KATIKA miaka ya 60 na 70
mpaka 80, karibu kila eneo la jiji la Dar es Salaam kulikuwa na makundi ya
muziki. Wakati huo muziki ulifanywa kwa makundi tofauti na sasa ambapo msanii
anaweza kuwa peke yake katika kutunga,
kurekodi na hata kufanya kazi yake jukwaani.
Muziki wa dansi uligawanyika katika makundi makubwa mawili, makundi
yaliyopiga muziki wa rhumba na yale yaliyopiga muziki wa magharibi. Kulikuwa na
ushindani mkubwa sana kati ya makundi haya kila mtaa ukijitahidi kupiga muziki bora zaidi ya mwingine. Hata
wazazi nao walijihusisha kuchangia ufanisi wa vikundi vya watoto wao, kwa
kuwanunulia vyombo vya muziki na kuwapa maeneo ya kufanyia mazoezi. Kulikuwa na
ushindani mkubwa sana kati ya vikundi vya muziki kutoka Kurasini na Chang’ombe
na vikundi ambavyo vilitoka Upanga. Ukiliangalia eneo la Upanga leo huwezi
kudhani kuwa lilikuwa eneo muhimu sana katika shughuli za muziki wa vijana,
lakini hakika eneo hili lilikuwa na vikundi kadhaa vilivyokuwa na wanamuziki
kutoka ambao wengi walikuwa ni watoto wa Upanga na wenzao ambao walijiunga nao
wakitoka mitaa mingine. Upanga ni eneo muhimu sana katika historia ya muziki
Tanzania. Enzi hizo vijana walipagawa na muziki wa soul, muziki ambao asili
yake ilikuwa Marekani, muziki ambao uliporomoshwa na wanamuziki kama Otis
Redding, Percy Sledge, Sam Cooke, James Brown, Clarence Carter, Wilson Pickett,
Aretha Franklin na wengi wengine. Vikundi vingi vya muziki vya vijana wa Upanga,
waliiga na kupiga muziki huu, na hata kuamua kupaita upanga, Soulville.
Kwenye kona ya barabara ya Mindu na United Nations, nyumbani kwa
familia ya Jengo, hapo ndipo palikuwa mahala pa mazoezi pa kundi moja maarufu
lililoitwa Groove Makers. Baadhi ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa
Mohamed Maharage, Joseph Jengo na nduguye Emmanuel Jengo, Herbert Lukindo,
Willy Makame, na mpiga Drums ambae mpaka leo yupo katika anga za muziki Habib Jeff
mwanamuziki ambaye toka amejiunga Mlimani Park miaka ya 70 hajawahi kuhama
kundi hilo. Kundi jingine maarufu pale Upanga lilikuwa The Strokers, hili
lilikuwa na awamu mbili, awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald
Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy
Lukindo.
Awamu ya pili ya kundi hili lilkuwa na Sajula Lukindo,Onesmo
Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad, Francis Kasambala,Vicent na
Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. The Barlocks ni
bendi nyingine iliyochipukia Upanga, jina la Barlocks lilitokana na kuweko
kwa kundi jingine lililojiita la The Barkeys, kundi ambalo lipo hai mpaka leo
ambalo kwa sasa linajulikana kwa jina la The Tanzanites, lililo chini ya
Abraham Kapinga. The Barlocks walikuwa wakitumia vyombo
vya Barkeys kwani kwa wakati huo bendi hizi zilikuwa kama mkubwa na
mdogo. Zamani lilikuwa jambo la kawaida kabisa bendi kuwa na makundi
mawili A na B, Dar es Salaam Jazz Band
enzi za Michael Enoch, iliwahi kuwa na Dar es Salaam Jazz Band B, bendi ambayo
ilikuwa na mwanamuziki maarufu Patrick Balisdya. Na bendi hii ikawa bora kiasi
cha kuwa tishio kwa Dar es Salaam Jazz Band A, ikalazimika Michael Enoch
amshauri mwenye bendi kulivunja kundi hilo la pili na kuwaunganisha wanamuziki
pamoja, jambo lililomuudhi Patrick na kuwa sababu moja ya kuanzishwa kwa Afro
70. Barlocks hiyo ya awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Jimmy
Jumba, Pimbi Sokoine, huyu alipewa jina la utani Pimbi kutokana na kuwa mrefu
sana, Said Mbonde kaka yake Amina Mbonde aliyekuja kuwa muimbaji wa kike mzuri
sana pia enzi zake, pia walikuweko Sajula Lukindo na Abraham. Kulikuweko na
makundi mengine mengi hapo Upanga, kama vile White Horse, Aquarius ambako
ndiko alikotoka producer maarufu Hendrico Figueredo, ambaye pamoja na wenzie
walikuja kuanzisha kundi ambalo liko hai mpaka leo linaoitwa InAfrika.
Wanamuziki wengine wa Upanga walikuwa akina Joe Ball, Joel De Souza, Mark De
Souza, Roy Figueredo, Yustus Pereira, Mike De Souza. Kama unavyoona majina yao
hawa walikuwa wengi ni Wagoa, kulikuwa na bendi nyingi za Wagoa katika miaka
hiyo kwani hawa walikuwa ni Waasia wa asili ya kisiwa cha Goa, na lugha waliyotumia
ilikuwa Kiingereza, hivyo muziki waliokuwa wakipiga ulikuwa wa lugha hiyo. Baadhi ya wanamuziki niliowataja walienda na
kuungana na wanamuziki wengine Arusha na kuvuma sana na kundi lililoitwa Crimson
Rage, baadae wakarudi Dar na kujiita The Strange. Leo ukijidai kupiga
gitaa Upanga kuna hatari ukaiyiwa polisi kwa kupigia watu kelele.
Comments