiana na hata madhara makubwa ya kutuhumiana mambo ambayo mara nyingi hayana ukweli wowote. Kuna mwanamuziki niliyejaribu kumshawishi aingie katika bendi niliyokuwa nikipigia , alikataa katakata kwa kuwa alidai mmoja wa wanamuziki katika bendi ni mchawi. Mwanamuziki mmoja aliwahi kuhadithia jinsi alivyopita uchochoro wa nyumba ya mwanamuziki mwenzake akashangaa kusikia jina lake likitajwa na mwenzie aliyekuwa chumbani kwake na kusema,’ Nyota ya …….izimike kama kaa hili’, akadai alichungulia katika ufa na akakuta mwenzie anatumbukiza kaa la moto kwenye maji. Ugonjwa wa ukimwi ulipoanza kuuwa wanamuziki kwa mara ya kwanza mara nyingi ulihusishwa na uchawi. Rafiki yangu mmoja nilipomtembelea wakati akiwa hoi kitandani akanambia,’Nikupe siri? Mi ntakufa lakini nauawa na wanamuziki wenzangu kwenye bendi. Nimepata mganga kanitajia na majina kabisa’. Miezi michache baadae mwanamuziki huyu kabla hajafariki alinambia,’Mjomba sijalogwa wala nini, udude huu, unaniua udude’. Alifariki siku chache baada ya kunambia haya. Mungu amlaze Pema peponi Mjomba.
Kitu ambacho kimenishangaza karibuni tuhuma kuwa kuna wanamuziki wa kizazi kipya wanaendeleza imani hii ya ushirikina. Producer maarufu amejitokeza na kuwakanya wasifanye mambo hayo kwenye studio yake. Na siku chache baada ya hapo tena mwanamuziki mwingine wa muziki huo kawataja ambao aliwaita wabaya wake wanaomloga.!!!!!!! Nikaona loh kumbe shughuli bado inaendeleaaaaaaaa

Dar Modern Taarab

Leo nimewatembelea Dar Modern Taarab, wakiwa katika sehemu yao ambayo wanapiga kila Jumanne, pale Copa Cabana Mwananyamala. Wiki ijayo tarehe 2 March 2012, watazindua album tatu kwa mpigo pale Traventine Hotel Magomeni, kwa kiingilio cha shilingi 8,000 tu, na hapo unapata na CD moja. 
Nilipita kuwasikiliza , wanastaili mpya kwa kweli katika Taarab, pia naona wanavyombo vipya kabisa basi muziki ni very clear. Wakongwe Sharif na Mridu naona bado wanapeperusha bendera


Mapacha Watatu Coco Beach

Kila Jumanne, Mapacha Watatu huporomosha rhumba kali pale Coco Beach. Kama kawaida Jumanne ya wiki hii niliwapitia na kupata raha kwa muda. Ni ukweli usiopingika Chokoraa, Jose, Kalala ni waimbaji wazuri sanaTaarifa kuhusu mapatano toka Mh. Joseph Mbilinyi (SUGU)

Kwanza poleni na samahanini kwa hali ya sintofahamu iliyotokea leo kutokana na taarifa za ghafla za usuluhishi kati yetu na Ruge/Clouds FM,ni kutokana na unyeti wa issue yenyewe ilibidi tufanye hivyo kwa nia njema kabisa...kwanza naomba tujipongeze kwa kuwa tukio la leo ni ushindi kwa Vinega kwa maana kwamba madai yetu yote ya msingi ndio yalikuwa msingi wa majadiliano na Ruge amekubali kuyatekeleza yote...kuanzia suala la studio ya Rais kurudishwa kwa BASATA ili iwe ya wasanii wote,pia T,FU ijikabidhi kwa chama halali cha wasanii yaani T.U.M.A kama ambavyo tulikuwa tunadai na mpaka issue za wasanii kunyanyaswa na kubaniwa na pia suala la malipo hafifu vyote vimejadiliwa na kukubaliwa kwa utekelezaji...haikuwa kazi rahisi,kwanza ilianza kwa wao kumpigia Mwenyekiti wangu Mbowe kutaka tukae chini,ambapo Kamanda Mbowe alinishauri tukae nao chini kama kweli wana nia ya kuyamaliza...baadaye wakampigia Mr Shigongo ambaye ni wazi kuwa ni kati ya watu wangu wa karibu naye baada ya kuongea na Mr. Kusaga tu alinipigia na kunishauri hivyo hivyo...na kama haikutosha wakalifikisha hili suala kwenye Kamati ya Bunge ambayo ilinitaka niipe maelezo ya kiini cha mgogoro na nikafanya hivyo ambapo pia baada ya kunielewa wakashauri nikae nao chini...na hatimaye suala hili likaishia mikononi mwa Waziri Nchimbi pamoja na Mhe. Tundu Lissu(MP) kuwa wapatanishi wetu...Waziri Nchimbi akaanza kwa kumuita Ruge Dodoma na alikuja tukakaa kwa hatua ya kwanza na hatimaye leo tukakaa tena makao makuu ya Wizara ya Utamaduni chini ya Dr Nchimbi na Mhe Tundu Lissu na hatimaye tukafikia hatua hii ya leo...vita yetu ilikuwa na hoja hatukuwa tunapigana tu kwa chuki binafsi kama baadhi ya watu walivyokuwa wanajaribu kuiweka,kwahiyo kama hoja zetu zimeeleweka kwa sasa tunatakiwa kushukuru na kufurahia...lakini naomba niwahakikishie misimamo iko pale pale na nimewaweka wazi kuwa anti-virus itaendelea kuwepo ili kuendelea ku-scan virus wengine kama mameneja masoko na wengine watakaojitokeza kwani nchi inaposhinda vita au hata kufikia tu makubaliano ya amani na nchi adui yake haina maana nchi hiyo inavunja jeshi lake...

asanteni sana...


Sugu na Ruge wapatanishwa

Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Mhe. Dr Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Singida Mashariki Mhe Tundu Lisu wamefanikiwa kumaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili kati ya Mbunge wa Mbeya Mjini Mh Joseph Mbilinyi na Mkurugenzi wa Clouds Media Rugemalila Mutahaba


Mshindi wa Singeli Michano ya EFM Mwanza apatikana

> Watanzania jana waliadhimisha kumbukizi ya miaka 18 tangu kufariki dunia kwa mwasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Mwl.Julius Kambara...