KUMBUKUMBU ZA KUWA MWANAMUZIKI KATIKA AWAMU MBALIMBALI ZA NCHI HII


THE REVOLUTIONS
Karibu kila kituo cha redio siku hizi kina kipindi maalumu cha muziki wa zamani. Nyimbo na hadithi za matukio ya wanamuziki enzi hizo zimekuwa zikiongeza wasikilizaji wa rika zote bila kujali jinsia. Lakini hali ilikuwaje kuwa mwanamuziki enzi hizo? Nina bahati ya kuwa mwanamuziki katika awamu za marais wote waliowahi kuongoza nchi hii, na hakika kumekuwa na tofauti za maisha katika katika kila awamu. Nilianza kujihusisha na muziki katika vikundi mwishoni mwa miaka ya 60 wakati nilipoingia sekondari. Enzi ya Mwalimu. Wakati huo shughuli za sanaa kwa ujumla zilikuwa na nafasi muhimu katika elimu. Wachoraji, wachongaji, wanamuziki walipewa nafasi ya kukuza na kuonyesha vipaji vyao, shule zilitoa nafasi maalumu kwa shughuli hizo. Hivyo nikiwa ‘Form One’, wakati huo neno ‘Kidato’ lilikuwa halijulikani, na wenzangu tulianzisha ‘bendi’ yetu. Shule yetu ikatukabidhi ‘Tape recorder’ tufanyie mazoezi na pia kujirekodi. Mashine hii ilikuwa na uwezo wa kuwa amplifaya hivyo tuliweza kuunganisha magitaa yetu na kufanya mazoezi. Tukipiga nyimbo za bendi mbalimbali kubwa za Afrika na Marekani, na nyingine tulitunga wenyewe. Kilele cha mazoezi yetu ilikuwa ni kufanya maonyesho yetu siku za ‘open day’ ambapo wazazi ndugu marafiki waliruhusiwa kutembelea shule kuangalia kazi zetu mbalimbali. Hali kama hii pia ilinikuta nilipokuwa chuoni nako pia kulikuwa na bendi ya wanachuo, vyombo vyote vilikuwa mali ya chuo, nakumbuka kilele cha maonyesho ya bendi hii ni siku bendi ya Baba Gaston ilipokuja kufanya onyesho chuoni kwetu, nasi tukapata nafasi ya kutumia vyombo vya kisasa kupiga nyimbo zetu mbili tatu. Katikati ya miaka ya sabini ndipo nikajiunga katika bendi ya ‘mtaani’ pale kwetu Iringa. Bendi yetu tulijiita Chikwalachikwala, wakati huo kama ilivyo sasa, linalotokea Kongo kimuziki ndilo linaloigwa na wanamuziki wetu, hivyo huko kulikuwa na bendi zenye majina ya kujirudia rudia, kama vile Lipua lipua, Bela bela nasi tukawa Chikwala chikwala, na bendi kubwa nazo zikawa na mitindo kama ‘heka heka, vangavanga, subisubi na kadhalika. Tulikuwa tukipiga muziki kila mahala, kwenye vilabu vya pombe za kienyeji, kwenye maghala ya mbolea vijijini, na  baada ya kumaliza kupiga hapo ndipo mahala pako pa kulala. Pesa iliyopatikana tuligawana japo ilikuwa ndogo sana. Ila jambo moja muhimu sana ni kuwa msaada mkubwa ulikuwa ukitolewa na Maafisa Utamaduni, ambao wakati huo tuliweza kuwalilia kama hatuna nyuzi za gitaa au vipaza sauti, na kwa kweli walihangaika sana kuhakikisha tunapata vitu hivi. Hata katika safari za wanamuziki , wakikwama kutokana na kukosa kipato kwenye maonesho yao, Maafisa Utamaduni walikuwa wakihakikisha wanatafuta njia ya kuwakwamua. Mwanzoni mwa miaka ya 80 ndipo nikapata nafasi ya kuja Dar es Salaam na kuingia studio kurekodi kwa mara ya kwanza katika studio za serikali za Tanzania Film Company. Hii ilikuwa baada ya kuigiza katika filamu ‘Wimbo wa Muanzi’ na kisha kutakiwa kurekodi muziki kwa ajili ya filamu hiyo. Safari hiyo ndiyo ikaniunganisha na Tchimanga Kalala Assossa ambaye wakati huo alikuwa ndio anasuka bendi yake ya Orchestra Mambo Bado. Mara baada ya kukamilisha kurekodi, mimi na mwenzangu marehemu William Maselenge tukajiunga na Orchestra Mambo Bado, na kwa mara ya kwanza kuanza kulipwa mshahara kwa kupiga muziki. Mshahara ukiwa shilingi 500/- kwa mwezi, na marupurupu mengine kutegemea na mapato ya mlangoni. Kwa kipato hiki hakika hakikuwa kinakidhi kuendeleza maisha, hivyo maisha hayakuwa rahisi. Furaha kwa kila mwanamuziki ilikuwa bendi kuwa safarini, kwani hapo una uhakika wa ‘allowance’ kila siku , ilikuwa kawaida kabisa wanamuziki wanne au zaidi kulala chumba kimoja ili kubana matumizi. Katika nyakati hizi kulikuwa na bendi nyingi ambazo zilikuwa zikiendeshwa na mashirika ya umma na taasisi nyingine za serikali, huku ndio kulikuwa na uhakika wa maisha kwani mishahara ilikuwa mizuri na kulikuwepo na mafao ya ziada kama nyumba, usafiri wa kwenda na kurudi kazini, matibabu na mengineyo mengi.
Katika awamu ya Pili ya uongozi wa nchi hii, ndipo kuporomoka kwa bendi nyingi za mashirika ya umma kulipoanza kutokea, mashirika mengi yalianza kufilisika na hivyo shughuli za burudani ndizo zilizoanza kufutwa. Japo pia wakati huohuo kulizaliwa bendi nyingine za mashirika ya umma kama vile TANCUT Almasi Orchestra ya Iringa, mali ya wafanyakazi wa kiwanda cha kuchonga almasi  ambayo hakika ni bendi ambayo ina nafasi ya pekee moyoni katika bendi zote nilizowahi kupitia. Maisha katika bendi hii kwa wastani yalikuwa mazuri, wanamuziki tulipewa nyumba za kuishi, mshahara mzuri, bonus kila mwezi, bonus kwa kila dansi ambayo haikuzidi shilingi 400/-. Vyombo vya muziki vizuri na sehemu nzuri ya kufanyia mazoezi, si ajabu kuwa bendi hii ilikuwa tishio japo ilikuwa na makao yake nje ya Dar es Salaam, na ilijulikana kwa jina la utani la ‘Bush Stars’. Katika bendi hii hakukuwa tena na shida ambazo zilikuwa kawaida kwa bendi nyingi binafsi, mambo kama kukosa mishahara au kulazimika kurudi nyumbani kwa miguu, pale ambapo onesho limekosa wateja, si mara moja nimeshatembea kwa miguu kutoka Kigogo Luhanga mpaka Kinondoni baada ya dansi saa nane usiku. Nakumbuka hata sababu ya kuacha Orchestra Makassy ilitokana na kutwanga mguu saa nane za usiku kutoka Makonde Bar Mikocheni mpaka Oyster Bay nilikokuwa nikiishi wakati huo.
Ni katika awamu hii ya Pili, nilipojiunga na Vijana Jazz band nikitokea TANCUT Almasi Orchestra. Kupitia bendi hii nilitembelea wilaya zote nchini kupiga muziki, na kwa kutumia usafiri wa aina mbalimbali, ukiwemo wa basi na malori, na hata kwa meli kwa safari za kwenda Mtwara, Unguja na Pemba. Kwa vile bendi ilikuwa ikipendwa maisha hayakuwa magumu. Bendi ilizunguka kufanya kampeni mbalimbali, kwa mfano tulizunguka kupiga  muziki vijijini Zanzibar katika kuhamasisha uvunaji bora wa Karafuu, na kwa kuwa ilikuwa bendi ya Umoja wa Vijana wa CCM, tulizunguka sana kwenye kampeni za kisiasa, ikiwemo kufanya maonyesho kwa viongozi mbalimbali wa Kimataifa, ikiwemo kupiga kila alipokuwa akihutubia Nelson Mandela alipotembelea Tanzania baada ya kufunguliwa kwake.  
Awamu ya Tatu ilikuja na mapya kabisa, siku ya kutangazwa kwa serikali mpya, idara ya Utamaduni haikutajwa. Ilizoeleka kuwa idara hii kuwa chini ya wizara ya Elimu, lakini kilichotajwa ni siku hiyo Wizara ya Elimu, Utamaduni haukutajwa hivyo kuacha swali kubwa kuwa utamaduni uko wizara ipi?  Baada ya  muda si mrefu Maafisa Utamaduni waliokuwa chini ya Wizara ya Utamaduni nao wakapotea, hali iliyopo mpaka leo hii. Ule ukaribu wa wanamuziki na serikali ukaanza kupotea, wafanya biashara wakachukua nafasi ya kuanza kuendesha shughuli ya muziki na kutafuta kuendeleza muziki wenye gharama ndogo kwa kupata faida kubwa.  Kupiga muziki kwa ajili ya upenzi wa sanaa ya muziki ukaanza kupotea na nafasi ya kupiga muziki kama kazi au biashara ukachukua nafasi. Na haswa ndio hali halisi ya sasa, Muziki haupimwi kwa ubora katika usanii, bali kwa uwezo wake wa kuingiza fedha. Kila zama na vitabu vyake.

Comments