KUNDI LA TAARAB LA G5 LATANGAZA HALI YA HATARI

JINSI mambo yalivyokuwa kwenye shoo ya Jumamosi iliyopita ndani ya ukumbi wa Sisi Club, Msasani, Dar es Salaam limeipa kiburi G5 Modern Taarab kuijinasibu kuwa kundi bora linalochipukia kwenye miondoko ya mipasho.
Hamis Slim ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa G5 Modern ameweka wazi kuwa, wameamua kuvunja ukimya na kuchomoa makucha ili kuwadhihirishia mashabiki wa mipasho kuwa wamekuja kuwashika.
Slim alisema kuwa, wakiwa wanajianda na uzinduzi wa albamu yao ya kwanza baadae mwaka huu, watayatia shoti makundi kadhaa ya mipasho hapa nchini kwa kunyakua baadhi ya wasanii wake mahiri.
Slim alisema kuwa, watafanya hivyo kwa ajili ya kuiimarisha zaidi G5 inayozidi kushika chati kila uchao kwa kuzoa mashabiki kutoka pande mbalimbali hapa nchini.
Tayari wameshafanya mazungumzo na baadhi ya wasanii kutoka katika makundi kadhaa ya taarab yanayotamba sasa ambao wameonyesha kuafikiana nao.
“Ni mapema mno kutaja majina ya wasanii hao na makundi wanayotoka, lakini ukweli ni kuwa, kabla hatujazindua albamu yetu mpya, tutawanyakua wasanii kadhaa wakubwa ili kujiboresha zaidi,” alisema Slim.
Slim alisema, uzinduzi wa albamu yao hiyo mpya, inayokwenda kwa jina la ‘Kigodoro’ utafanyika kabla ya mwezi Oktoba, katika ukumbi utakaotangazwa hivi karibuni.
Baadhi ya wasanii waliopo sasa ndani ya G5 ni pamoja na Mwanahawa Ali, Ashura Machupa, Zena Mohammed, Abdul Misambano na Mwamvita Shaibu.

Yaliojiri Sisi Club
Comments