MAPACHA WATATU NDANI YA MASAI CLUB

MWIMBAJI Januari Mavoko amerejea kwenye kundi la Mapacha Watatu kwa mbwembwe za mkwara mzito wa kutotaka kuajiriwa na badala yake sasa ameanza kufanya kazi kimkataba.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwenye ukumbi wa Masai Club,Kinondoni jijini Dar es Salam ambako bendi hiyo ilikuwa ikitumbuiza, Mavoko alisema kuwa, amejifunza mengi kuhusiana na maisha ya kufanya kazi kwa kuajiriwa.
“Nimerudi kuongeza nguvu kwenye bendi yangu hii ya nyumbani, lakini kwa mkataba maalum, hivyo kama unaenda kuandika kaandike kuwa nimekuja kuzidisha mashambulizi,” alisema Mavoko.
Alipoulizwa kuhusu zawadi aliyowaletea mashabiki wa Mapacha, Mavoko alisema kuwa, amerudi na tungo kali atakayoifyatua hivi karibuni, ambayo itakuwamo ndani ya albamu ijayo ya Mapacha Watatu. Wakati huohuo Mapacha Watatu jana iliitumia fursa ya onesho lao la Masai Club, kutambulisha wimbo wao mpya unaokwenda kwa jina la ‘Kombe Uwanjani’, ambao ni makucha ya Mkurugenzi wa kundi hilo, Khalid Chokora.
Wimbo huo ulioko kwenye miondoko mchanganyiko ya Rhumba na Sebene, ulionekana kupokelewa vema na mashabiki ambao baadhi yao, ulipomalizika walikuwa wakishinikiza urudiwe.
Ndani ya ‘Kombe Uwanjani’ ambao kwa mujibu wa Chokoraa mwenyewe, tayari umesharekodiwa, kuna ujumbe wa mpenzi wa zamani anayepashwa kuwa wakati wake umeshapita hivyo amwache mwenzie atanue na mtu aliyenaye sasa.
“Kibao hicho ni hatua za awali kabisa za mchakato wa maandalizi ya albamu yetu ijayo tutakayoifyatua baadae mwaka huu,” alisema Chokoraa.
Ukumbi wa Masai,ulianza kuonekana mdogo tangu mishale ya saa 6:00 usiku , wakati bendi ya muziki wa Dansi, Mapacha Watatu ilipokuwa ikirindimisha muziki wa aina yake.
Mashabiki wengi walioingia kuanzia majira ya saa 5:30 na kuendelea, walionekana kusimama kwa muda wote kutokana na kukosa viti, jambo lililozidi kuufanya ukumbi huo kuonekana mdogo zaidi hapo jana.
Hakuna aliyejali ingawaje pia kulikuwa na hali ya joto la kiaina lililotokana na kuzidiwa nguvu kwa kiyoyozi humo ndani.
Muziki mtamu wa vijana wa Mapacha Watatu, uliokuwa ukinakshiwa na rapu za Issa Saad ‘Tulanongo’ na Khalid Chokora, uliwafanya mashabiki ‘kusahau shida zao’ kwa kuchizika katikati muda wote.
Waimbaji Jose Mara, Januari Mavoko, Cindy na wengineo, sambamba na wapiga ala wao, walitosha kabisa kuwafanya mashabiki kuiona burudani ya jana kuwa ni ya kipekee. Pata picha za shughuli hapa.........


Comments