HONGERA MISS UTALII-ILALA/KINONDONI








Jioni ya jana ilinikuta nikizunguka sehemu mbalimbali zilizokuwa na burudani. Niliamua kuanza safari zangu kwenye shughuli ya kumtafuta  Miss Utalii wa Ilala na Kinondoni, shughuli ilifanyika Hotel Lamada Msimbazi. Nilipofika mahala pa kukatia tiketi nikakuta jamaa 'wanapiga panga’,'wanachakachua', ukiwapa fedha za kiingilio wanakuamrisha uingie ndani bila kukata tiketi, nikang’ang’ania kupewa tiketi yangu tukaanza kuzungushana, nikaanza kuulizwa maswali kama nina complementary ticket’, nikawaambia, 'Jamani si nimewalipa alfu kumi naomba tiketi', ‘We mzee ingia tu’, nilijua mtayarishaji yuko bize huko akijua kuna watu mlangoni kumbe hakuna kitu, hatimae akaja jamaa mwenye headphone kama bodyguard akalazimisha nipewe tiketi ikachanwa nikaingia. Japo katika dakika za mwanzo kulikuwa na ukimya ambao ulikuwa unaleta uvivu, MC alipoingia alianza kuupa uhai usiku wa Utalii. Kwa kweli niliweza kuona tofauti kubwa kati ya Miss Utalii na Miss Tanzania, nimeipenda zaidi Miss Utalii kwa kuwa ilikuwa imechangamka zaidi ukiachia kipengele cha wasichana kujitambulisha ambacho kilichukua muda mrefu sana ukikumbuka kuwa kulikuwa na washindani 26, na pia kule kuhangaika ku ‘cat walk’ ilikuwa ni vichekesho, watoto wa watu kuanza kutembea kama maroboti. Nilipenda  sana Uafrika uliokuwemo ndani ya onyesho hilo, muziki wa kiasili na uonyeshaji wa vipaji kwa kucheza ngoma za kiasili za Kitanzania. Baadae sikuelewa kwanini aliletwa ‘ Michael Jackson wa Tanzania aliyecheza Thriller fake, na baadae jamaa waliokuja kucheza Kwaito.  Jambo ambalo nategemea litakuwa somo zuri kwa watayarishaji wa Miss Utalii, ni kuwa wakati washiriki wakipita na kucheza ngoma za makabila mbalimbali, mabinti ambao kwa mtizamo wa kawaida wasingejihusisha na muziki wa kiasili, ndio walikuwa msitari wa mbele kucheza ngoma ya Kihaya, ngoma ya Kingoni, ngoma ya Kizaramo, na tena kuzicheza vizuri sana. Na hawa ndio walipiga kelele na kudharau Michael Jackson ‘fake’ alipomaliza kucheza. Kweli lilikuwa onyesho la Miss Utalii. Katika kipindi cha mwezi mmoja nimeangalia maonyesho mawili ya Mamiss ambayo yenye mlengo wa vipimo vya kizungu, na hili moja lenye vigezo vya kwetu, sina wasiwasi kuwa nilifurahishwa zaidi na Miss Utalii.

Comments

Anonymous said…

Ukweli Utabaki kuwa ukweli. Asante wewe ni kielelezo cha ukomavu na hekima katika sanaa.

Ila ndugu yagu ,mti wenye matunda ndio unaotupiwa mawe, mnyama aliye nona ndiye hutegwa na kuwindwa kila kukicha