Skip to main content
ELIMU YA HAKI ZA WASANII INATAKIWA HARAKA
WASANII kwa ujumla hawakubali kuwa wanahitaji elimu kuhusu haki zao. Ukiongea na wengi na hasa wakiwa maarufu wanaona kuwa wanaamini kuwa hawana sababu ya kupata elimu yoyote ya sanaa, kwani aidha wanaridhika na kipato wanachopata na wanaamini kuwa hicho ndio kipato sahihi walichotakiwa kupata. Kuna wale ambao wanaowaongoza wanawadanganya kuwa hawana haja ya kupata elimu yoyote ya haki zao kwani mameneja wao watahakikisha kuwa wanafuatilia haki zao. Asilimia kubwa ya mameneja hawajui sheria zinazolinda haki za wasanii wao, lakini nao pia hawonyeshi nia ya kutaka kujua au wasanii wao wajue, Mara nyingine kwa makusudi kwani wanajua kuwa wasanii wao wakipata mwanga kuhusu haki zao watagundua ukubwa wa wizi wanaofanyiwa. Viongozi wengi wa wasanii huhakikisha wanachafua majina ya chombo au mtu yoyote anaejaribu kutoa elimu ya haki kwa wasanii. Kampeni kubwa hufanywa na hivyo wasanii maarufu wengi utasikia COSOTA ni mbaya, BASATA ni mbaya, CMEA ni mbaya, Hakimiliki haifai kwa wasanii wa Tanzania, na majina ya wahusika wa hakimiliki hutangazwa kuwa ndio wakwamishaji wa vita ya haki za wasanii. Na hii imekuwa hivyo kuanzia miaka ya tisini. Wakati wasanii wakigawiwa makombo ya chakula na kuaminishwa ndio chakula chenyewe, wajanja hawa wamekuwa wakiingiza mabilioni ya fedha mifukoni mwao. Na kati ya fedha hizo, chache sana zinakatwa kodi maana zinakuwa fedha zisizo na uwazi. Ukimuuliza msanii atakwambia kasaini mkataba ukimuuliza nakala ya mkataba, hana au uko na tajiri yake , lakini kamwe hawataji thamani ya mkataba. Waendeshaji wa kampeni hizi wananguvu za kifedha na pia kimahusiano na viongozi wakubwa wa nchi kiasi cha mapendekezo yao kuhusu ulinzi wa haki za wasanii huchukuliwa na hata kufanyiwa kazi, na mwisho wa siku hakuna chochote kinacho wasaidia wasanii.
Umefika muda wa wasanii, serikali na wadau wenye nia njema kujiuliza kwanini wasanii wa Tanzania hawataki kujua haki zao, kwanini hawataki kufuata sheria za kujisajili na kusajili kazi zao? Na kikubwa kwanini serikali haitaki kusisitiza utimizwaji wa sheria za kulinda haki za wasanii?
Comments