KIZUNGUMKUTI CHA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA HAKIMILIKI


Hakika neno Hakimiliki si jipya kwa wapenzi wa muziki nchini. Lilianza kuwa maarufu miaka ya tisini wakati biashara ya kanda za kaseti imeshamiri. Wanamuziki walianza harakati za kudai Hakimiliki kwa sauti zaidi baada ya kuanza kuona kanda zao zinauzwa lakini hawapati chochote. Je, Hakimiliki ni nini?
Hakimiliki ni haki anazopewa mtunzi ili kuweza kulinda maslahi yake katika tungo zake. Tungo ni mali, lakini mali hii bahati mbaya ikishatoka hadharani ni vigumu kuzuia wengine kutumia. Hivyo ili kulinda maslahi ya mtunzi kumetengenezwa sheria za Hakimiliki, sheria zinazompa mtunzi haki kuu mbili, haki za kimaadili na haki za kiuchumi. Haki za kimaadili, ni zile haki zinazolazimisha mtunzi kutajwa wakati kazi yake inapotumika. Hivyo basi jina la mwandishi wa kitabu linapoonekana juu ya kitabu, ni katika kutimiza haki za msingi za mtunzi kwa kujulisha kuwa tungo ile ni mali yake, au majina ya wasanii wa filamu kuonyeshwa mwanzo au mwisho wa filamu ni katika kutekeleza haki hii, na hata mwanamuziki kutajwa juu ya jarada la kazi yake ni katika kutimiza haki hii. Haki ya pili ni kundi la haki za kiuchumi. Haki hizi kumuwezesha mtunzi kupata pato la kiuchumi kutokana na kazi yake. Hivyo anakuwa na haki ya kurudufu kazi yake,kusambaza, kutafsiri, kuazimisha, kuitangaza katika vyombo vya utangazaji, kuibadili matumizi na kadhalika na katika njia hizi mbalimbali za matumizi akapata malipo kutokana na kazi yake. Kwa kuwa mtunzi anaweza kuwa hana uwezo wa kurudufu na kusambaza, huingia makubaliano na wasambazaji kwa kuwapa haki yake ya usambazaji, ili wasambaze kazi yake nae apate mgao wake. Hivyo kusambaza kazi bila makubaliano na mwenye kazi ni kumnyima haki mwenye kazi. Kwa kuwa mtunzi wa muziki anahitaji kazi yake isikike, hutoa haki ya kazi yake kutangazwa kwenye vyombo vya habari, lakini kwa kuwa vyombo vya habari hutumia kazi ile kupatia wasikilizaji zaidi kwenye vyombo vyao na hivyo kuvutia watangazaji, na hata kutumia katika vipindi vinavyoingiza fedha, mtunzi hulazimika kulipwa mirabaha, ambayo ni asilimia ndogo ya pato la vyombo vya habari kama stahili yake katika biashara hiyo. Vivyo hivyo iwapo kazi ya utunzi itatumika kwenye biashara ya muziki katika simu kama ‘ringtones’ au ’caller tunes’ na kwa kuwa kuna fedha hupatikana, mwanamuziki anastahili kupata mgao wake wa biashara hiyo, na utaratibu huo hutumika popote pengine ambapo tungo hutumika na yakafanyika malipo. Kwa muda mrefu swala hili limekuwa likigusiwa na viongozi mbalimbali wakitoa mifano ya wanamuziki wa nchi nyingine kufaidika na kazi zao lakini bado kimekuwa kitendawili kwa wanamuziki wa hapa nchini, ambao wengine hufa kwa dhiki japo kazi zao zinaingiza fedha kwa njia moja au nyingine. Tatizo liko wapi? Tatizo kubwa la kwanza ni kuwa hakuna nia thabiti ya kubadili hali ilivyo. Hivyo hatua kali za kudhibiti dhuluma kubwa wanayofanyiwa wanamuziki na wasanii wengine kupitia kudhulumiwa haki zao hazichukuliwi. Mwaka 2001 ilitengenezwa kamati iliyoitwa National Anti Piracy Committee, kamati ambayo kazi yake ilikuwa ni kutengeneza kanuni zitakazoweza kudhibiti wizi wa kazi sanaa za video na audio. Kamati hii ilitengeneza kanuni ambazo ziliongoza kuwa kila CD, DVD na vifaa kama hivyo ambavyo vinakazi za sanaa na vinatakiwa kuuzwa, lazima view na stika ya COSOTA. Stika hii ilipewa jina la Hakigram, na mwaka 2005 kanuni hii ilisainiwa na Waziri wa Viwanda na Biashara wakati ule na kuwa tayari kutangazwa katika gazeti la serikali ili kuwa sheria halali. Karatasi zenye saini ya Waziri zilipotea katika mazingira ya kutatanisha kabla ya kutangazwa!! Mwaka uliofuata COSOTA iliwezesha mchakato kurudiwa kupitia Waziri  wa kipindi hicho na hatimae sheria ikapitia taratibu zote na kuwa rasmi. Baada ya hapo COSOTA ilianza jitihada kuiomba serikali kutoa fedha za kuanza kufanikisha taratibu hizi za kisheria kwa kununua stika za awali, pamoja na maneno mazuri sana ya viongozi mbalimbali kuonyesha kuwaonea huruma wasanii kwa kuibiwa , lakini fedha hazikutolewa kwa shughuli hiyo mpaka leo hii. Mwaka 2007 zikaanza harakati nyingine za kutengeneza sheria ya kuweka stika kwenye CD na DVD ila awamu hii stika hizo zilikuwa ni za TRA. Zaidi  ya mara moja ilitangazwa na viongozi wa juu kuwa serikali ilitoa shilingi milioni 20 kwa ‘mtaalamu’ toka Chuo Kikuu Dar es Salaam ili kufanya utafiti ambao uliwezesha serikali kuanzisha utaratibu wa stika ya TRA ambao utaratibu huu ungemaliza wizi wa kazi za muziki na filamu. Mpaka leo ‘Mtaalamu’ hajulikani jina wala ‘utafiti’ haujulikani uko maktaba gani. Lakini sheria iliyoitwa ‘The Films and Music Products (Tax Stamps) Regulation, 2013’ iliweza kupatikana. Ni mwaka wa tatu sasa sheria hii ipo, wizi uko palepale, mbaya zaidi kutokana na utekelezaji wa sheria hii, uuzaji halali wa CD na DVD za  wanamuziki wa Tanzania ndio umetoweka kabisa,  wasambazaji wamekimbia kwa maelezo kuwa biashara hiyo hailipi tena. Matokeo ya kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo iliyofanyiwa ‘utafiti wa milioni 20’.
Mwaka 2003, ilipitishwa kanuni ambayo ilielekeza utekelezaji wa vyombo vya utangazaji, radio na TV kulipia kazi za muziki zinazorushwa na vyombo hivyo.  Kanuni hii inayoitwa ‘The Copyright (Licensing of Public Performances and Broadcasting) Regulations 2003’ ilitangazwa kwa mara ya kwanza , tarehe 10 Oktober 2003, ina miaka 13 sasa, na bado hakuna kinacholipwa. Hakika umefika muda muda sasa hadithi ziishe kazi ianze, hebu fikiria nchi nzima zimejaa DVD za filamu zisizo halali na CD za muziki zisizo halali na zinauzwa hadharani, biashara ya kuingiza muziki kwenye flash na memory card bila ruksa ya wenye muziki haifanywi kifichoni nini kinakwamisha sheria isifuatwe?



Comments