MTN NIGERIA YAPELEKWA MAHAKAMANI KWA MADAI YA KUTOLIPA MIRABAHA

CHAMA cha hakimiliki cha Nigeria, Copyright Society of Nigeria(COSON), kimeipeleka kampuni ya simu ya MTN mahakamani na kufungua shtaka la madai la naira bilioni 16 au kiasi cha shilingi bilioni 168 za Kitanzania, Shitaka hilo linatokana na kampuni hiyo ya simu kutolipa mirabaha inayostahili kwa muda mrefu. Kiwango hiki kinasemekana ni kikubwa zaidi kuwahi kudaiwa Afrika, kwa madai yanayohusiana na muziki. Hivi karibuni COSON na International Federation of the Phonographic Industry (IFPI),shirikisho la vyama vya watengenezaji wa santuri, zimetiliana saini makubaliano ya kufanya kazi pamoja hii ni kama imeizindua  COSON ambacho ndio chombo pekee cha ukusanyaji wa mirabaha kinachotambuliwa na serikali ya Nigeria, kuanza kukomaa na kudai na kulinda haki za wadau wanaofanya kazi katika tasnia ya muziki kwa nguvu mpya.
Kutokana na maelezo rasmi ya COSON, hatua ya kwendaa mahakamani imekuja baada ya taratibu za kuikumbusha MTN mara kadhaa kuhusu wajibu wao wa kulipa mirabaha  kupuuzwa. Taarifa hiyo ilisema “COSON imefanya mambo kadhaa ikiwemo matangazo kupitia vyombo vya habari, na pia kutumia fedha nyingi kuitaarifu MTN kuhakikisha inapata ruksa stahiki toka kwa wenye muziki na kulipia mirabaha stahiki, lakini MTN ilikuwa ikijifanya kama iko juu ya sheria, wakati COSON imekusanya na kugawa mamilioni ya naira kwa wanachama wake, na washirika wake, hakuna hata senti iliyotoka MTN, ambayo hujisifu kuwa ndio kampuni kubwa kuliko zote kwa kusambaza muziki, na kujinadi kuwa ni rafiki wa wanamuziki” MTN ilikuwa ikijikatia asilimia 60 mpaka 70 ya mapato yaliyotokana na Caller Ring Back Tune (CRBT), asilimia 30 mpaka 40 iliyobaki ndio ambayo iligawanywa kwa Value Added Service, label za records, msanii na malipo mengine. Mgao huu uliwahi kulalamikiwa na D’Banj katika mkutano wa Nigerian Entertainment Conference uliofanyika karibuni jijini Lagos.
Kesi hii inakuja mara baada ya MTN kushindwa kesi nyingine mwaka 2015, na kulazimishwa kulipa faini ya kiasi cha shilingi bilioni 10,920, kwa kuendelea kuwahudumia wateja ambao hawakuwa wamesajiliwa, jambo lililopelekea Sifiso Dabengwa aliyekuwa CEO wa MTN Group of Companies kujiuzuru. Huko South Africa kwenye makao makuu ya MTN, kampuni hiyo karibuni ilijikuta kwenye matatizo ya kuonekana haijalipa mirabaha tokea mwaka 2013, hivyo ikawa inadaiwa na chama cha watunzi Composers, Authors and publishers Association ( CAPASSO), japo MTN ilitoa tamko kuwa haidaiwi na CAPASSO wala chama kingine chochote, iliomba kupewa invoice mpya na ikamaliza deni husika mara moja. Wakati huohuo Mwenyekiti wa COSON Tony Okoroji aliapa kuwa chama chake kitahakikisha kinalinda Hakimiliki kwa nguvu zaidi hasa kipindi hiki ambacho pato la Taifa limeshuka kutokana na bei ya  mafuta kushuka. ‘Tunataka kazi ya wanamuziki na waliowekeza katika muziki ambao hufanya kazi ngumu kila siku ya kuhakikisha watu wanafurahi walipwe stahili zao, haiwezekani wao wawafanye watu wawe na furaha lakini wao wawe na uchungu, muziki wetu na filamu zetu zinatakiwa kote duniani, mapato yake yanatakiwa kuchangia pato la Taifa hasa kipindi hiki cha kuanguka kwa bei ya mafuta, alimaliza kwa kusema, there will be no untouchables and no sacred cows; no retreat, no surrender!”

Comments