TAARIFA KWA UMMA YA TBN
KUMUOMBA MH. RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE
ASIPITISHE
MUSWADA WA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAONI,
2015
Mtandao wa waandishi kupitia mitandao nchini, Tanzania Bloggers Network (TBN)
tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete
kutumia mamlaka yake vyema kwa kutokupitisha muswada wa Sheria ya Makosa ya
Mtandao, 2015 unaokandamiza uhuru wa mawasiliano mitandaoni.
Muswada wa sheria ya makosa ya Mtandaoni unaainisha
makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano, na kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi
wa kieletroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.
MUSWADA WA
SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAONI, 2015
Umoja huu (TBN) ulishtushwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kukubali kupitisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao
2015 kwa hati ya dharura kitendo ambacho hakikutarajiwa kutokana na kuwa
mitandao bado ni kitu kipya nchini hivyo tulihitaji maridhiano na wadau na
elimu kati ya raia na Serikali ili wengi watambue yapi ni makosa kwa kutumia
mitandao na yapi yanakubalika.
Kimsingi TBN haipingi Tanzania kuwa na Sheria ya
Makosa ya Mtandao bali inaiomba Serikali kuwashirikisha wananchi na hasa wadau
wa habari na wanamitandao ya jamii ili kuridhiana kwa vipengele ambavyo
vinaonekana kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Na hatimaye kutoka na
sheria isiyo na viashiria kandamizi juu ya uhuru wa kupata na pokea habari.
Hali kadhalika tulishuhudia watetezi wa haki za
binadamu pamoja na wawakilishi wa watumiaji wa Mtandao wa intaneti nchini
wakitoa sababu zenye uzito za kwanini sheria hii isipite kwa hati ya dharura na
kuhoji kwanini sheria hii ipite kwa dharura bila ya kupata majibu.
Muswada huu ambao kati ya makosa mengi uliyonayo kubwa
moja wapo ni majukumu makubwa aliyopewa Mkuu wa Kituo chochote cha Polisi kuwa
na uwezo wa kupekuwa na kuchukua vielelezo/data pale anaposhuku kuna suala la
uhalifu unaohusu mtandao. Swali ni kuwa kwanini polisi apewe mamlaka ya
kumsulubisha mtuhumiwa katika hatua ya mwanzo bila uthibitisho wa sahihi?
Mbali na hapo, sisi kama waandishi ulimwenguni kote
tunatakiwa kufuatilia maadili ya kazi zetu. Maadili ya mwandishi yeyote yule ni
kutunza usiri wa chanzo cha habari yake pale inapotakiwa lakini katika sheria
hii sisi kama bloggers, sheria hii
inakiuka hili kwa kutulazimisha kutaja vyanzo vya habari.
Kupitia sheria hii, bloga yeyote yupo hatarini
kutokana na kwamba sheria inaainisha ni kosa la jinai kutoa ujumbe unaoweza
kumuudhi mtu kihisia.
Aidha, tunamuomba Mheshimiwa Rais pia asipitishe Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka
2013.
Muswada huu unavinyima uhuru vyombo vya habari
vinavyotangaza takwimu mbalimbali. Kama ilivyo Ibara ya 7(4) ‘‘Chombo chochote cha habari ambacho
kinachapisha taarifa za kitakwimu za uongo au upotoshaji, au kinatangaza
kipindi chochote kinachohusu shughuli za ukusanywaji wa taarifa ambayo
imefanywa au inafanywa na Ofisi, na hatimaye kusababisha wananchi wasishiriki
kwenye shughuli hiyo ya ukusanywaji wa taarifa au wasishirikiane na maafisa wa
Ofisi, kinatenda kosa.’’
Hii iki maanisha kuwa hata blog zetu ziko hatarini
kuelekea katika kulazimika kufanya kazi za kuisifia serikali na kutangaza
takwimu zilizopitiwa na serikali tu, jambo ambalo litaharibu ukuaji wa uhuru wa
habari nchini.
Tunamkumbusha mwananchi wa kawaida
anayetumia mtandao wa intaneti kuwa hayuko salama kwani sheria hii
inamlazimisha mtoa huduma wa mtandao kutoa taarifa za wateja wake jambo ambalo
linahatarisha uhuru wa kutoa na kupokea habari.
Mungu Ibariki
Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
IMETOLEWA NA;
Chama cha
Bloggers Tanzania (Tanzania Bloggers Network-TBN)
04/03/2015.
Comments