Mhe Nape M Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo |
Rais John Pombe Magufuli ameunda Wizara mpya itakayoshughulikia pia wasanii. Katika kutangaza baraza jipya la mawaziri ambalo hakika litakuwa dogo kama alivyoahidi wakati wa kampeni, pia Ria amekuja na Wizara mpya. Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo. Waziri aliyeteuliwa ni Mheshimiwa Nape Moses Nnauye. Kwa wengine tuliomo katika Wizara hii hakika tunaona tunahitaji mabadiliko mengi, yakiwemo uongozi wenye uzalendo wa kupenda utamaduni wa Kitanzania, pia uongozi utakaotengeneza na kuheshimu mtiririko wa uongozi wa kiserikali wa shughuli za Utamaduni. Pia tungependa uongozi ambao unakubali kusikiliza pande zote za wadau wa tasnia ya sanaa. Uongozi ambao utaelewa tofauti kati ya Utamaduni, sanaa na burudani. Uongozi ambao utakuwa wa kwanza kuhakikisha sheria na taratibu zihusuzo sanaa zinafuatwa. Tuna uhakika Mheshimiwa Nape atayaweza haya na zaidi, hivyo kuweza kuweka kumbukumbu ya uwepo wake katika historia ya sanaa ya nchi hii. Bado jina la Wizara linaleta chemsha bongo katika kipengele cha wasanii, je Wizara itahusika na wasanii au Sanaa? Najua inawezekana likaonekana ni swali la ajabu lakini ukukikumbuka tu kuwa kuna wizara ya kilimo sio ya wakulima, au wizara ya biashara na si ya wafanyabiashara, kuna wizara ya uvuvi si ya wavuvi, ni mifano michache ya kuonyesha changamoto hii.
Comments