UNAKUMBUKA KUNDI LA MASS MEDIA? BASI LINARUDI TENA

Zahir Ally Zorro
MASHABIKI wa muziki wa dansi nchini wameombwa kukaa mkao wa kula kusubiri ujio mpya wa bendi ya Mass Media iliyoanzishwa na kuwahi kutamba kwa mwaka mmoja pekee, 2000 kabla ya kuvunjika na wanamuziki wake kusambaratika. 
Ombi hilo limetolewa na aliyekuwa Kiongozi wa kundi hilo, Zahir Ally ‘Zorro’ aliyesema kuwa makao makuu ya Mass Media mpya yatakuwa nyumbani kwake Vijibweni, jijini Dar es Salaam ambako ameandaa sehemu maalum ya kufanyia mazoezi na wanamuziki kupumzika.
“Unajua, nimebakiza miaka isiyozidi 10 tu katika muziki kama Mungu atanijaalia, hivyo ni muhimu kuwaachia mashabiki wa dansi kitu cha ukumbusho kutoka kwa Zorro,” alisema.
Alisema, maandalizi ya Mass Media inayotarajiwa kuanza kambi mwezi ujao yamekamilika kwa asilimia 75, kutokana na kuwa tayari ana seti nzima ya vyombo, huku akitamba kuwa ana wanamuziki wake wa kudumu kutoka katika mikoa mbalimbali nchini.
Zorro alisema kuwa, ujio mpya wa Mass Media utakuwa ni uliojaa wanamuziki chipukizi lakini wenye vipaji na heshima ya hali ya juu, wasiovuta bangi wala kunywa pombe na ambao wataporomosha zaidi muziki wa Rhumba kuliko sebene.
KARIBU TENA MASS MEDIA (Picha kwa hisani ya http://abdallahmrisho.blogspot.com)

Comments