Kwa
kuangalia hali inayoendelea katika tasnia ya muziki hapa Tanzania, tafsiri ya
muziki ni nini, jibu linaelekea kila siku kuwa kwa Tanzania muziki ni kuimba. Fungua gazeti, sikiliza redio,
angalia luninga, hiyo ndio picha inayoonekana na kusisitizwa.
Kwa
kweli kuimba ni sehemu tu ya muziki. Sio siri kuwa katika nyimbo karibu zote
ambazo waimbaji tu ndio wanaosifika au kuonekana, muziki uliopigwa na vyombo
unachukua nafasi kubwa sana ya tungo hizo, kwa kweli ni jambo la ajabu kwanini
waimbaji tu ndio wanaoonekana wanamuziki katika tungo hizo.
Pamoja
na kuwa ni kweli kuwa kuna aina ya nyimbo ambao kazi ya kuutengeneza muziki wa
ala hufanyika studio kwa kutumia vifaa vya studio, na kwa hiyo muimbaji ndie
anakuwa na sifa kubwa zaidi, pia ni muhimu mbunifu aliyetengeneza hizo ala nae
pia atambuliwe katika tungo hiyo. Kuna nyimbo nyingi ambazo zimekuwa maarufu
kwa kuwa muziki wa ala ulikuwa mzuri, aidha umekuwa ukiwafanya wapenzi
wasikilizaji watake kuucheza kila wanapousikia, tena bila kujali muimbaji yupo
au hayupo, hivyo umaarufu wa nyimbo nyingine za aina hii hauna uhusiano na
muimbaji japo sifa na tuzo zote huenda kwa muimbaji.
Katika
muziki wa bendi au vikundi vya taarab, kazi hufanyika kwa umoja toka mwanzo wa
tungo mpaka kazi kufika jukwaani. Utakuta utunzi wa maneno hufanyika na mtu
mwingine, utunzi wa sauti ya uimbaji hufanyika na mtu mwingine, upangaji wa ala
hufanyika na mtu mwingine, na hata uimbaji hufanyika na watu kadhaa. Asipofika
mpiga bezi kazi haifanyiki, asipofika mpiga ngoma kazi haifanyiki, lakini bado
vyombo vya utangazaji vinafanya kama vile hawa wanamuziki wengine na hata wale
wengine ambao humsindikiza mwimbaji mkuu hawana maana, ila muimbaji kiongozi
pekee ndie anastahili kutambuliwa!!!. Nyimbo nyingi za bendi au taarabu huimbwa
na zaidi ya mtu mmoja ni kizunguzungu kuona mmoja tu wa hao waimbaji na kuonekana ndie nguzo ya wimbo
huo, na mara nyingine hata kuteuliwa kupewa tuzo.
Umefika wakati sasa, hasa vyombo vya
habari kuanza kuwatambua hata watendaji wengine katika tasnia ya muziki.
Majina makubwa katika muziki zamani
hayakutokana na uimbaji tu bali umahiri katika vyombo mbalimbali, kwa mfano
Mafumu Bilali-Saxophone, Ally Jamwaka- Tumba, Shem Karenga-Solo, Mjusi Shemboza-
Rhythm, Sadi Mnala- Drums, na kadhalika na hata majina ya vyombo hivi yalikuwemo katika mazungumzo ya
watu wa kawaida, jambo ambalo limepotea siku hizi. Kwa mfano ni lini mara ya
mwisho uliona au kusikia chombo cha habari kikitaja gitaa la rhythm, au
kumuhoji mpiga gitaa hilo? Si sikwamba halipo, wala si kwamba halipigwi, siku
hizi wakati muziki wa taarab ukiingia
katika sehemu ambayo huchezesha sana ni mpiga solo kuchukua sehemu ya kupiga
gitaa la rhythm, wakati akipiga gitaa hilo ndipo utaona watu wanavyopagawa kwa
raha. Bendi kama Fm Academia,
Msondo Twanga, Extra Bongo na bendi karibu zote zinatumia gitaa hilo, tunawajua wapigaji wake?
Waandishi
wa mambo ya muziki wawatendee haki wanamuziki hawa na kuwatoa nyuma ya pazia
ambako wametupwa. Pia katika vyombo ambavyo vinatoa tuzo kwa ajili ya muziki,
ni muhimu kuangalia mfumo ambao utawapa haki stahili wanamuziki wote bila
kujali fani zao.
Kuna
kinachoitwa kusaka vipaji kinachoendelea kipindi hiki, mi naona ni shughuli ya
kutafuta vipaji vya uimbaji tu , maana hata majaji niliyowaona ni mahiri katika
fani ya muziki kutumia mdomo. Vipaji katika muziki ni zaidi ya kuimba.
Kuna
vijana wengi ambao wanapenda na wanajifunza ala mbalimbali za muziki, na hapa
nisisitize kuwa ninaposema muziki nina maana muziki wa kiasili na muziki huu wa
mapokeo, japo ukisoma magazeti na kusikiliza vyombo vya habari utaweza kudhani
vijana hawashughuliki tena na kujifunza ala za muziki, hili ni kosa. Binafsi
nina wanafunzi wawili waliochini ya miaka kumi na tatu wanajifunza kupiga gitaa
tena kwa kutaka wao wenyewe na kuwashikiza wazazi wao wawatafutie waalimu.
Ninachokiona
ni vyombo vya habari kuegemea aina fulani ya muziki na kudhani ndio maendeleo
au ndio unaoonyesha kuwa na wanamuziki wa nchi hii wanaweza kuvaa kucheza kama
wa mataifa yaliyoendelea . Mtizamo huo pengine unatokana na malezi yao, kwa
hiyo naona ni wakati sasa viongozi wa vyombo vya habari , ili kuwatendea haki
wananchi wengi wengine, walio na kiu cha aina nyingine ya muziki, kufanya jitihada
ya kuajiri waandishi na watangazaji wa ziada, ambao kwa malezi yao ni wapenzi
wa aina tofauti ya muziki na wale waliopo, kwani ni wazi sioni uwezekano wa
mtangazaji aliyebobea katika Bongoflava kuwa na hamu ya kufungua mdomo wake
kuongelea utamu wa ngoma ya kabila la wazazi wake kwani hiyo haina swaga.
Comments
Abbu Omar Prof. Jnr(Mwanamuziki)Tokyo,Japan.