Mara nyingi sana nimeulizwa na kwanini nyimbo nyingi za
zamani bado zinadumu, wakati nyimbo za siku hizi zinakuwa na umaarufu wa muda
na kupotea? Nimeshaulizwa swali hili na
wapenzi wa muziki, watangazaji wa vipindi vya muziki, waandishi wa makala za muziki
na hata wanamuziki vijana wa kizazi hiki
wamekuwa wananiuliza swali hili tena na tena. Labda leo nitoe tena mawazo yangu
juu ya swali hilo. Kuna mambo mengi ambayo ni tofauti sana katika jamii ya
watunzi sasa na watunzi wa zamani, hapa nitaongelea hali ya watunzi wakati nikiwa katika bendi
mbalimbali kati ya mwaka 1975 mpaka 1990. Tofauti ya kwanza kubwa ilikuwa ni
malezi ya awali ya watunzi. Kuna msemo maarufu unaosema ‘msanii ni kioo cha
jamii’. Hivyo basi ukitaka kujua jamii ikoje angalia kazi za wasanii.Tungo za
miaka hiyo zinaonyesha kuwa jamii
ilikuwa na staha katika mambo mengi, jamii ilikuwa bado ni ya watu waliokuwa
watoto au wajukuu wa wazee waliokuwa wanazingatia sana malezi ya kiasili, malezi
yaliyosisitiza kujiheshimu na kuheshimu watu wengine. Hivyo tungo zilikuwa ni
zile zilizokuwa zikijikita bado katika misingi hiyo. Jambo jingine muhimu, kulikuwa
na taratibu rasmi na zisizo rasmi za kurekibisha wale waliopotoka na kukiuka
misingi hii.
Kama nilivyosema nitaongelea miaka niliyokuwa katika bendi,
na kwa kuwa nilipata bahati ya kuwa katika bendi ambazo nyimbo zake bado
zinapendwa na hata kupigwa na bendi za sasa miaka karibu arobaini na zaidi toka
tulipotunga nyimbo hizo. Jambo la kwanza ni tofauti kubwa ya sababu za kuamua
kutunga, ni kawaida kabisa kusikia msanii siku hizi akiasema anataka kutunga
ili’ atoke’. Au anatunga kwa kuwa ‘muziki ni biashara’. Katika utunzi wa namna
hii kunakuweko la lengo linaloongoza aina ya utunzi. Hivyo mtunzi anaweza
kutunga wimbo wa mapenzi lakini nia yake si kuonyesha hisia ya mapenzi bali
kutengeneza wimbo ili uuze au apate umaarufu. Msanii anaweza kutunga wimbo wa
msiba. Lakini hisia yake haikuwa msiba bali ni kutafuta kutoka au kutimiza amri
ya kutunga wimbo wa msiba. Hisia za ukweli ni muhimu katika tungo. Watunzi niliokuwa nikiishi na kufanya nao kazi
wakati huo walikuwa wakitunga wimbo kutokana na mwongozo wa hisia zao tu. Tungo
zilitokana na tukio la kweli au la kubuni lakini kilichowaongoza kutunga
hakikuwa faida au umaarufu bali kutoa hisia zao kuhusu kile walichokuwa
wakikielezea. Msanii ambaye anatengeneza kazi yake kwa hisia , hisia zile
huambukiza kila anaesikia au kuangalia kazi ile. Wimbo ambao mtunzi kaimba
kusikitika husikitisha kila anaeusikiliza, na ule
anaouimba kufurahi hufurahisha kila anaeusikia.
Kwa kuwa muziki wakati huo ulikuwa ni mkusanyiko wa watu
wengi kila tungo ilipitia katika chujio kubwa. Mtunzi ukifikisha tungo yako
kwenye kundi lako, bendi, taarab au kwaya, watu wa kwanza kuanza kuukosoa au
kukusifu walikuwa wenzio katika kundi, kisha
hawa hukusaidia kuuboresha na kila mtu kushiriki katika kuufanikisha, mpiga solo alitunga mapigo yako yake, mpiga
bezi nae, wapulizaji na kadhalika, na kila mmoja alikuwa anauwezo wa kutoa
ushauri kuhusu sehemu yoyote ya wimbo. Hatimae kama kundi hufikia mahali na
kuridhika kuwa kazi yao sasa inaweza kutolewa kwa umma. Katika bendi zote nilizopitia, siku ya
kuupiga wimbo kwa mara ya kwanza ilikuwa muhimu, kwani wanamuziki wote kwa
ujumla mlikuwa na kazi mbili, kwanza kupiga kwa ufasaha tungo yenu mpya na pili
kuangalia washabiki wenu wanaichukuliaje nyimbo yenu mpya. Kama wimbo
haukupokelewa vizuri na mashabiki wenu, ulikuwa unarudi tena jikoni, kuliwekwa hata vikao vya kujiuliza kwanini watu
hawakuuchangamkia wimbo. Na kama ingeonekana kuwa wimbo umefurahiwa na wapenzi
wenu, basi ungeendelea kupigwa kwenye kumbi hata mwezi mmoja zaidi kwa kile
tulichokiita ‘wimbo uive’. Baada ya hatua hii ndipo mipango ya kurekodi wimbo
huanza kufanyika. Na kwa miaka hiyo kulikuwa na chujio jingine, tungo
zilipelekwa mapema Radio Tanzania ambako ndiko kulikuwa na studio za kurekodi,
na huko kulikuweko na kamati iliyokuwa ikiangalia kama tungo zimefuata maadili
yaliyokuweko wakati huo. Tungo zilizopita chujio hilo ndizo zilizorekodiwa. Na
hakika ndizo nyimbo ambazo zingine zina miaka zaidi ya hamsini lakini zinafurahiwa na wapenzi wa
muziki wa rika zote hadi leo.
Kwa utaratibu wa
sasa, ni kawaida msanii kutunga wimbo wake chumbani kwake peke yake, kisha
akaingia studio, wakawa watu wawili yeye na producer wake na kutengeneza wimbo
ambao ukitoka hapo unapelekwa redioni tayari kwa kurushwa kwa umma. Lakini
katika zama hizi ambazo kwanza kuna tatizo kubwa la malezi, ambapo si ajabu
kusikia mzazi akimtusi mwanae wa kumzaa kwa matusi ambayo kimsingi anajitukana
mwenyewe, mtaani watoto wanakua wakisikia lugha za ajabu na hakuna mtu
anaonekana kushtuka, hakika msanii aliyekulia katika mazingira haya na kwa kuwa yeye ni ‘kioo’ cha jamii yake, kazi
yake si ajabu kabisa unapokuta akiongelea mambo ambayo mtu mwingine unastaajabu
kapata wapi ushujaa wa kutamka maneno ya faragha bila ukakakasi mdomoni. Kazi
za namna hii ni nadra sana kuwa na maisha marefu
Comments