Jioni ya jana ilinikuta nikizunguka sehemu mbalimbali
zilizokuwa na burudani. Niliamua
kuanza safari zangu kwenye shughuli ya kumtafuta Miss Utalii wa Ilala na Kinondoni, shughuli ilifanyika Hotel
Lamada Msimbazi. Nilipofika mahala pa kukatia tiketi nikakuta jamaa 'wanapiga panga’,'wanachakachua', ukiwapa fedha za kiingilio wanakuamrisha uingie ndani bila kukata tiketi,
nikang’ang’ania kupewa tiketi yangu tukaanza kuzungushana, nikaanza kuulizwa
maswali kama nina complementary ticket’, nikawaambia, 'Jamani si nimewalipa alfu
kumi naomba tiketi', ‘We mzee ingia tu’, nilijua mtayarishaji yuko bize huko
akijua kuna watu mlangoni kumbe hakuna kitu, hatimae akaja jamaa mwenye
headphone kama bodyguard akalazimisha nipewe tiketi ikachanwa nikaingia. Japo
katika dakika za mwanzo kulikuwa na ukimya ambao ulikuwa unaleta uvivu, MC alipoingia alianza kuupa uhai usiku wa Utalii. Kwa kweli niliweza kuona
tofauti kubwa kati ya Miss Utalii na Miss Tanzania, nimeipenda zaidi
Miss Utalii kwa kuwa ilikuwa imechangamka zaidi ukiachia kipengele cha
wasichana kujitambulisha ambacho kilichukua muda mrefu sana ukikumbuka kuwa kulikuwa na washindani 26, na pia kule kuhangaika ku ‘cat walk’ ilikuwa ni vichekesho, watoto wa watu kuanza kutembea kama maroboti. Nilipenda sana Uafrika uliokuwemo ndani ya onyesho hilo, muziki wa kiasili
na uonyeshaji wa vipaji kwa kucheza ngoma za kiasili za Kitanzania. Baadae
sikuelewa kwanini aliletwa ‘ Michael Jackson wa Tanzania aliyecheza Thriller
fake, na baadae jamaa waliokuja kucheza Kwaito. Jambo ambalo nategemea litakuwa
somo zuri kwa watayarishaji wa Miss Utalii, ni kuwa wakati washiriki wakipita na
kucheza ngoma za makabila mbalimbali, mabinti ambao kwa mtizamo wa kawaida
wasingejihusisha na muziki wa kiasili, ndio walikuwa msitari wa mbele kucheza
ngoma ya Kihaya, ngoma ya Kingoni, ngoma ya Kizaramo, na tena kuzicheza vizuri sana. Na hawa ndio walipiga kelele
na kudharau Michael Jackson ‘fake’ alipomaliza kucheza. Kweli lilikuwa onyesho
la Miss Utalii. Katika kipindi cha mwezi mmoja nimeangalia maonyesho mawili ya
Mamiss ambayo yenye mlengo wa vipimo vya kizungu, na hili moja lenye vigezo vya kwetu, sina wasiwasi kuwa
nilifurahishwa zaidi na Miss Utalii.
Comments
Ukweli Utabaki kuwa ukweli. Asante wewe ni kielelezo cha ukomavu na hekima katika sanaa.
Ila ndugu yagu ,mti wenye matunda ndio unaotupiwa mawe, mnyama aliye nona ndiye hutegwa na kuwindwa kila kukicha