JAHAZI MODERN TAARAB YATEKA NYOYO GADAFFI SQUARE

UKUMBI wa Gadaffi Square, jijini Dar es Salaam, jana uliwaka moto pale kundi mahiri la mipasho, Jahazi Modern Taarab linalotumia mtindo wa ‘Wana Nakshi Nakshi’, lilipokuwa likimwaga burudani ya aina yake.
Onesho hilo lililoonekana kujaa msisimko wa hali ya juu, lilianza kurindima majira ya saa 4:00 usiku na kuendelea hadi saa 9:00, huku mashabiki waliokuwa wamefurika wakijirusha kati kucheza karibu kila kibao kilichokuwa kikitumbuizwa.
Wakati mwingine, baadhi ya mashabiki walikuwa wakinengua hata pale magitaa na vinanda vilipokuwa vikidodoswa peke yake baada ya wimbo kumalizika na kabla ya mwingine kuanzishwa.
Baadhi ya wasanii walioonekana kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki, ni Kiongozi wa kundi hilo, ‘Mfalme’ Mzee Yussuf, Aboubakar Soud ‘Amigo’ na Khadija Yussuf ‘Sauti ya Chiriku’.
Kati ya vituko vya jukwaani vilivyokuwa vikisisimua wengi kwenye onesho hilo  ni mpapasa kinanda Rashid Yussuf kupiga kinanda kwa mbwembwe za upande upande na wakati mwingine kujifanya anasinzia.
Aidha, alipopanda Mzee Yussuf na baada ya kutumbuiza vibao vyake vitatu vya ‘Nani Kama Mama’, ‘Najiamini’ na ‘Wasiwasi Wako’, Mchiriku wa aina yake ulirindimishwa na kuwafanya mashabiki wajisahau na kuanza kunesa kitejateja.
Kwa ujumla onesho hilo lilikuwa zuri kutokana na kufana vilivyo, hasa kwa kuhudhuriwa na mamia ya mashabiki, ingawaje kulikuwa na dosari ndogondogo za fujo za hapa na pale kwa baadhi ya mashabiki waliokuwa wamekolea kinywaji.



























Comments