RAIS wa Burundi Pierre
Nkurunziza, ametoa agizo jipya kuhusu upigaji wa ngoma za matambiko na kupiga
marufuku wanawake kupiga ngoma hizo. Pia ameamuru kuwa ngoma hizo za matambiko
kupigwa tu katika shughuli maalumu. Katika agizo lake imeelezwa kuwa ni marufuku mwanamke kupiga ngoma hizo
za tambiko lakini wanawake wanaruhusiwa kushiriki katika kucheza wakati
wakipigiwa ngoma hizo.
Pia amri imetolewa kuwa vikundi vyovyote ambavyo vinataka
kufanya maonyesho ya sanaa hiyo, lazima vijiandikishe Wizara ya Utamaduni na
havitakuwa na ruksa kufanya maonyesho hayo katika shughuli zisizo rasmi.
Ngoma hii ya matambiko ya
Burundi, mwaka 2014 iliwekwa katika orodha ya mali asili za dunia na UNESCO na kuingizwa katika UNESCO’s Intangible Cultural Heritage list, ambapo
ngoma hii inaelezewa kuwa ni muunganiko wa ngoma na kucheza kukiambatana na
mashahiri ya ushujaa, na pia nyimbo za kiasili za Burundi. Kama ilivyo katika nchi nyingi za Kiafrika ngoma hii ya tambiko siku
hizi inachezwa kama burudani, lakini kwa miongo mingi ilikuwa ni ngoma
iliyoabudiwa na kabila zima la Kirundi. Katika siku za karibuni ngoma hii
imekuwa ikichezwa kwenye maharusi, graduation hata ubatizo. Ngoma hii ambayo
awali ilikuwa ikipigwa na wanaume tu, kwa sasa kulianzishwa hata vikundi vya
wanawake ambavyo vilianza kupiga ngoma hii. Kwa tamko jipya kila anaetaka
kufanya onyesho la ngoma hii atalipia $280, na kama onyesho litafanyika nje ya
nchi kiwango hicho kitalipwa kila siku.
Comments