MUZIKI na filamu ni ndugu, japokuwa muziki ulikuweko kabla
ya filamu. Filamu za kwanza zilipoanza kutengenezwa, kulikuwa hakujagundulika
utaalamu wa kuunganisha picha na sauti, hivyo sinema hizo za kimya kimya za awali
za kati ya mwaka 1895 hadi 1927zilijulikana kama kama ‘silent films’. Filamu
zilitumia mabango yaliyoandikwa maneno kuonyesha nini muigizaji alikuwa akisema
Nyakati hizo wanamuziki walikodishwa kupiga muziki wakati filamu inaonyeshwa,
baadae kukawa kunatumika gramophone, chombo ambacho ni cha kupiga santuri za muziki
wakati filamu inaonyeshwa. Filamu za kwanza kuunganishwa filamu na sauti
zilianza mwaka 1930 na ziliitwa ‘talkies’ au ‘talking pictures’. Teknolojia
hiyo ikafungua uwanda mpana wa matumizi ya muziki katika filamu. Muziki
ukaendelea kutiliwa umuhimu mkubwa katika utengenezaji wa filamu bora, na
katika filamu zote kuna kuweko na msisitizo maalumu kuhusu aina ya muziki
utakaosindikiza filamu. Muziki hufanya kazi muhimu sana katika filamu, husaidia
kuongeza hisia ya tukio, husaidia kuhadithia tukio, nakadri muziki ulivyo bora
ndivyo na utamu wa filamu unavyozidi. Uhusiano huu wa muziki na filamu uliendelea kukua kiasi cha
kuweza kusaidiana kukua kwa tasnia hizi mbili. Filamu ikaweza kupata umaarufu
kutokana na muziki mzuri au muziki ukaweza kupata kupata umaarufu kutokana na ubora
wa filamu. Kuna mifano mingi ya jambo hili katika filamu za kihindi, ambazo
zimejijengea umaarufu mkubwa katika kuunganisha tasnia za muziki na filamu.
Watu wengi wanazifahamu nyimbo kama Kuch kuch hota hai (filamu Kuch Kuch hota
hai) , Kabhi kabhi Mere Dil Mein (filau Khabi Khabi), Goro ki na Kalo ki(
filamu Disco Dancer) na nyimbo nyingine nyingi ambazo ni nyimbo zilizokuwa
katika filamu mbalimbali za Kihindi na mara nyingine kuzifahamu nyimbo bila
hata kujua filamu husika. Nyimbo hizi zimefanya filamu zipendwe zaidi, na
hakika filamu zimewezesha nyimbo hizi kuingiza fedha nyingi. Fursa hii ilisomwa
vizuri na tasnia ya filamu ya India Bollwood na mapema kabisa Wahindi walijenga utamaduni wa kutengeneza
filamu nzuri za utamaduni wao, ambazo ziliambatana na muziki ulitungwa na
kupigwa na kuimbwa na kati ya wanamuziki bora waliowahi kutokea India, waimbaji
wa kike kama Lata Mangeshka na dada yake Asha Bhosle, waimbaji maarufu wa kiume
akina Mukesh, Mohammed Rafi na wengineo waliweza kurekodi maelfu ya nyimbo
ambazo waigizaji walizitumia na kuonekana wanaimba katika filamu zao na kupata
umaarufu duniani kote, watu wengi ambao hawakujua hata maana ya neno moja la
Kihindi walijikuta kuwa mashabiki wakubwa wa filamu za Kihindi. Lakini hebu tuangalie hali ya uhusiano
kati ya tasnia ya filamu na muziki hapa kwetu. Pamoja na kuwa tasnia hizi bado
ziko chini sana katika ramani ya ulimwengu, hakuonekani mpango wowote wa kuunganisha
nguvu ili kupata faida ya pamoja. Katika kipindi cha karibuni watu muhimu
katika tasnia ya filamu wamekuwa wakionyesha wazi wazi kuwa tasnia hiyo ni
muhimu kuliko tasnia ya muziki na hakika kudai ni muhimu kuliko tasnia nyingine
za sanaa. Filamu na muziki zina mambo mengi ambayo ni ya pamoja. Sheria
zinazoongoza muziki ni zilezile zinazoongoza filamu, matatizo ambayo sekta ya
filamu inayapata sasa ni yale yale ambayo sekta ya muziki imeyapitia. Biashara
ya kuuzwa kwa kazi haramu za ndani na za nje ndizo zimeua biashara ya kuuza
kazi za muziki, rushwa katika tasnia hizi ni kutoka watu wale wale, si busara
kabisa tasnia hizi kutengena. Ningeshauri sana kwamba tasnia hizi mbili
ziangalie na zijifunze kutoka India kwa hili. Nchi hiyo imejenga tasnia za muziki
na filamu kwa misingi ya utamaduni wa nchi yao. Na kwa kutumia raslimali hii
muziki na filamu kutoka nchi hii zimekuwa za kipekee na kuweza kusambaa dunia
nzima. Wasanii wenye hofu na ubora wa utamaduni wao huona utamaduni wa nchi
nyingine ni bora na kuamua kuuiga kwa nguvu zote na kwa daima hubakia kuwa kivuli cha wenye utamaduni ule.
Filamu na muziki wetu ni mfano mkubwa wa uoga huu, wa kudhania tusipofanya kama
wengine tutakosa ‘soko la kimataifa’, kazi zetu za sanaa zinaiga tungo,
maudhui, na hata vitu vya kawaida kama mavazi, kuiga sio dawa ya kupata kazi bora bali ni njia ya kutengenza
soko kwa unaowaiga. Swala la kupata faida kutokana na kazi za filamu na muziki
hakika ni jambo muhimu sana, lakini biashara isiruhusiwe kuondoa Utanzania
wetu. Hapa sasa ni nafasi ya serikali, nchi zote ambazo zina maendeleo katika
kazi zake za sanaa zimeweka sheria ya
kipengele muhimu
kinachoitwa ‘local content’. Hii ni sheria inayoelekeza ni kiasi gani
cha kazi za nje kitatumika katika vyombo vya utangazaji kama TV na redio, kwani
vyombo hivi ni muhimu sana katika kujenga tabia za wananchi. Ni muhimu sasa
kulazimisha kipengele hiki ili kubadili mwelekeo wa kizazi kipya na kijacho cha
Watanzania.
Comments