MUZIKI NI BURUDANI, LAKINI BURUDANI KWA NANI?


Pombe ni burudani kwa mnywaji, lakini si burudani kwa mtengeneza pombe. Pale mtengeneza pombe atakapoanza kuburudika na pombe yake mwenyewe, ndio utakuwa mwisho wa yeye kufaidika kiuchumi na pombe hiyo. Hali kadhalika katika muziki burudani ni kwa wasikilizaji, na pale mwanamuziki anapotekwa na muziki wake kuwa burudani kwake, swala la muziki huo kumpa faida za kiuchumi hupungua. Kwa miaka mingi muziki katika nchi yetu umekuwa ukisisitizwa kuwa ni burudani, jamii huitaja hivyo vyombo vya habari husisitiza hivyo, japo vingine huingiza mabilioni ya shilingi kwa mwaka kutokana na ‘burudani’ hiyo. Kutokana na mambo kadhaa, ni wazi kuwa serikali pia huamini muziki ni burudani tu. Utamaduni huu ni moja ya sababu kubwa kwanini wanamuziki wa Tanzania hawafaidi matunda ya kazi yao kama wanavyofaidi wenzao wa nchi nyingine, japo mara nyingine ubora wa muziki wa Tanzania ni sawa  na mara nyingine ni bora kuliko wa nchi nyingine.
Juzi juzi nilipata bahati ya kuongea na mama mmoja ambaye alikuwa mmoja wa wanamuziki wa bendi iliyokuwa ni ya wanawake tu. Bendi hiyo iliitwa TANU Youth League Women Jazz Band, historia inatuambia kuwa bendi hii ilitokana na safari ya Rais Sekou Toure alipokuja Tanzania akiwa amesindikizana na bendi ya Les Amazones de Guinee. Bendi hii ilikuwa ni ya wanamuziki wanawake ambao walitoka kwenye jeshi la polisi la nchi ya Guinea. Les Amazones ilizaliwa mwaka 1961 ilikuja kuwa ndio  moja ya bendi maarufu za Guinea, hasa baada ya Rais Sekou Toure kusambaratisha bendi zote binafsi na kuunda bendi zilizofadhiliwa na serikali yake. Ujio wa bendi ya wanamuziki wa kike wakipiga kila chombo katika bendi kikahamasisha TANU Youth League kuamua kutengeneza bendi ya aina hiyo. Mwaka 1965, mabinti kadhaa wakajiandikisha na kuanza kupewa mafunzo na kitengo cha muziki cha Jeshi la polisi, chini ya Mzee Mayagilo. Tarehe 31 May 1966, kundi hili likarekodi nyimbo zake 6 za kwanza ndani ya studio za RTD. Kundi lilianza kufanya maonyesho na hata kusafiri nje ya nchi. Kwa kadri ya maelezo  ya mmoja wa wanamuziki wa bendi hiyo, waliwahi kukaa Nairobi kwa wiki mbili wakifanya maonyesho yaliyohudhuriwa na watu wengi. Lakini tatizo likawa hawakuona matokeo yoyote kiuchumi, siku za mwanzo waliona kuwa ilikuwa ni raha sana kushangiliwa na kusafiri huku na kule na kupiga katika hafla kubwa kubwa lakini baada ya muda wakaanza kujiuliza mapato yanakoishia, kutokana na kutokupata mgao wa mapato yaliyotokana na maonyesho yao bendi ikasambaratika, swala la burudani tu likawashinda, tena bendi ilisambaratika wakati imeshatayarishiwa safari ya kwenda kufanya maonesho China. Viongozi wao hawakuona sababu ya kuwalipa wanamuziki hawa wa aina yake, kwa kuamini burudani ya kupiga  na kusafiri ni mshahara tosha. Wanamuziki wengi wa zamani wanaeleza jinsi walivyokuwa wakitumika kufanya maonyesho ya kupokea viongozi kukesha kwenye shughuli za Mwenge na kulazimishwa kupiga kwenye sikukuu mbalimbali bure kwa maelezo kuwa wanatoa burudani kwa wananchi hivyo hakuna sababu ya malipo. Bendi nyingi zilikufa na wanamuziki wengi mahiri waliacha muziki na kuamua kufanya kazi nyingine. Kwa bahati mbaya sana hata leo hii kuna wanamuziki wengi wengine wamo katika tasnia ya muziki kwa ajili ya burudani, hivyo hawanatatizo kubwa la kulipwa, nia yao ni kupanda jukwaaani au kujisikia redioni tu. Jambo ambalo limewezesha utamaduni wakutoa rushwa ili nyimbo zao zirushwe kwenye radio na luninga,kukomaa katika tasnia hii. Kuna majadiliano makali yanaendelea ambapo wakati baadhi ya wanamuziki wanadai kulipwa mirabaha kutokana na nyimbo zao kurushwa hewani na vyombo vya habari, kuna upande wa pili wa wanamuziki wakisisitiza kuwa hawataki kulipwa chochote, jambo ambalo limevifanya vyombo vingine kulazimisha wanamuziki kusaini karatasi kuhakiki kuwa hawatadai malipo yoyote kwa nyimbo zao kukutumika na vyombo hivyo. Jambo jingine ambalo linaonyesha wazi kuwa serikali inaona shughuli ya muziki ni burudani ni ukubwa wa kodi za vifaa vya muziki. Wakati viongozi wakinadi kuwa sanaa ni kazi, kodi ya vyombo  iko juu sana na hivyo kufanya mwanamuziki wa kawaida kutoweza kununua kitendea kazi chake. Vyombo vya muziki viko katika kundi la ‘luxury items’ vitu vya anasa, harakati za kutaka kodi ya vifaa hivi iangaliwe upya zilizna toka miaka ya 80, lakini mpaka leo hazijazaa matunda. Viongozi wa Utamaduni na michezo, utawasikia mara zote wakisisitiza kutengwa kwa maeneo ya michezo lakini husikii wakihamasisha kutengwa maeneo ya kujenga kumbi za kujifunza na kuendeleza muziki. Ni wazi utamaduni wa kuona muziki ni burudani tu na si jambo la kuweza kuleta tija kwa jamii na nchi, umeota mizizi katika kila ngazi ya jamii.

Comments