WASANII NA HAKI ZAO KATIKA KATIBA MPYA, SAFARI YA MAFANIKIO


Kati ya Jumatatu tarehe 25, 26 na 27 Agosti 2014, kundi la wasanii 27 lilifika katika Bunge la katiba kufuatilia mapendekezo yao katika Katiba ambayo waliyoyatoa kuanzia katika hatua za mwanzo za mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi. Kwa kutumia haki anayostahili kila mwananchi wasanii hawa waliweza kukutana na kuzungumza na Mwenyekiti na makamu Mwenyekiti wa Bunge la katiba na baada ya hapo kutembelea na kujieleza katika kamati mbalimbali za Bunge hili. Wasanii wana mambo mawili ambayo wanahitaji yaweko katika Katiba

i.                Wasanii kutambuliwa kama kundi maalumu kama yalivyotambuliwa makundi ya wakulima wafugaji, wavuvi. Sababu za kutaka kutambuliwa huku, ni kuwa kundi hili ni kubwa kuliko hata makundi mengine yaliyotajwa hapo juu. Takwimu za Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2006 zinaonyesha kuwa wasanii nchini walikuwa kiasi cha milioni 6. Leo ni mika minane imepita na si siri kuwa kundi hili limekuwa na hivyo kukaribia robo ya Watanzania. Kwa bahati mbaya jamii huchukulia neno wasanii kuwa ni wale wa muziki na filamu tu, lakini sanaa ni pan asana na hivyo kuwa na watu wengi sana hata wengine hawajui kama wamo katika kundi hili. Wachoraji, wachongaji, wasusi, wafinyanzi, mafundi sonara, mafundi wa nakshi za aina mbalimbali, wabunifu wa mitindo, waandishi, wapiga piga picha, watangazaji, djs, wahariri, na kazi nyingi ambazo unaweza kujaza ukurasa huu kuziandika, hao wote wanahitaji kutengenzewa taratibu zikiwemo za elimu rasmi ya vipaji vyao, taratibu za ukuzaji na uendelezaji wa kazi hizo na hatimae kuboresha mchango wao wa mapato yao na mapato ya Taifa kwa ujumla.



i.              Milikibunifu (Intellectual Property) itajwe rasmi kama moja ya aina za mali zinazohitaji kulindwa katika katika Katiba.  Katika katiba kuna Ibara (Ibara ya 37) inayoongelea ulinzi wa mali. Lakini mali zinazoongelewa hapa ni zile zinazohamishika na zisizo hamishika. Lakini kuna mali muhimu ile isiyoshikika haikutajwa ulinzi wake. Pamoja na kuwa wasanii kwa kawaida hulindwa na hakimiliki, lakini haingekuwa busara kushikilia kipengele hicho tu kutajwa kwenye Katiba, kwani ni sehemu tu ya Milikibunifu ambapo kuna Haki nyingine kama vile ;
·      Patent – (Hataza) hii ni njia ya kulinda na kusajili uvumbuzi mbalimbali wa kiteknolojia. Mfano vifaa vya kuvunia mazao kwa haraka zaidi, au kulima kwa haraka zaidi, vifaa vya uvuvi wa haraka, vifaa vya mawasiliano na vifaa vyovyote ambavyo vitaongeza thamani ya maisha yetu. Katika nchi kama Korea ya Kusini ulinzi wa Milikibunifu uliwekwa katika Katiba kuanzia baada ya vita ya pili ya dunia kwa kufuatia mfumo wa  Katiba ya Marekani na ulinzi huo umeifanya wananchi wake ambao ni wabunifu kuweza kuja naubunifu ambao unatikisa dunia vifaa kama Samsung, Daewoo, KIA, LG ni matokeo ya ulinzi wa kikatiba wa wa Milikibunifu
·      Trademarks – (Alama za Biashara ) Alama za biashara huweza kufikia hatua ambapo zikawa na thamani kubwa kwani huweza kuaminika. Ili kulinda zisitumiwe hovyo au hata kuibiwa na wenye uwezo zaidi hulindwa na sheria za kulinda alama hizi. Kwa mfano Cocacola, Vodacom, Dell, na hapa kwetu Azam, ni majina ya bidhaa ambazo zina aminika, na hivyo kuwa na dhamani kubwa japo hazishikiki, nazo ni sehemu ya mali  ambazo hazishikiki lakini zina thamani kubwa
·      Industrial designs – Hizi ni haki wanazopewa wale wenye ubunifu wa kuweza kufanya usanii wenye kuboresha muonekano wa kitu ambacho tayari kimeshagunduliwa. Kwa mfano kila mtu ana simu ya mkononi lakini muonekano wa simu mbalimbali shape nap engine hali ya kuwa ni ya ku slide au kufungua au kupokea moja kwa moja ni matokeo ya design, pia vitu kama design za nguo, viatu , kiti ulichokalia makochi magari, vyote hivyo ndivyo matokeo ya industrial designs. Kazi za ubunifu huo ni muhimu kulindwa kwani huwa na thamani kubwa sana, kwa mbunifu na kwa mchango wake kwa nchi.
·       Geographical Indication – Huu ni utambulisho wa wapi chanzo cha mali husika. Kwa mfano mvinyo kutoka Dodoma, Dodoma Wine ni mzuri na hivyo huitwa Dodoma Wine bila kulinda hili, watu watachukua mvinyo huu na kuupa hata jina jingine ukaitwa South African wine na hivyo kuiba haki wanazostaili kupata wakulima wa Dodoma, kutambuliwa kwa jina hili kutasababisha kutakiwa zaidi kwa wine hii duniani na hivyo kuweza kufanya hata Dodoma kuwa Wine City jambo ambalo linawezekana lakini nchi haijatambua umuhimu huu. Pia kuna mchele wa Kyela, Dagaa wa Kigoma na vitu kama hivi ambavyo havipatikani popote duniani kasoro sehemu iliyotajwa.  Nchi kama Uswiss imejenga jina miaka mingi ya utengenezaji wa saa bora hivyo saa ikiandikwa Swiss made huwa inajulikana ni bora na huwa gharama zaidi, Sigara kutoka Cuba, Cuban Cigars ni bei kubwa kwani hazipatikani popote kasoro Cuba, au mvinyo maarufu kama Champagne, ambao hutoka jimbo la Champagne Ufaransa, umejijengea sifa kubwa duniani na kuwa na bei kubwa sana kiasi cha kwamba si rahisi kwa mtu wa kipato cha kawaida kununua. Harusi zetu hutumia Sparkling Wine na kuiita Shampeni.
·      Hakimiliki na Hakishiriki – Hizi ni haki zinazolinda kazi za kisayansi na kisanii. Computer Programs, Data, Utunzi wa vitabu, miswaada, hotuba, uchoraji, muziki, kazi za usonara, picha za mnato na filamu, uchongaji na kadhalika. Kazi hizi zimekuwa ni chanzo cha utajiri mkubwa kwa watu binafsi na Mataifa. Katika nchi ya Marekani kazi za Hakimiliki na Hakishiriki ni za pili katika uchangiaji wa pato la Taifa. Ripoti ya WIPO ya 2010 ilionyesha kuwa katika nchi ya Tanzania kazi za hakimiliki na Hakishiriki zilichangia asilimia 4.3 ya pato la taifa, karibu mara mbili ya mchango wa Madini!. Katika mwaka 2009 kazi za hakimiliki zilitengenza aslimia 5.63 ya ajira nchini, ikiwa juu ya mchango wa Afya (4.23), Biashara na mambo ya Fedha Real estate, &Business Service(2.37), Ujenzi (1.38),Usafirishaji na Mawasiliano (0.92), Umeme, Gas na maji (0.91), Madini (0.89) .
Ukiangalia utaona wazi kuwa Milikibunifu ni haki zinazolinda wavumbuzi, watafiti, wanasayansi, wagunduzi wa madawa, ya kisasa na kiasili, wavumbuzi wa mbegu za aina mbalimbali, ulinzi wa alama za biashara hivyo wasanii wameweza hata kuwasaidia wenye viwanda wakulima na wafanya biashara wakubwa katika safari yao hii iliyoanza mwaka jana.
Baadhi ya hasara ambazo Taifa hili limepata kutokana na kutokuwa na taratibu zifaazo katika kulinda Milikibunifu;
a.     Michoro ya Tingatinga milikibunifu yake iko chini ya kampuni ya Walt Disney ya Marekani
b.     Mgunduzi wa Tanzanite ni maskini ambaye amekuwa kwa muda mrefu akijitahidi kupata chochote kutokana na ugunduzi huo ameishia kupata vyeti vya kumtambua  wakati India na South Africa vikitambulika zaidi kuwa chanzo cha madini hayo yapatikanayo Tanzania tu
c.      Ulaghai mkubwa wanaofanyiwa wasanii wa Tanzania kwa kazi zao kutumika masaa 24 na vyombo vya habari wakati wao hawalipwi chochote kwa kisingizio cha promosheni
d.     Wagunduzi wengi kazi zao zikiishia kuonekana kwenye maonyesho tu na hakuna taratibu za kuendeleza kwa kazi hizo wala wabunifu hao
e.     Nchi kukimbiwa na wabunifu wa teknolojia , ambao huona ni heri waende nchi nyingine ambako watathaminiwa, au wabunifu kuacha kufanya ubunifu wowote  kwani hauna faida.


Comments