RUSHWA KATIKA TASNIA YA MUZIKI HAIKUANZA JANA WALA JUZI


Leo nitaongelea jambo ambalo lipo lakini gumu kulisikia likiongelewa maana wanaoweza kuliongelea ndio watuhumiwa wakubwa wa jambo hilo. Rushwa limekuwa tatizo kubwa katika nchi yetu, karibu kila siku utasikia habari za rushwa kwenye mikataba, katika kutafuta haki, huduma na kadhalika. Sanaa ya muziki haijakwepa hilo tatizo japo ni mara chache sana kusikia likiongelewa, hii ni ni kutokana na sifa moja ya rushwa, muathirika anakuwa katika nafasi ambayo anajua akilalamika ndio atakosa hata kidogo anachokipata, wala rushwa huwa na umoja sana himaya yao inapotikiswa. Rushwa katika muziki si jambo geni hata kidogo na limetia hasara wanamuziki wengi  kwa miaka mingi na kukosesha wapenzi wa muziki kusikia nyimbo nyingi nzuri miaka nenda rudi. Rushwa imekuwa ikifanywa kwa sababu mbalimbali katika nyakati tofauti. Katikati ya miaka ya 70, kulikuweko na mkanganyiko wa kisiasa kati ya Tanzania na Kenya, hali hii ilifikia mpaka mipaka ya nchi hizi mbili kufungwa. Hili liliathiri ule utaratibu wa wanamuziki wa Tanzania kwenda Kenya kurekodi na kutoa santuri, kwani kwa wakati huo nchi hiyo ndiyo ilikuwa na makampuni yenye uwezo wa kutoa santuri. Wanamuziki wa Tanzania ikalazimika kutegemea kurekodi na hatimae muziki wao kurushwa na redio ya Taifa. Biashara ya muziki ilikuwa ni ile ya kutegemea mapato kutoka kiingilio cha kwenye madansi. Hivyo wanamuziki walitegemea sana redio ipige nyimbo zao zisikike na kuhamasisha wapenzi kuingia kwenye maonyesho. Kabla ya kurekodi, wanamuziki walipaswa kutanguliza mashahiri ya nyimbo zao Radio ya Taifa, ambapo mashahiri yalikaguliwa na kamati maalumu iliyokuwa na uwezo wa kuruhusu au kukataa bila maelezo kurekodiwa wimbo wenye mashahiri hayo. Utaratibu huu ukatoa mwanya wa kuanza kuomba rushwa. Wanamuziki waliombwa rushwa ili nyimbo zao zipitishwe kwenye kamati hii. Hakika bendi ambayo haikuweza kutoa chochote zilipokutwa na hali hii nyimbo zake hazikurekodiwa. Rushwa wakati huu ilikuwa katika njia mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, au hata kuhakikisha kuwa muomba rushwa akiingia kwenye onyesho la muziki analipiwa vinywaji na hatimae usafiri wa kumrudisha kwake, au pengine hata kumlipia ‘guest house’ akiamua kujipumzisha mahala baada ya muziki kwisha. Naikumbuka bendi moja kutoka mkoani ambayo ilikuwa ikija Dar es Salaam na magunia ya mahindi kwa ajili ya kulikabili jukumu hili. Baada ya nyimbo kupitishwa na hatimae kurekodiwa kulikuwa na rushwa ikidaiwa na watayarishaji wa vipindi ili muziki upigwe kwenye vipindi mbalimbali. Na huu ndio ulikuwa utaratibu kwa miaka mingi.
Miaka ya 90 redio binafsi zikaanza. Wanamuziki wengi wakati huo waliamini kuwa kuja kwa redio binafsi kutakuwa ndio mwanzo wa mafanikio makubwa katika muziki, hali haikuwa hivyo. Muziki wa hapa nchini ukawa hausikiki katika vyombo hivi, na sababu kubwa iliyokuwa ikitolewa wakati huo ni kuwa muziki wa Tanzania ulikuwa umerekodiwa katika kanda za kaseti na haupigiki katika mashine za vituo hivyo. Muziki kutoka nje ukashika kasi kubwa na hakika wanamuziki kutoka nje walikuwa walipata umaarufu na kuwa wakifanya maonyesho makubwa nchini karibu kila mwezi. Lakini taratibu ikaonekana kuwa ukipenyeza rupia kazi yako inarushwa hewani. Na katika awamu hii, wanamuziki walikuwa wakitaka kazi zao zirushwe hewani sio kwa ajili ya kufanya biashara ya maonyesho pekee, bali pia ili wasambazaji waweze kuzinunua na kuzisambaza. Watangazaji wengi wakaingia katika biashara ya kujiita mameneja wa wanamuziki, kwa nafasi zao walizirusha nyimbo za wateja wao na hatimae kuingia mikataba na wasambazaji. Wanamuziki ambao hawakuingia katika mfumo huu nyimbo zao hazikupata nafasi ya kusikika hewani. Biashara ya kuuza kanda na hatimae CD ilikuwa kubwa sana, kukaweko makubaliano kati ya wasambazaji na watangazaji ambayo yaliwaweka wanamuziki katika hali ya utumwa wa kutafuta yoyote aliye na uwezo wa kusababisha kazi yao isambazwe wampe chochote. Kulikuweko na rushwa za kutuma vocha kwa watangazaji, rushwa ya ngono, fedha, pombe na kadhalika. Kwa mfano kuna mtangazaji mmoja maarufu alikuwa anahitaji kufanya sikukuu kwa ajili ya mwanae akaagiza kikundi kimoja kutoka Dodoma kimletee mbuzi na na mchele, na hata hivyo hakupiga nyimbo zao japo aliletewa alivyotaka, na huo ndio ukawa kama utaratibu rasmi. Mwaka 2004, chama cha muziki cha TAMUNET kiliandaa maswali na kuyasambaza kwa wanamuziki mbalimbali, maswali hayo yakitaka kujua kama mwanamuziki amewahi kuombwa rushwa, na aina ya rushwa aliyoombwa, majina ya watangazaji waomba rushwa, vituo vya utangazaji ambavyo ndivyo maarufu kwa rushwa na kadhalika. Majibu yaliporudi, sura mpya ikajitokeza, kuwa hata watangazaji wa redio za dini nao walikuwemo katika kundi la wapokea rushwa. Na takwimu zikaonyesha pia kituo gani kati ya hivyo kinaongoza. Jambo la ajabu ni kuwa mwenye kituo kilichokuwa kinaongoza kwa kudai na kupokea rushwa toka kwa wanamuziki wa injili, alipopewa taarifa hiyo, alikuwa mkali na kusema kuwa ni njama za kuharibu jina lake binafsi, hata alipoelezwa kuwa taarifa ile aichukue imsaidie kusafisha kituo, hakutaka kukubali kuwa kuna tatizo katika kituo chake!!
 Jambo la faraja ni kuwa kumekuweko na taratibu ambazo zinaonyesha kuwa baadhi ya vituo vimejaribu kuweka taratibu za kujiondoa katika aibu ya kujihusisha na rushwa. Lakini wasanii wengi bado wana imani kuwa bila kutoa chochote wimbo wako hata uwe mzuri vipi hautasikika hewani.

Comments