VITA VYA HAKI ZA WASANII VILIANZA TOKA MIAKA YA 80


VITA  ya wasanii kudai ulinzi wa Hakimiliki za kazi za sanaa haukuanza leo na nia ya kuandamana sio mpya kabisa, ila wiki hii yamefanyika kwa mara ya kwanza na mambo yasiporekibisha haitakuwa mara ya mwisho wasanii kuandamana. Wanamuziki wa Tanzania walianza kudai Hakimiliki mwishoni mwa miaka ya 80. Hali hii ilijitokeza baada ya teknolojia ya kanda za kaseti kuanza kuenea, na ilisababisha kwa mara ya kwanza kazi za wanamuziki kuwa rahisi kurudufu na kuanza kuuzwa bila ruksa yao. Kabla ya kipindi hicho, wanamuziki waliotaka kuuza nakala ya nyimbo zao walilazimika kuvuka mpaka na kuingia Kenya ambako kulikuwa na kampuni kadhaa ambazo zilikuwa na viwanda vya kutengeneza santuri. Ujio wa kanda za kaseti uligongana na kipindi ambacho mpaka wa Tanzania na Kenya ulikuwa umefungwa kutokana na migongano ya kisiasa kati ya nchi mbili hizi, kwa kuwa santuri zilikuwa zikitengenezwa Kenya ikawa ni vigumu kupata santuri hizo, santuri chache zilikuwa zikiingia nchini kupitia njia za panya na nyingine chache kupitia maduka ya umma ya Regional Trading Company (RTC), kwa ujumla kulikuwa na uhaba wa kazi za muziki. Hivyo basi wafanyabiashara wenye akili za haraka wakaanza kurudufu nyimbo maarufu na kuziuza kwa njia ya kaseti. Biashara hiyo iliweza kukuwa na kufikia nchi hii kuwa na mitambo iliyoweza kutoa maelfu ya kanda kwa muda mfupi, kanda ambazo zilisambazwa kote nchini na hata nchi jirani, kwa kuwa nyingi za kanda hizi zilikuwa zimerudufiwa bila ruksa ya wenye nyimbo hata nchi jirani zilianza kulalamika kuhusu biashara hii haramu ambayo Tanzania ilikuwa kinara, Afrika Mashariki na Kati. Hadithi za wanamuziki kama Defao kuanguka kilio baada ya kuingia kwenye duka moja na kukuta kazi zake zikiuzwa bila yeye kujua na hata mwanamuziki Fan Fan wa Orchestra Somosomo kumlamba kibao mfanya biashara mmoja, au Mbilia Bel kuanza kuzurura kwenye maduka na kudai malipo ya papo kwa papo zilijitokeza kwenye magazeti wakati huo. Harakati za wanamuziki kudai sheria bora ya Hakimiliki zilizaa matunda mwaka 1999, ambapo sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki no 7 ya 1999 ilipitishwa na Bunge. Mwanzoni mwa 2000, Chama cha hakimiliki cha Tanzania (COSOTA) kilizaliwa na Waziri wa sasa wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr Harrison Mwakyembe akawa mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya  chama hicho. Pamoja na juhudi hizi za kwanza kuna kila dalili kuwa serikali na jamii kwa ujumla haijawahi kuona umuhimu wa ulinzi wa Hakimiliki.  Inawezekana jambo kubwa linalofanya serikali kutokuona umuhimu wa Hakimiliki ni kwa sababu ya kutokujua faida za hakimili kwa wasanii, sanaa, utamaduni, jamii na serikali yenyewe, na hivyo kuziba masikio hata ya kupewa elimu kuhusu swala hili. Wabunge pia wanastahili kubeba lawama kwa hili kwani nao wamekuwa wagumu kutaka kuelewa kwa undani kuhusu sheria hii na hivyo pale wanapokuwa na nia ya kusaidia ‘wasanii’ huongea kwa wepesi sana hoja zao kuhusu Hakimiliki. Labda nitoe mfano rahisi wa kuonyesha umuhimu wa ulinzi wa Hakimiliki. Ripoti ya World Intellectual Property (WIPO) ya Mchango wa Tasnia ya Hakimiliki katika Uchumi wa Taifa (2012) iliyoitwaThe Economic Contribution of Copyright-Based Industries in Tanzania, ilionyesha kuwa katika mwaka 2009, himaya ya Hakimiliki iliingiza jumla ya shilingi 676,458,324,498/-. Ripoti ilionyesha pia kuwa mchango wa asilimia katika pato la taifa GDP ulikuwa ni 4.6%, mwaka huohuo pato kutokana na madini lilikuwa ni 2.5%. hakika wote tunajua jinsi shughuli za madini zinavyoangaliwa kwa jicho makini, na kila siku tunasikia ripoti za kuboresha mikataba yake, serikali, Bunge, wananchi wote wako makini sana na madini lakini hesabu ndio hizo. Hizo zilikuwa hesabu za 2009, ni miaka 7 imepita na ripoti hii iko Wizara ya Viwanda na Biashara, lakini COSOTA ambayo imepewa jukumu la kusimamia Hakimiliki haijapewa uwezo wa kufanya lolote kuhusu kuratibu mapato haya makubwa. Ukwepaji mkubwa sana wa kodi na udhulumati mkubwa wa haki za wasanii unaendelea bila kushughulikiwa, matokeo ni kurudi nyuma kwa ubora wa kazi za sanaa nchini wakati dunia nzima wasanii wanaenda mbele. Mwaka 2006 Wizara ya Viwanda na Biashara iliweza kutunga kanuni iliyolazimisha kazi zote za muziki na filamu kuwa na stika zilizoitwa Hakigram, serikali haijawahi kutoa fedha za kuwezesha stika hizo zianze kufanya kazi. Lakini mwaka 2007 ikatungwa kanuni nyingine ya Wizara ya fedha ikilazimisha kazi za muziki na filamu kuwa na stika za TRA, kanuni hii ya pili ilikuja pitishwa bila utafiti wowote, japo kila mara kumekuwa na taarifa kuwa ‘Ikulu’ iliyoa shilingi milioni 20 kwa mtafiti kutoka ‘Chuo Kikuu’ ili kufanya utafiti uliopelekea kutungwa kwa kanuni hizo, hakika mtafiti huyo’ kama alikuweko’ angejua kuwa kuna stika tayari hivyo cha kufanya pemngine ingekuwa kuiboresha stika hiyo, kimsingi kwa sasa kisheria kila kazi ya muziki na filamu inatakiwa iwe na stika mbili!!. Mheshimiwa Rais wa awamu ya awamu ya nne alirudia zaidi ya mara moja taarifa ya Ikulu kutoa fedha kwa ajili ya mtafiti. Lakini mpaka leo, hiyo ripoti haionekani, mtafiti hajulikani na hakika stika za TRA utekelezaji wake ni Dar es salaam tu na kwa kazi za filamu na muziki za Tanzania tu, na wizi wa kazi za sanaa unazidi kushamiri na kugeuka utamaduni wa Watanzania.
Katika nchi zilizoendelea Hakimiliki ni moja ya misingi  wa maendeleo na eneo kubwa la pato la Taifa. Kila mara viongozi wetu hutoa mifano ya nchi kama Korea ya Kusini, wakieleza kuwa Tanzania na nchi hiyo tulikuwa sawa kwa kimaendeleo miaka ya 60 na sasa ni moja ya nchi zilizoendelea sana, moja ya nguzo kuu za kuendelea kwao ni kuzingatia haki za wabunifu, walijenga misingi imaa ya kulinda na kuendeleza ubunifu. Katika zama hizi ambazo Tanzania inataka kuwa nchi ya viwanda, ni muhimu sana misingi ya kulinda ubunifu kuimarishwa, labda kama nia ya viwanda vyetu ni kutengeneza mali ambazo zina Hakimiliki za wabinifu kutoka nje ya nchi. 
Wiki hii kumekuweko na harakati za kudai haki hii, bahati mbaya wajanja wamegeuza mada na kuonekana wasanii wanataka kuzuia kazi kutoka nje, huu ni ujanja ili wezi wapate kuungwa mkono na jamii. Kinachodaiwa hapa ni kuwa sheria na taratibu zifuatwe kwa kazi zenye hakimiliki iwe ni za wabunifu wa ndani ya nchi au nje ya nchi, Tanzania ilisaini mkataba wa Berne Convention mwaka 1994 ambao unailazimu kulinda hakimiliki za wabunifu wa nje kwa nguvu sawa na wabunifu wa ndani. Ulinzi wa Hakimiliki ni muhimu katika kulinda na kuendeleza kazi za sanaa za jamii na ni nguzo muhimu katika kulinda na kuendeleza utamaduni wa Taifa.

Comments