AWAMU YA TANO;;;KILIO CHA WASANII KILE KILE TOKA AWAMU YA KWANZA

Gazeti la mwezi March 1976
Ni miaka miwili ya awamu hii ya serikali, katika kipindi hiki watu na makundi mbalimbali yanajaribu kuangalia ni nini kimefanyika kuhusiana na kila sekta ambayo mtu au kundi linawahusu. Kama msanii nami najaribu kuangalia kilichotokea katika fani yangu?
Katika sanaa, mambo kadhaa yametokea, katika kipindi hiki tumekuwa na Mawaziri wawili, Mheshimiwa Nape na sasa Mheshimiwa Mwakyembe, pia tumekuwa na  Naibu mawaziri wawili, Makatibu wakuu wawili. Wizara yetu pia imekuwa katika msafara wa kuhamia Dodoma.
Vilio vya wasanii vimekuwa vilevile ambavyo tulikuwa navyo 1987, vilio vya wasanii kulalamika ukosefu wa kulindwa kwa haki zao za  kiuchumi, vilio vya kudai maeneo ya kufanyia kazi za sanaa, vilio vya kudai ruksa ya kulipa kodi, vilio vya kudai punguzo la kodi kwenye vitendea kazi, vilio vya kudai serikali kutengeneza mfumo mzuri wa utawala wa sanaa na utamaduni, vilio vya kudai kurudishwa masomo ya sanaa kwenye ratiba za shule, vilio vya kutaka serikali za mitaa kutenga maeneo ya shughuli za sanaa kwenye kila kata. Kwa kifupi kwa msanii wa kawaida hakuna jipya.
Katika mkutano wake wa kwanza na wasanii ambao walishiriki katika kampeni za uchaguzi, mkutano uliofanyika Ikulu siku ya Alhamisi  February 18 2016,  Rais John Pombe Magufuli alizungumzia swala la wizi wa kazi za sanaa, na wasanii walishangilia pale alipoiagiza TRA kukamata kazi zote zisizo na stika za kuonyesha uhalali wa kazi hizo, hatua ambayo ingeiwezesha serikali kupata kodi yake kutokana na kazi hizo, na wasanii kupata stahiki yao. Haina haja ya kuwa na macho ya ziada kuona kuwa biashara ya kazi za sanaa, za muziki na filamu zisizo halali zinavyoendelea bila kificho. Tukio moja la Waziri kutembelea maduka ya kazi za sanaa zisizo na stika katika eneo la Kariakoo na maandamano ya wasanii chini ya MKuu wa Mkoa wa Dar es salaam yamebakia kuwa matukio yaliyoishia magazetini hakuna mabadiliko yoyote katika biashara hiyo.
Vyombo vya utangazaji ni sehemu moja muhimu ya pato la wasanii kutokana na vyombo hivi kulipia mirabaha kwa kazi mbalimbali zilizotumiwa na vyombo na kuingiza kipato. Vyombo vya utangazaji nchini vikiongozwa na chombo cha utangazaji cha serikali TBC, ambacho kipo chini ya Waziri yuleyule wa wasanii, vyote havilipi mirabaha, kwa lugha nyingine serikali nayo imo katika kuwanyima wasanii haki yao, hakuna dalili zozote kuwa hili litabadilika karibuni.
Kitu ambacho ni nadra kukiona ni sehemu maalumu za wasanii kufanyia kazi zao. Maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa shughuli vijana kwa ujumla yaliwekwa kwa mara ya  kwanza wakati wa ukoloni na baadae yakaongezwa wakati wa awamu mbili za kwanza za uongozi wa nchi hii, karibu yote yamebadilishwa matumizi. Kumbi za maonyesho ya sanaa zimegeuka kumbi za mikutano, na kumbi nyingine kubomolewa na kujengwa sehemu za biashara nyingine, na jambo la ajabu hata kwenye ramani za miji mipya sehemu hizi hazipo, wasanii tunajiuliza hawa wachora ramani wasomi sana, hawajui kuwa sehemu za kutuliza akili ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii? Au kwa wachoraji hawa, sehemu za kutuliza akili ni baa peke yake? Utakuta katika mipango ya miji ramani mpya zinakosa hata sehemu za kucheza watoto, Je jamii mpya ni ya watu wazima ambao hawatakuwa na watoto na pia hawapendi kupumzika? Moja ya haki muhimu ya mtoto ni haki ya kucheza, hivyo ni unyanyasaji pale unaponyang’anya eneo la kucheza watoto au pale ambapo hutengi kabisa eneo la kucheza watoto. Katika awamu ya kwanza na ya pili kulitengwa sehemu nyingi zikiitwa social halls, na kulikuweko na nyingi zilizokuwa zikimilikiwa na Umoja wa Vijana wa CCM. Sehemu hizi ziliwezesha vijana kukutana na kufanya mengi, nyingi ya sehemu hizi zimekwisha geuzwa matumizi na kuwekwa biashara nyingine, na maarufu kama vitega uchumi. Imesahaulika kabisa kuwa sehemu hizi zilikuwa ni sehemu muhimu sana kutega vijana wapya ambao walikuja kuwa wanachama wa kweli wa Umoja wa Vijana.

 Swala la Wizara ya utamaduni kutokuwa na watendaji katika Mikoa na Wilaya ni pengo la wazi katika kukosa wawajibikaji katika utekelezaji wa sera na maamuzi ya Wizara. Mikutano mingi na matukio mengi ya kiserikali yanayohusu wasanii huishia kufanyika Dar es Salaam tu, na hakika ikiwa serikali ina hitaji kubadilisha  hali ya wasanii nchini ni lazima kusuka mfumo ambao utaanzia ngazi za chini, mfumo wa sasa wa Maafisa Utamaduni kuwa Wizara tofauti na Wizara ya Utamaduni kamwe hautasaidia kulinda, kukua na kuendelea kwa sanaa na utamaduni.
Ili kufanya vizuri katika sanaa kwenye dunia hii ya ushindani ni muhimu kuwekeza katika elimu ya sanaa. Mitaala ya elimu hii, kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari ipo lakini imebaki kwenye makabrasha. Muda wa kuhakikisha masomo ya sanaa yanarudi umefika. Kauli mbiu ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda itatekelezeka pia kwa kuangalia kwa upana zaidi mahitaji ya viwanda. Mali zitakazotokana na viwanda zinahitaji pia mkono wa wasanii. Kuna hitajika wachoraji wa kubuni sura mpya za mali zitokana na viwanda vyetu ili kutambulisha utofauti wa mali zetu.
Kama ilivyo kwenye Tanzanite, pamoja na Tanzania kuwa na wachonga vinyago wengi lakini taratibu kuna nchi jirani inaanza kuwa maarufu kwa kuuza vinyago vilivyochongwa Tanzania. Wachonga vinyago wanajikuta wanachonga na kuuza kwa bei ndogo wakati kazi zao zinavushwa kwenda nchi jirani na kuonekana ndio vinatokea huko.

Utamaduni wa kusoma vitabu ni pengo kubwa jingine, hivyo sio tu kutengeneza Taifa lisilo na taarifa kamili lakini pia kufanya shughuli ya uandishi wa vitabu kuwa ni shughuli isiyolipa. Kuna umuhimu mkubwa kuwa na maktaba kila kata kuhamasisha usomaji wa vitabu. Kwa sasa watoto wengi vitabu wanaviona pale tu wakiwa darasani. Tasnia nzima ya utunzi wa vitabu imo katika shimo kubwa, watunzi hawaoni faida ya kuandika vitabu, publishers wanakumbana na matatizo ya wizi wa kazi zao kama vile kazi za muziki na filamu, kodi za karatasi ni kubwa na hivyo wachapishaji nao kukosa kazi. Ni gharama ndogo zaidi kuchapisha kitabu India na China na kukisafirisha kuja Tanzania kuliko kuchapisha kitabu hicho Kariakoo, hii inasababisha viwanda vya uchapishaji vya hapa kwetu kukosa kazi. Nimalize kwa kutoa sehemu ya takwimu zilizotolewa na ripoti iliyoitwa Economic Contribution of Copyright Industries in Tanzania 2007-2010, katika ripoti hiyo ilionyesha kuwa pato lililopatikana kutokana na tasnia ya Hakimiliki katika mwaka 2010 mwaka lilikuwa ni Tsh 680,989,952,456 na tasnia hii iliajiri watu  44,331. Je mwaka huu hiyo takwimu itakuwa imefikia wapi?
John Kitime
Andiko hili limetoka pia kama makala katika gazeti la Mwananchi Jumamosi 11 Novemba 2017. 

Comments