KESI ZA WANAMUZIKI KUIBIANA NYIMBO ZIKO NYINGI DUNIANI HEBU SOMA HIZI CHACHE KWA LEO

Wapenzi wa muziki wa Tanzania wiki hii wamejikuta wakisikia jambo ambalo si la kawaida kwa nchi hii. Wanamuziki kuanza kudaiana fidisa kubwa kwa kuibiana kipande cha nyimbo. Lakini kwa jinsi mambo yalivyokuwa yanakwenda hakika ilikuwa ni muda tu kabla jambo hili halijalipuka, kwa muda mrefu mwanaharakati wa hakimiliki John Kitime amekuwa akitoa mafunzo kuhusu Hakimiliki na hakika jambo hili amekuwa akielezea kuwa iko siku litatokea, kwani nyimbo nyingi maarufu za wasanii hapa nchini zimekuwa zikidokoa nyimbo za wanamuziki wengine bila kujali kutafuta ruksa rasmi, na  sasa Msondo Ngoma Band inataka fidia ya shilingi milioni 300 kutoka kampuni ya Wasafi Classic kwa madai ya matumizi ya kipande cha nyimbo yao bila ruksa. Kwa kawaida kutumia kipande bila ruksa huwa na mambo mengi, kwanza dharau ya kutoheshimu watunzi wa awali, hii huudhi zaidi, pili ndipo linapokuja swala la kudai fidia ya matumizi ya kazi bila ruksa, ambapo anaedai huwa katika nafasi ya kudai fidia kubwa kadri ya anavyoona yeye anastahili kulipwa. Lakini si mara ya kwanza duniani hili linatokea, tena kwa wanamuziki wenye majina makubwa duniani. Hebu tuangalie mikasa iliyowahi kutokea huko Magharibi.
1.      Muimbaji  Ed Sheeran amejikuta akidaiwa fidia ya ya $20milioni kutokana na wimbo wake unaoitwa, wimbo huo unadai kuwa ni wa kujaradia wimbo wa Matt Cardle  unaoitwa Amazing, ulioachiwa mwaka  2009. Amazing uliandikwa na Martin Harrington na Thomas Leonard.  Waandishi hawa kesi yao inashikiliwa na mwanasheria maarufu  Richard Busch, ambaye aliwahi kuitetea familia ya Marvin Gaye katika kesi yao ya kudai haki za wimbo  wa marehemu  Marvin Gaye mwaka 2013. Katika kesi hiyo ya Sheeran, inasemekana  kwenye  chorus nyimbo hizo mbili zinafanana kwa nota 39.  Kwa maelezo yanayosema ‘ the notes are identical in pitch, rhythmic duration, and placement in the measure’. Pia maelezo yaliyopelekwa mahakamani yanasema kuwa  nyimbo hizo. Photograph na Amazing, zimefanana hata katika staili ya uimbaji, melodia ya uimbaji, mapigo au mkong’osio pia vinafanana
2.      Wengi wa wapenzi wa kundi la  Led Zeppelin hukubaliana kuwa wimbo Stairway to heaven ndio wimbo bora wa kundi hilo. Lakini wimbo huo ulilifikisha kundi hilo mahakamani likidaiwa kuwa liliujaradia kutoka wimbo wa kundi jingine. Muimbaji wa  Led Zeppelin Robert Plant, na mpiga gitaa  Jimmy Page walijikuta wako mahakamani wakituhumiwa kuiba wimbo wa Taurus, ulioandikwa na bendi ya Spirit, ambayo iliwahi kufanya maonyesho ya pamoja kadhaa na Led Zeppelin miaka ya 60. Inasemekana wimbo huo umeshaingiza kiasi cha Pauni za Kiingereza  400milioni (wastani wa TSHS 8, 000,000,000/-) kutokana na mirabaha toka wimbo huo ulipoachiwa mwaka 1971. Aliyetunga wimbo wa Taurus, Randy Wolfe alizama mwaka 1997 wakati akijaribu kumuokoa mwanae. Inasemekana aliwahi kusema atawapa wimbo huo Led Zeppelin bila malipo yoyote!!!! Led Zeppelin mpaka sasa wanasema wao hawakukopi huo wimbo.
3.      Kundi maarufu la Beatles liliwahi kusimamishwa mahakamani na kampuni ya Big Seven iliyokuwa iki’publish’ nyimbo za mpiga gitaa Chuck Berry kwa kosa la la kutumia baadhi ya mistari kutoka wimbo wa You can’t touch me wa Chuck Berry na kutengeneza wimbo wao wa Come together. Wimbo wa Chuck Berry ulitungwa mwaka 1956 na kesi ilikuja funguliwa mwaka 1973. John Lennon wa Beatles alikiri kuwa aliuitumia wimbo wa Chuck Berry kumpa hisia tu ya kutunga wimbo wa Come together. Hatimae walikubaliana  nje ya mahakama kuwa Lennon  arekodi nyimbo 3 za kampuni Big Seven.
4.       Do Ya Think I’m Sexy? Ulikuwa wimbo maarufu wa mwanamuziki  Rod  Stewart, lakini alipobanwa aeleze ukweli alikubali kuwa wimbo huo chanzo chake ni  wimbo a mwaka 1979,  Taj Mahal uliokuwa mali ya mwanamuziki wa Brazil Jorge Ben. Ben alipoenda mahakamani Stewart alikubali kutoa sehemu ya pato la wimbo huo kwa UNICEF.
5.   Kundi la Radiohead la Marekani liliachia wimbo lililouita Creep,  lilichukua melody ya wimbo wa  miaka ya 60 wa kundi la The Hollies ulioitwa The Air that I breath, wapenzi wa muziki wakagundua mapema kuwa melody hiyo ni ya wizi, wakawataarifu waandishi wa awali wa wimbo huo, Hammond na Mike Hazelwood. Jamaa wakaenda mahakamani, na ikalazimika wakubaliwe kuwa nao ni sehemu ya watunzi wa wimbo huo mpya na lazima wapewe mgao wa mirabaha.

6.   Rapa Jay Z nae alishtakiwa kwa kuiba vipande vya filimbi vilivyokuwemo katika wimbo wa Khosara  uliorekodiwa mwaka 1957 Misri ukiwa utunzi wa Marehemu Hafez na Hamdy. Jay Z akatumia vipande hivyo kwenye wimbo wake wa 1999 aliouita “Big Pimpin”. Jay Z alishinda kesi hiyo, lakini baadae  yeye na Timbaland walidai walilipia Pauni 66,000 mwaka 2001, kwa kampuni ya EMI Music Arabia ili kupata leseni ya kutumia wimbo huo !!!!!!

Comments