NINI MATOKEO YA MAAMUZI YA KUZUIA MUZIKI WA NJE KUPIGWA KATIKA RADIO NA TV ZA SABC?


BAADA ya malalamiko ya wanamuziki wa Afrika ya Kusini kuhusu uchache wa muziki wao katika radio na TV za huko, shirika la utangazaji, South African Broadcasting Corporation (SABC) hivi karibuni lilitangaza kuwa litaanza kupiga muziki wa nyumbani kwa 90% katika vituo vyake 18 mara moja. Swala la ‘local music’ lilianza kulalamikiwa toka mwanzoni mwa miaka ya 90, lakini nguvu za kelele hizi zilizidi kuanzia Februari mwaka huu kutokana na kampeni za Don Laka, kiongozi wa wanamuziki na producer ambaye kwa kutumia mitandao ya kijamii aliweza kuonyesha jinsi  tabia ya vyombo vya utangazaji kupendelea kupiga muziki kutoka Marekani ulivyosababisha ukosefu wa mapato na ajira katika tasnia ya muziki Afrika ya Kusini. Hali ya kupiga muziki mwingi kutoka Marekani ulisababisha South African Music Rights Organisation (SAMRO) kupeleka asilimia kubwa ya mirabaha iliyokusanywa kutoka vyombo vya utangazaji kupelekwa nje kulipia mirabaha ya wanamuziki wa huko. Mwezi March mwaka huu, Independent Communications Authority of South Africa(ICASA) chombo kinachoratibu tasnia ya habari South Africa, kilipandisha mgao wa ‘local content’ kutoka 25% na kuwa 35% kwa vituo vya biashara, na kutoka 40% kwenda 60% kwa radio za kijamii. Pamoja na kupanda huku on wanaharakati wa swala hili walitaka asilimia hii ifikie 70%. Na hapo ndipo Laka na wafuasi wake waliojipa jina la  ‘SA Music Movement’ wakitumia kauli mbiu ya ‘nchi yangu muziki wangu” waliendelea kupigania kuongezeka asilimia ya ‘local content’.

Maamuzi muhimu

Jumatano tarehe 12 May, ndipo SABC ilipotangaza kuwa itafikisha 90% ya muziki wa nyumbani kwenye vituo vyake. Na pia shirika hilo likasema litapiga muziki wa wakongwe na wanamuziki wapya katika tasnia bila upendeleo. Wakati huohuo Chief Operating Officer wa SABC,  Hlaudi Motsoeneng alitangaza kuwa SABC ilitegemea kufungua kituo kipya cha TV ambacho kilikuwa na lengo la kukuza local content.

 Katika enzi za ukaburu vituo mbalimbali za SABC vilitumia lugha tofauti, hali iliyopo mpaka sasa, lakini SABC ya sasa ilitaka kila mwanamuziki wa Afrika ya Kusini ajione nyumbani kwenye kila kituo cha shirika hilo. Utumiaji wa asilimia hiyo mpya umepangwa kuanza tarehe 1, July 2016. Utaratibu huu utakuwa katika TV na radio.  Uongozi wa SABC ulisema utakuwa na mikutanao ya mara kwa mara na wadau kutathmini utendaji kazi wa SABC.


Uamuzi ulivyopokelewa na Laka na wanamuziki wengine

Kati ya watu waliokuwa na furaha kubwa kwa uamuzi huu alikuwa ni Don Laka, ambaye aliandika katika ukurasa wake wa Facebook “Thanks to everyone who supported this, I am very emotional at this stage. Thanks Bra Kaizer and Hlaudi, a bold leader who listened to my emotional plea to save our arts. This man shares the same vision as me. The people of SA: this is a chance to pride yourselves with your own culture!”

Chini ya picha ambayo Laka alikuwa anapeana mikono na kiongozi mmoja wa SABC aliandika haya  “Today I am proud to be a South African.  This man Hlaudi made me shed a tear for the first time in many years…. Freedom at last!“

Wakongwe wa muziki wa Afrika ya kusini nao walichangia kwa maneno yenye kuonyesha furaha kubwa Sipho ‘Hotstix’ Mabuse aliandika ‘Katika miaka yangu 50 katika muziki ni habari njema kwa SABC kupiga muziki kwa 90%. Viva SA music’. Producer Black Coffee aliandika’ Asante wakubwa, asante Don Lakakwa mchango wako”. Muimbaji wa R&B Danny K aliandika kuonyesha mshangao na kusema, “Hakika sikutegemea katika maisha yangu ntaona hii -90%”

Je, hali hiyo itadumu?

Wakati jambo lenyewe linafurahiwa kuna wanaouliza je, litadumu? Kwa vile SABC imeahidi kukutana na wadau mara kwa mara, inategemewa mazungumzo hayo yataonyesha dira kama swala hilo litakuwa la kudumu. Ukikumbuka kuwa SABC walisema kuwa jambo hilo litaanza kwa majaribio ya miezi mitatu. Hili jambo la kuweka majaribio ya miezi mitatu nalo limechukuliwa kuwa ni kikwazo. Ian Osrin  producer na sound engineer mwenye hadhi katika tasnia ya muziki Afrika ya Kusini, kisha sema ana wasiwasi na kipengele hicho kwani kinaweza kuwa ni njia ya kujipanga kurudia kwenye taratibu zilizozoeleka. Na kuwa ikiwa jaribio hilo litashindwa, basi kwa miaka 50 ijayo inawezekana hiyo ikawa kisingizio cha kutoongeza asilimia ya local content.

Wakati wanamuziki kwa ujumla wamefurahia hili watangazaji wengine wa SABC walikuwa na wasiwasi wa matokeo ya jambo hili katika mapato ya vituo vyao vikubwa vyenye wapenzi wengi ambavyo muziki wake ulikuwa hasa ni wa wanamuziki kutoka nje, hasa Metro FM na 5FM.

Je wanamuziki watapata fedha zaidi?

Lalamiko kubwa la Laka lilikuwa mamilioni ya dola hupelekwa nje ya nchi yao kila mwaka kulipia mirabaha, tena kuwalipa wanamuziki ambao ni matajiri sana tayari. Swali lilikuwa je kupiga huku muziki kutafanya wanamuziki walipwe zaidi na je  muziki wa ndani utanunuliwa zaidi? Mwana Hip Hop AKA anaamini kuwa hatimae wanaweza kuanza kuuza mpaka album milioni moja nchini mwao kwani wasikilizaji watasikia na kujua kazi zao. Kila mtu anasubiri kuangalia ikiwa hili litatokea.

Mwisho kuna wale ambao wanasema 90% ni juu mno, na hakika kampuni za nje zenye kutaka kuuza kazi zake SA hazitakaa kimya kwa hili. Korea ya Kusini iliwahi kuonja joto la Mmarekani lilipoweka local content kuwa 80%, USA ikaanza kutumia mabavu yake ya kisiasa kuishusha asilimia hiyo kwani ghafla mauzo ya kazi za Kimarikani yalishuka. Ubabe huu ndio uliofanya nchi kadhaa kukutana ka kutengeneza UNESCO Conventiona 2005, ili kulinda maamuzi ya utamaduni yasiingiliwe kama moja ya rejea katika  maamuzi ya kisiasa.

SABC ina vituo 18, japo hivyo ndivyo vyenye wasikilizaji wengi lakini kuna vituo 150 ambavyo havina uhusiano na SABC, Je, nini kitatokea?

Swala la muziki wa nje kuteka anga za nchi za Kiafrika si la Afrika ya Kusini peke yake, malalamiko kama haya yanaendelea Kenya, Tanzania na Gambia, je nchi nyingine zitafuata nyayo za SABC?

Comments