PRODUCER MANEKE...MUZIKI UMO KWENYE DAMU YAKE KIUKWELI


MANEKE

MZEE SEWANDO
Mara nyingi sana utasikia mwanamuziki akidai kuwa muziki uko ndani ya damu yake, akiulizwa zaidi unaanza kusikia hadithi isiyo na kiungo kuhusu jambo hilo, katika blog hii hii niliongelea kuhusu Vanesa Mdee na kuelezea jinsi alivyokuwa anafanana kimuziki na baba yake mdogo ambaye sasa ni marehemu ingia VANESSA kwa habari hiyo. 
Leo nitaongelea msanii mwingine kabisa ambaye yeye ni msaada mkubwa kwa wanamuziki wengi wa Bongofleva na jinsi muziki ulivyo kweli kwenye damu yake. Emmanuel Sewando alizaliwa saa 5 usiku mkesha wa mwaka mpya, tarehe 31 Desemba 1988, kwa wazazi ambao walikuwa na uhusiano mkubwa na sanaa. Mama yake ni Afisa utamaduni mpaka leo, wakati  baba  yake Emmanuel, Mzee Sewando, alianza kupenda muziki toka yupo kidato cha pili  katika shule ya sekondari ya Kwiro. Ila kwanza alianza kuwa fundi mitambo wa bendi akapewa jina la The Mad Scientist na wenzie. Mwaka 1969 bendi yao iliweza kurekodi kwa mara ya kwanza RTD ikiwa na mtindo wao wa Mahoka, ambao baadae ulitekwa na Morogoro Jazz na kuja kutumiwa na bendi hiyo 1972. Wakati akiwa fundi mitambo akaanza kujifunza gitaa, mwenyewe anasema baada ya kuona anaweza kupiga vyombo kadhaa vya kiasili kama marimba, filimbi akageukia gitaa, japo hapo shuleni kwao vilikuwepo vyombo vyote vya muziki. Mwaka 1970 akahamia Mkwawa High School ambapo alikuta kuna magitaa ya TANU Youth League bila amplifier, the Mad Scientist sio tu akatengeneza amlifier lakini pia akatengeneza transmitter, ikawa wakati bendi inafanya mazoezi wanafunzi katika mabweni walikuwa wanaweza kusikiliza katika redio zao. Na Mkwawa akendelea sana kupiga gitaa akiwa na wenzie huku akiendelea kuwa fundi mitambo. Lakini turudi kwa mtoto Emmanuel, huyu amekuwa Producer maarufu ambaye amekwisha chukua tuzo kadhaa za muziki, na kuweza kuwatengenezea wasanii chungu nzima muziki, nae anajulikana kwa jina la Maneke wa AM Records. Jina Maneke ni jina la babu yake ambalo kwa sasa limechukua kabisa  nafsi ya jina lake halisi la Emmanuel. Blog hii inasema,Keep up the good work.
 Na habari za uhakika zina sema kuwa mtoto mwingine wa Mzee Sewando nae yuko mbioni kuweka alama yake katika muziki wa hapa Tanzania





Comments