KIZUNGUMKUTI CHA TASNIA YA MUZIKI TANZANIA


Tasnia ya muziki Tanzania ina mambo mengi sana ya ajabu ukiyaangalia kwa makini. Kuna vyeo lukuki, huko. Kuna Wakurugenzi wa Bendi, Marais wa Bendi, kuna Madokta, Maprofesa na vyeo vya aina aina huko. Hebu tuanze na kitendawili cha kwanza, kuna huu muziki ambao huitwa ‘Muziki wa Dansi’, aina hii ya muziki ilipata sifa ya kuitwa hivyo miaka ya miaka ya themanini na ulikuwa na maana muziki unaopigwa na bendi na ambao unatokana na mahadhi ya muziki wa Kongo. Palikuweko na bendi nyingine zikipiga muziki ambao watu walikuwa wakicheza lakini cha ajabu haukuwa unaitwa muziki wa dansi. Kwa mfano bendi ambayo iliamua kupiga muziki wa reggae japo ulikuwa ni muziki wenye dansa lakini haukuitwa ‘muziki wa dansi’, hata bendi ambazo zilikuwa zikipiga muziki wake katika mahoteli, japokuwa zilikuwa zikipiga muziki wa mitindo mbalimbali kama chacha, rumba, tango , bosanova na kadhalika, na watu walikuwa wakicheza muziki wao, muziki huu ulipewa jina la muziki wa hoteli, na si muziki wa dansi. Kati ya mwaka 1980 na 1990 vilianzishwa vyama ambavyo viliundwa kuwakilisha aina mbalimbali za muziki na hivyo kukaweko na Chama cha Muziki wa Dansi (CHAMUDATA) na kulikuweko na Chama cha Muziki wa Taarab (TTA-Tanzania Taarab Association)na Tanzania Disc Music Association (TDMA) chama kilichokuwa cha wadau wa muziki wa Disko. Mapungufu ya utaratibu  huu wa kupanga wa kupanga ‘muziki wa dansi’ yalijitokeza wakati wa mashindano ya Bendi Bora yaliyoitwa Top Ten Show mwishoni mwa miaka ya 90 ambapo kundi la Varda Arts, ambalo lilikuwa kundi la vijana wenye asili ya Kihindi walipoingia kwenye mashindano haya na kuwa kati ya bendi kumi bora, malalamiko yakaanza, wanamuziki wengine walipoanza kulalamika kuwa Varda Arts hawapigi ‘muziki wa dansi’.
Katika zama hizi maana hii ya zamani ya ‘muziki wa dansi’ inakuwa na utata zaidi pale unapoona zipigapo bendi zinazoitwa za muziki wa dansi, watu hawachezi  na pale vikundi vya muziki mwingine, kama Taarab au hata muziki wa injili vikiporomosha muziki watu wanajimwaga kucheza dansi. Muziki wa Taarab umeweza kuwa na mabadiliko mengi kadri miaka inavyoenda na umeweza kutengeneza matawi mengi kiasi cha kuwa wengi wapenda taarab asili huwa hawataki baadhi ya matawi hayo kuitwa Taarab, hii ni kutokana na muziki huo kuwa na mambo mengi ambayo wapenzi wa Taarab asilia hawakubali kabisa, nakumbuka sentensi moja ya Bi Kidude aliposema hii ya sasa si Taarab kwa kuwa waimbaji wanacheza jukwaani. Hakika siku hizi sit u kuwa wanacheza bali kuna ‘wacheza show’ na wapenzi wa muziki huo wamegundua dansa za aina mbalimbali. Hivyo kutokuita aina hiyo ya muziki kuwa ni muziki wa dansi ni kukwepa ukweli.
Tasnia ya biashara ya muziki nchini ilitokana na misingi ya biashara ya maharamia wa muziki (music pirates), kazi za awali za muziki zilizouzwa katika kanda za kaseti asilimia 99 zilikuwa si halali, wafanya biashara hawa walionza biashara hii mwishoni mwa miaka ya 70 waliikuza biashara hii na kufikia miaka ya 90 zilipoanza kupamba moto harakati za kudai Hakimiliki, walianza kubadilika na kuanza kuingia mikataba na wanamuziki wa hapa nchini na kusambaza kazi zao. Haikuwa mikataba yenye haki, lakini inatokana na ukweli kuwa shetani hawezi kugeuka malaika. Nyadhifa muhimu katika tasnia ya muziki zikaanza kusikika, kukawa na wasambazaji, mameneja, mapromota,  maproducer’ . Vyeo hivi vingi vilikuwa ni vya kujipachika, havikuwa na elimu ya awali bali ile ya mtaani. Hali hii ilikuwa nzuri kwa maharamia waliogeuka wasambazaji, walikuwa wanafanya kazi na watu ambao hawana upeo wa kutosha wa tasnia. Wanamuziki walisainishwa mikataba ya ajabu, mingi ikiwa ni ile ya kuuza Hakimiliki. Na wasanii wengi walisikika wakijisifu kwenye vyombo vya habari kuwa ‘wameuza master’ kwa msambazaji huyu au yule. Jambo ambalo ni Tanzania tu ndio walikuwa mabingwa wa kulifanya, kutokana na upeo mdogo wa ‘mameneja’ na ‘maproducer’ wao. Bahati mbaya hali hii haijabadilika sana japo kumekuweko na maendeleo ya wasanii kujulikana zaidi na hata kutayarisha na kufanya maonyesho yao nje ya nchi yetu. Haki nyingi na fursa nyingi zinapotea kutokana na kutokuwa na elimu halisi ya kazi zinazofanywa na wanaoongoza njia za wasanii katika maendeleo yao. Si mara moja ambapo utasikia msanii akiwa na malengo ya kuingia katika soko la kimataifa, swali Je, ana menejimenti yenye uelewa wa Kimataifa?

Comments