Unajiona
una uwezo wa kuanzisha bendi, je uanzie wapi? Pengine nikueleze vitu ambavyo
wanaoanzisha bendi wengi huanza kuviwaza na kuvipanga ambavyo ikiwa uko serious
unataka kuanzisha bendi lazima uvikwepe kama ukoma.
1. Usianzishe bendi ili
kushindana na bendi fulani…..umekwisha kabla hujaanza
2. Usianzishe bendi kwa kuwa
fulani kaweza kuanzisha…umekwisha kabla ya kuanza
3. Usianzishe bendi ili ipige
kama kama Wenge au Franco…umekwisha kabla hujaanza
4. Usianzishe bendi ukategemea
kuwa kwa kuloga bendi itakuwa juu….umekwisha kabla ya kuanza
Bendi
yenye uwezekano wa kuendelea huwa ni bendi iliyoanzishwa na wanamuziki, ambao
wanakuwa na aina ya muziki au ndoto ya muziki wanaotaka kupiga. Mara nyingine
ndoto hii anaweza kuwa nayo mwanamuziki mmoja tu, akiwa anajua kabisa anataka
kupiga muziki wa aina gani atatumia vyombo gani, ataendesha mazoezi vipi,
uwezekano wa kuendelea ni mkubwa
zaidi. Na kama ilivyo miradi mingine ni muhimu anaeanzisha bendi awe na maono
ya wapi atakuwa katika miezi mitatu, sita mwaka, miaka miwili, mitano na
kadhalika. Bendi inayokwenda bila kujua inakwenda wapi hata inapoanza kuangula
huwa haijijui kama imeanza kuanguka. Mpaka hapo utaona sishauri asie
mwanamuziki kuanza mipango ya kuanzisha bendi, kazi hiyo waachie
wanamuziki. Ikiwa unataka kufanya
biashara ya muziki nawe si mwanamuziki angalia nafasi yako katika hili, ingia
katika makubaliano na wanamuziki ili wakulipe kiwango fulani, au asilimia
fulani kwa kila onyesho au kila
wiki au kila mwezi kama vile wafanyavyo wenye magari ya kukodi,hili
litakuondolea kichwa kuuma kuwaza utapata wapi mishahara kodi za nyumba na
kadhalika. Najua hili ni gumu kwani kale kamvuto kakutambulika kama wewe ndie
mwenye bendi kagumu kukakwepa. Kuna watu huingia katika mtego wa kuanzisha
bendi na kupata fedha nzuri wakati wa uchanga wa bendi, baada ya muda wao ndio
kazi yao kubwa inakuwa ni kutoa ruzuku kwa bendi, kwani kuiacha bendi ife
inakuwa ngumu. Ushauri mzuri ni kutokuhangaika kudhibiti fedha za mlangoni bali
kukodisha vyombo au kuingia mkataba wa malipo ya kiwango fulani kwa maonyesho
na wanamuziki, wangapi wenye daladala hukaa kufuatilia konda kakusanya shilingi
ngapi? Ni kupoteza muda kufanya kazi ambazo zina wenyewe. Na mara nyingi
utajikuta unamuweka ndugu achunge kipato, nah ii mara nyingi nimekuta inaleta
matatizo kwani ndugu hawa huwa hawajui mwanzo wa hadithi na hata umuhimu wa
wanamuziki na huamini kuwa bendi ni vyombo, na kuingia katika uhasama mkubwa na
wanamuziki ambao hupelekea kufa kwa bendi……………
Comments