Talent Manager au pia anayejulikana kama Artists Manager au
Band Manager, ni mtu au kampuni
mwenye kazi ya kumuongoza msanii katika taaluma yake. Pia kazi yake ni
kufuatilia biashara za msanii kila siku na kutoa ushauri na muongozo kuhusu
mipango ya muda mfupi na mrefu ya msanii na hata maamuzi ya kibinafsi ambayo
yanaweza kuathiri kazi ya msanii, kama vile tabia za matusi, ulevi, uchelewaji
kazini nakadhalika. Meneja humsaidia msanii kupata Talent Agent na hata
kushauri kuachana na agent aliyepo, Meneja pia kazi yake kubwa ni kutoa ushauri
kuhusu maonyesho, promotion, mikataba mingine ya kibiashara, mikataba ya
kurekodi na kadhalika.. Agents ndio wanaoingia mikataba kwa niaba ya wasanii,
meneja huwa mshauri tu wa mikataba hiyo.
Meneja mara nyingi huajiriwa na Bendi au mwanamuziki, au mara
nyingine meneja hugundua kipaji cha mwanamuziki na wakaanza mahusiano ya msanii
na meneja, mahusiano haya kwa kawaida huhalalishwa kwa mkataba wa maandishi
ambao hueleza wazi mipaka na majukumu ya meneja na mwanamuziki kwa upande wake.
Kwa kawaida meneja hulipwa kwa kamisheni, hii kwa kawaida huwa kuanzia 15% ya mapato ya msanii yaliyotokana na
juhudi za meneja, kwa meneja mzuri kazi zote za msanii huwa zimepitia mikononi
mwake. Nimeona leo niongelee kuhusu mameneja bada ya hasa kusikia vituko vya
mameneja wa wanamuziki fulani maarufu wiki chache zilizopita, ambao
waliwakosesha wanamuziki wao nafasi ya kushiriki jukwaa moja na wanamuziki wa
jazz wenye heshima kubwa katika muziki wa jazz duniani, kwa kudai vitu ambavyo
haviwezekani.
Maquis Original |
Bendi nyingi zilianza kwa kuwa na aliyejulikana kama Katibu wa
bendi, huyu kimsingi alikuwa akifanya kazi nyingi za meneja wa bendi, ila
alikuwa mmoja wa wanamuziki, ambaye pia alifanya shughuli ya Ukatibu wakati wa
mikutano ya bendi, hakuwa na mkataba tofauti na wanamuziki wenzie ila mara
nyingi alikuja kuwa na nguvu sana kwa kuwa yeye ndie aliyekuwa na maamuzi mengi
ya matumizi ya pesa za bendi.
Karibuni
kumekuweko na taratibu za bendi kuwa na mameneja ambao wengi hulipwa mshahara, lakini kazi zao haziko
sawa na mameneja wengine wa muziki duniani, maana mara nyingine ni vigumu
kutambua nani mkubwa kati ya meneja na mwanamuziki, ambaye kimsingi ndie
muajiri wa meneja.
Wiki chache zilizopita kulikuweko na Tamasha la muziki wa
Jazz, wanamuziki wenye uzoefu mkubwa walikuwepo hapa nchini, japo ni wazi promo
ya Tamasha hilo aidha haikuwa nzuri, au ililengwa kwa kundi fulani la
Watanzania tu kwa hiyo wengi hawakulijua, hata wanamuziki wengi wapenzi wa Jazz
na wapigaji wa muziki wa jazz, hawakuwa na taarifa kuhusu tamasha la Jazz
ambalo lilikuwa likiendelea jijini Dar es Salaam. Hata hivyo nilipenda kuwaasa
wanamuziki kuwapa semina mameneja wao kuwa katika maendeleo ya muziki si kila
mara lazima udai malipo. Leo hii mwanamuziki kuambiwa ufanye onyesho na
mwanamuziki ambaye amekwishafanya kazi na wanamuziki walio katika ngazi za juu
za muziki duniani ni muhimu, inasaidia kupata uzoefu na kujifunza mengi mapya,
na pia huwezi kujua matokeo ya
kukutana huko. Mameneja kadhaa walikataza wanamuziki wao kupanda jukwaani na
wanamuziki waliokuwa nchini kutoka Marekani na Afrika ya Kusini, sina uhakika
kama wanamuziki wenyewe wangekubaliana na uamuzi huo wa mamenjea wao. Meneja
anatakiwa aangalie faida za onyesho kwa muda mrefu na si kujali laki mbili ya
mara moja ambayo inamdhalilisah mwanamuziki.
Comments