VANESSA MDEE ANANIKUMBUSHA MBALI


Vanessa
Sauti ya Vanessa Mdee ni mpya katika anga la muziki Tanzania, kwangu mimi ni ushahidi mwingine kuwa kipaji huwa kinatembea katika familia. Kwa kweli kilichonifanya nitake kusikiliza  muziki wa huyu binti ni jina hili la Mdee. Mwaka 1972 nilijiunga na Chuo cha Ualimu  Kleruu Iringa, pale chuoni kulikuwa na magitaa mapya kabisa, hiyo ilisababisha wote tuliokuwa wapiga magitaa kujenga urafiki na kukusanyika  kila jioni kwenye kachumba kadogo na kufanya mazoezi, kwa kuwa chuo kilikuwa tayari kina mwaka mmoja tulikuta tayari wananchuo waliotangulia walikuwa wameanzisha bendi, na hapo ndipo nikamuona kwa mara ya kwanza mtengeneza filamu mashuhuri kutoka Tanga Kassim El  Siagi akiwa anapiga gitaa la solo. Kati ya wanachuo tulioingia mwaka huo pia alikuweko mmoja aliyeitwa Yusuph Mdee. Tulipatana mara moja baada ya kujiona wote tunapenda muziki aina moja, haraka tukafanya mpango mpaka kuweza kuishi katika chumba kimoja na magitaa yetu, tulipenda kupiga na kuimba muziki uliokuwa maarufu wakati huo, muziki wa soul, uliokuwa ukitamba wakati huo na wanamuziki kama Otis Redding, James Brown, Percy Sledge, Clarence Carter na wengine wengi. Na pia tulipenda muziki wa bendi wa bendi za Kitanzania zilizokuwa zikipiga muziki wenye uhusiano na huo, kama Afro70, Safari Trippers, Sparks, Commets na kadhalika. Yusuph alikuwa wakati huo ametoka Dar es salaam ambapo aliwa mwanamuziki mzuri wa bendi maarufu ya Upanga iliyokuwa ikiitwa the Groove Makers, ambayo ilikuwa na wanamuziki maarufu  ambao kwa sasa wana nyadhifa nzito serikalini, hivyo sitawataja hapa, lakini sisi tukawa katika mpango wa kujaribu kupiga muziki tulioupenda . Yusuph alikuwa muimbaji na mpigaji mzuri wa gitaa, baadae alijikita zaidi katika uchoraji na hata kufikia kwenda Italy kuendeleza fani yake hiyo, aliishi Arusha kwa muda mrefu akiwa graphic artist na DJ maarufu wa wakati wake, urafiki wetu ulidumu mpaka alipofariki Oktober 1999. Kwa kuufahamu uhusiano wa Vanessa na Yusuph nayaona mambo mengi ya Yusuph katika Vanessa japo sidhani kama Vanesa anaona hivyo kutokana na tofauti kubwa ya umri kati ya Yusuph na Vanessa. Uhakika nilionao ni kuwa ikiwa Vanessa ataendelea na ubora alionao sasa ni wazi akiwa na menejment nzuri atafika mbali sana. Wish you all the best Vanessa 

Comments