Januari
2013, niliandika makala kuhusu nilivyouona muziki mwaka 2012. Naona nirudie
makala ile kama nilivyoiandika, na kukuachia msomaji kulinganisha na hali
ilivyokuwa 2016.
Mwaka
2012 ndio huoo umetokomea, ni vizuri kuangalia yaliyopita ili kujitayarisha na
yajayo. Muziki wa nchi yetu ulitawaliwa na muziki wa Bongoflava, Taarab, muziki
wa bendi, matarumbeta, muziki wa Enjili, na muziki wa kiasili. Si siri kuwa
muziki wa Bongoflava ndio uliokuwa ukitawala katika vyombo vya habari na sehemu
nyingi za maonyesho. Muziki huu ulikuwa ukifuatiliwa na muziki wa Taarab na muziki wa enjili. Katika muziki wote huu jambo lililokuwa
wazi ni kuwa waimbaji ndio waliokuwa wakipewa kipaumbele katika tasnia
hii. Waimbaji katika aina zote za
muziki uliotajwa hapo juu ndio waliotajwa sana na kupewa sifa kwa ubora wa
muziki. Kumekuweko na mashindano kadhaa ambayo yote yamejikita katika kutafuta
vipawa vya waimbaji japo mara nyingi yamejitambulisha kama mashindano ya kusaka
vipaji mbalimbali.
Hakuna
ubishi muziki wa dansi na muziki wa asili ndio muziki uliopewa muda mchache
sana katika vyombo vya habari. Na hata katika muziki huo, bendi ambazo zimejikita
kufuata mipigo ya Kikongo zilipewa nafasi zaidi kuliko bendi ambazo
zimejichagulia njia nyingine za muziki wao.
Kuna
sababu kadhaa ambazo zimefanya muziki wa bongoflava kuchukua nafasi zaidi
katika vyombo vya habari, la kwanza ni uwingi wa kazi za bongoflava
zinazorekodiwa. Karibu kila mji una studio ya kurekodi, na katika studio hizo
kazi nyingi zaidi zinazorekodiwa ni aina hiyo ya muziki, hivyo kutokana na
uwingi wa kazi hizo ni wazi kabisa ndizo ambazo zitaendelea kutawala anga la
vyombo vya habari, na kutokana na mfumo wa vyombo vyetu vyote kujikita katika
mfumo wa aina fulani tu za muziki.
Kwa
mtizamo wangu heka heka za muziki wa Enjili zilipungua 2012. Yale matamasha
makubwa ya muziki huo yalipungua sana, na hata nyimbo za kushtua jamii hazikuwa
nyingi kama ilivyokuwa miaka ya
nyuma.
Muziki
wa Taarab haujaleta mabadiliko kimuziki, mengi yaliyofanywa katika 2012 ni
marudio tu ya ubunifu uliofanyika nyuma. Kama vile uanzishwaji wa kucheza show
katika taarab, upigaji wa gitaa na kuliachia pekee yake kama ilivyokuwa kwa
bendi kuachia gitaa la rhythm miaka kabla ya tisini. Kumekuweko tu ubunifu wa
misemo na mipasho, jambo jingine ambalo limesababisha kuenziwa zaidi kwa
waimbaji tu katika fani hiyo.
Bendi
ziko katika wakati mgumu, wakati wanamuziki wengi wa bendi wakilalamika kuwa
muziki wa bendi haupigwi katika redio na TV, kumekuweko na jitihada ndogo za
bendi kurekodi nyimbo mpya, maelezo mengi yamekuwa ni kuhadithia enzi ambapo
muziki wa bendi ulitawala na kuona kama hiyo ni sababu tosha ya muziki huo kuendelea
kurushwa hewani. Bendi chache zilizorekodi hazijaja na nyimbo zilizoweza kuteka umma wa Tanzania na hivyo kusababisha muziki
huu kukosekana katika anga za muziki. Matangazo mengi ya muziki wa dansi
yamekuwa ni kutangaza rap mpya au kupatikana kwa msanii mpya, lakini kiujumla
hakujakuwa na kitu kipya katika muziki wa bendi.
Muziki
asili pia umekosekana kwenye vyombo vya habari kwa kuwa si vikundi vingi vya
muziki huu vyenye uwezo wa kulipia gharama za studio. Pia studio nyingi
zimejengwa kuruhusu wasanii wa Bongoflava tu kurekodi, studio za kuweza
kuruhusu kundi la muziki wa asili kurekodi ni zenye gharama kubwa sana. Kundi
la Makirikiri lilitakiwa kuwa elimu tosha kwa wasanii wa muziki wa Kiasili,
kuwa na muziki wao ukifuata taratibu nzuri unauza, bahati mbaya kuna vikundi
sasa vimeacha kuboresha muziki na ngoma zao, badala yake vinaiga uchezaji wa Makirikiri.
Pengine
watu watasema nimesahau muziki wa kwaya, sijausahau, kwa kweli muziki huu
umebaki hasa kwenye muziki wa
Enjili. Hapo zamani ulikuwa ukitumika sana mashuleni na kwenye siasa na kampeni
, lakini kwa mwaka 2012 hali imekuwa mbaya kwa muziki huu.
Pamoja
na kuwa wengine wangeweza kusema tunasonga mbele katika muziki, kwangu mimi
naona tunarudi nyuma kitaaluma. Tasnia inaingiza pesa nyingi zaidi, na hata
kuna wasanii walioingiza pesa nyingi sana, lakini kwangu hilo si kipimo cha maendeleo katika tasnia hii.
Kama
nilivyoanza kusema washika maikrofon wamekuwa ndio alama ya muziki wa Tanzania.
Muziki ni zaidi ya kuimba. Katika kuimba sauti nzuri ya muimbaji ni muhimu, na
ninashukuru kwa hilo tunao waimbaji wazuri wengi sana, lakini ule muziki unaomsindikiza muimbaji ni
muhimu sana kwani ule hauna mipaka wala lugha, na ndio unaoweza kutufungulia
mlango wa soko la kimataifa. Wengi tunapenda sana muziki wa kutoka Kongo,
Nigeria, South Africa, pamoja na kuwa hatujui hata moja wanaloliongelea
tunaupenda muziki huo kutokana na mpangilio wa vyombo vyao. Kutokujali wapigaji
katika mfumo wa nchi yetu ndio unatupelekea kuwa watu wa ‘copy and paste’ wa
upigaji wa muziki wa nchi nyingine. Ukiorodhesha nyimbo zote zilizotikisa nchi
hii kwa mwaka 2012 utagundua asilimia kubwa ya muziki uliotumika ulikuwa ni wa
kunakili mipigo kutoka muziki wa nchi nyingine, Nigeria, Congo na Afrika Kusini
ndio wamekuwa waalimu wetu wakuu wa muziki.
Na JOHN KITIME wa <www.johnkitime.co.tz>
Comments