TWANGA PEPETA WAFANYA MAMBO SUNSET CLUB -JET LUMO

USIKU wa jana kuamkia leo ulikuwa ni uliojaa msisimko wa kipekee kwa wakazi wa Jeti Lumo, jijini Dar es Salaam pale wakali wa Kisigino, African Stars ‘Twanga Pepeta’ walipofanya shoo ya kufa mtu, kwenye ukumbi wa Sunset Club.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kampuni ya ASET Entertainment inayomiliki bendi hiyo, Asha Baraka, shoo hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya utambulisho wa wanamuziki wao wapya, nyimbo pamoja na rapu zilizopangwa kuwamo kwenye albamu ijayo.
Ukumbi wa Sunset tangu kuanza kwa shoo hiyo, ulishuhudia namna mashabiki walivyokuwa mara kwa mara wakiviacha viti vyao vikiwa tupu na kujimwaga katikati kucheza kwa mzuka.
Baadhi yao walioonekana kupagawa zaidi walionekana kupigana vikumbo kupanda jukwaani kuwatuza baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiwavutia zaidi.
Vibao vya zamani kama vile; ‘Sumu ya Mapenzi’, ‘Password’ na ‘Safari 2005’ viliwakosha zaidi mashabiki waliokuwa wamefurika ukumbini humo, huku kile kipya kiitwacho ‘Mapenzi Yanauma’, nacho kikipokelewa vizuri kilipotumbuizwa.
Rapa Frank Kabatano aliyejiunga na bendi hiyo hivi karibuni akitokea TOT Plus, ni kati ya wanamuziki waliong’ara vilivyo usiku wa jana, huku pia ‘kiraka’ Kalala Junior ‘akivuruga’ akili za watu kwa kuchanganya rapa za Msaga Sumu kwenye sebeni ya baadhi ya vibao vyao.
Kwa upande wa rapu mpya, ndewe za wapenzi na mashabiki waliokuwamo kwenye ukumbi huo jana, ziliondoka na faida ya kusikia meseji za kisasa za ‘Kantangaze’, ‘Heshima Pesa’ na ‘Ahmada Umelewa’.

Picha za yaliyojiri
Comments