MISAMBANO ALAUMU WENYE BENDI KWA KUSHUSHA HADHI YA MUZIKI WA DANSI

MWIMBAJI mahiri wa kundi la TOT, Abdul Misambano ‘Super Rocks’ yuko mbioni kuvirekodi upya baadhi ya vibao vyake vya Dansi, ili kutekeleza matakwa ya mashabiki wake wanaomuomba kufanya hivyo.
Akizungumza jijini Dar es Salam, Misambano alisema kuwa, hivi sasa anamalizia kutengeneza albamu yake binafsi ya mipasho ambapo baada ya hapo ndipo ataingia kwenye kuvirudia vibao vyake vya dansi.
“Nitakapovirudia vibao hivyo, nitahakikisha siharibu uhalisia ingawaje nitaviongezea ladha na vionjo ili kuvinogesha zaidi,” alisema Misambano.
Alisema kuwa, badhi ya wanamuziki atakaowashirikisha kwenye shughuli hiyo ni wale aliorekodi nao awali TOT, huku wengine wakiwa ni Wakongo wachache.
Baadhi ya vibao vitakavyokuwamo kwenye albamu yake hiyo, ni ‘Mpende Akupendae’, ‘Mnyonge Mnyongeni’, ‘Acha Waone Wivu’ pamoja na kile cha kwanza kukitunga alipojiunga na TOT, ‘Naachia Ngazi’.
Wakati huohuo  mwimbaji huyo, ‘Super Rocks’ amefunguka na kusema kuwa amevunja rasmi ndoa yake na muziki wa Dansi iliyodumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Akizungumza na blog hii, Misambano alisema kuwa, kuanzia sasa atakuwa tu akijihusisha na miondoko ya muziki wa mipasho, huku akifanya shughuli zake nyingine.
“Sina muda tena kwenye Dansi hata nikifuatwa na bendi nyingine kwa dau lolote lile,” alisema Misambano.
Hata hivyo, Misambano alisema kuwa, deni pekee alilobakisha sasa kwenye dansi ni kuvirudia vibao vyake vya zamani alivyoviimba akiwa na TOT Plus Band.
Abdul Misambano  amesema  kuwa muziki wa Dansi umeshuka chati huku akishusha  shutuma nzito kwa wamiliki wa bendi kwa kudai wamechangia kwa kiasi kikubwa kuuporomosha muziki huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Misambano alisema kuwa, nafasi ya wamiliki wa bendi katika kuliporomosha Dansi ipo pale wanapohusika kuwahamisha ovyo wanamuziki na kuvuruga bendi nyingine.
Alisema kuwa, wanamuziki wengi wameshindwa kubaini walipokosea ili kusawazisha makosa yao na badala yake kuishia kutupia lawama kwa vyombo vya habari hapa nchini.
“Hata hivyo, Dansi linaweza kurudi kwenye hadhi yake wakati wowote kwasababu muziki ni mzunguuko, lakini ni vema pia wanamuziki wakajitoa kwenye utumwa wa kuyumbishwa na baadhi ya wamiliki,” alisema Misambano. Picha za misambano kazini hizi hapa.......







Comments