PICHA KWA HISANI YA MICHUZI BLOG |
Pole
muziki wa Tanzania. Pole muziki wa Tanzania uliojitahidi sana kwa miaka mingi
kuondokana na dhana kuwa muziki ni uhuni, pole muziki wa Tanzania uliopata kuwa
na ushiriki wa nguli kama Marijani Rajabu, moshi William, Muhidin Gurumo, Bi
Shakila, Rahma Shally, Jerry Nashon, Raphael Sabuni, David Musa, Patrick
Balisdya, na orodha ndefu ya wanamuziki ambao kazi zao zinaheshimika miaka
mingi baada ya kutangulia mbele ya haki. Pole muziki wa Tanzania ambao ulikuwa
mstari wa mbele wakati wa kupigania uhuru na wanamuziki kama Frank Humplink na
dada zake, Salum Abdallah na wenzake, pole muziki wa Tanzania, ambao kwa miaka
mingi baada ya Uhuru ulikuwa darasa kwa Watanzania katika kuelimisha kila nyanja
ya maisha ya Mtanzania kuanzia siasa, kilimo, ukombozi wa Afrika, na hata afya
na chakula bora. Pole sana muziki
wa Tanzania uliokuwa ukitungwa kwa usanifu ili kila mtu mkubwa na mdogo aweze kuburudika
na kujifunza mema. Pole ua lililokuwa likitoa harufu nzuri kwa wasikilizaji
wote wa Kiswahili, hapa nyumbani na duniani kote. Pamoja na pole zote hizo hakika
wanamuziki wa zamani huwezi kutamka kuwa walikuwa malaika wa tabia, la hasha,
lakini walilelewa wakijua nini cha kutamka hadharani, hata pale walipoudhiwa sana
au walipofurahishwa sana, tungo zao zilifikisha ujumbe bila kutumia lugha
isiyoweza kutamkika katika hadhara ya mchanganyiko wa rika. Muziki sasa umejaa
wajuzi wa kutunga tungo zilizojaa ukakasi wa maneno na mawazo, unaokufanya
ujiulize mtunzi huyu hana wakubwa kwao? Wenyewe hujitetea kuwa uhuru wa kujieleza
kwa kusema lililo kichwani kwa lugha yoyote ndio usasa, na kwa kuwa jamii
hailalamiki, pengine ndio hali halisi. Mtunzi ni binadamu aliyetoka katika
jamii, na hivyo hutunga kutokana na jinsi alivyolelewa na familia yake na jamii
iliyomzunguka. Mtunzi aliyelelewa katika mazingira yaliyojaa matusi na lugha
sizizo na staha, bila hofu tungo zake zitafuata reli ya malezi yake, na jamii
itafurahia kazi hiyo. Wahenga walisema ‘Msanii ni kioo cha jamii’, wengi
hukosea tafsiri ya ‘kioo’ hiki na kudhani ni kile ambacho unaona upande wa
pili, na hivyo husisitiza kuwa wasanii wabadilike pale wanapoona wasanii
hawafanyi yale yanayokubalika katika jamii, bahati mbaya ‘kioo’
kinachozungumziwa kwenye usemi huo ni kile cha kujiangalia sura yako, hivyo
basi ukitaka kuijua jamii fulani ilivyo angalia wasanii na sanaa zao. Kama
ambavyo ukijiangalia kwenye kioo ukakuta sura mbaya, ujue ndio sura yako hiyo, kuvunja kioo au kulaani
kioo hakutabadilisha sura yako, kazi hapo ni kutafuta wajuzi wa kurekibisha
sura, kama ni ndevu wanyoe, kama ni kupaka wanja wafanye hivyo, kioo hakidanganyi.
Tungo
za zamani ambazo zinadumu zilitungwaje? Kwanza kabisa, watunzi walilelewa na
jamii iliyokuwa ikijua kuwa kuna maneno ya kutamka hadharani na kuna yale
maneno ya faragha, hivyo utunzi wa wasanii hawa katika bendi au vikundi vya taarab au kwaya ulikuwa wa
kufuata maadili ya jamii yao, pia vikundi vilikuwa ni chujio zuri la kwanza
la kusahihisha pale mtunzi binafsi alipopotoka. Kulikuweko na swala la kupeleka
tungo kwenye kamati ya maadili kabla kazi hiyo haijarekodiwa. Kupita chujio
hizi kazi zilizotoka zilikuwa na uhakika kuwa hazikuwa na ukakasi wa kimaadili, japo kwa njia hii ya
kamati kulikuwa na mapungufu ya kuzuia kazi kutokana na ujumbe wake badala ya
kuhakiki maadili ya tungo. Katika hali ya sasa, mtunzi anakuwa peke yake
akitengeneza tungo kadri hisia zake zinavyompeleka, hapo ndipo malezi yake huonekana
katika tungo. Tatizo lililopo bila shaka litaendelea kuwa kubwa zaidi kadri
siku zinavyoendelea kwani hakuonekani nia yoyote ya kuandaa malezi ya vijana Kitaifa.
Kwa
kuwa tuna Waziri mpya wa Utamaduni ni vizuri akaiangalia hali hii na kupanga
mikakati ya muda mrefu, kujenga vijana wetu kurudi katika maadili ya
Kitanzania. Kati ya mambo ambayo yanggekuwa nyenzo kubwa katika hili ni
kuhakikisha elimu ya sanaa inarudishwa mashuleni, sanaa isiwe kitu cha
kujifunzia vijiweni na kwenye masikani. Kwa njia hiyo sio tu kwamba tutapata
wasanii makini zaidi bali pia tutapata wapenzi wa sanaa makini. Hali hii ya kuachia
wafanya biashara kuongoza mwelekeo wa sanaa ni hatari kubwa sana ya kupoteza
utu wa Mtanzania. Sanaa ikishakuwa inaendeshwa na biashara, maadili yake
hutegemea soko linahitaji nini, na katika ulimwengu wa utandawazi hili ni
hatari kwa uhai wa maadili ya jamii ambazo hazina msingi imara wa utamaduni
wao.
Tanzania
tunajipanga kuwa Taifa la viwanda, ni muhimu kulea wananchi watakaokuwa
wazalendo wa kujivunia vyao au la pamoja na viwanda vyetu tutakuwa soko la
bidhaa toka viwanda vya nchi ambazo utamaduni wake utakuwa umejikita katika
nchi yetu, sanaa ni njia moja kuu ya kujenga uzalendo, na hivyo pia kujenga
wateja wa bidhaa za viwanda tunavyotaka kuvijenga.
Comments