MBARAKAH OTHMAN WA SIKINDE AONJA JUKWAA LA MSONDO

MBARAKAH OTHMAN
 MPULIZAJI tarumbeta mkongwe, Mbaraka Othman amefichua kuwa, anaichukia kupita kiasi bendi ya Msondo Ngoma Music, licha ya jana kuonekana kupanda kwenye jukwaa lao na kushiriki kupiga baadhi ya vibao vya zamani. 
Mbaraka aliyasema hayo jana, muda mfupi baada ya kutelemka kwenye jukwaa la Msondo alipopanda na kusaidia kupuliza tarumbeta kwenye vibao ‘Piga Ua Talaka Utatoa’, ‘Kaza Moyo’ pamoja na ‘Kilio cha Mtu Mzima’.
Huku akishangiliwa na baadhi ya mashabiki, Mbaraka alipanda kwenye jukwaa la Msondo majira ya saa 7:00 usiku na kujiunga na wapulizaji tarumbeta wa bendi hiyo, Roman Mng’ande, Hamis Mnyupe pamoja na mkali wa Domo la Bata, Shaaban Lendi.
“Nimepanda kujifurahisha tu, lakini sina mpango wowote na bendi ya Msondo,” alisema Mbaraka alipoulizwa kama ana nia ya kujiunga na Msondo.
Alisema, alikuwa anarudi nyumbani kwake jirani na hapo walipokuwa wakitumbuiza Msondo, akitokea DDC Kariakoo wakati huo, baada ya kumaliza shoo na bendi yake ya Mlimani Park Sikinde, ndipo alipokatiza kusalimia wanamuziki wenzake.
Alisema kuwa, mbali ya baadhi ya wanamuziki wa Msondo kumsifu aliposhuka jukwaani, bado katika maisha yake hatarajii kuwa siku moja atakuja kujikuta akiitumikia bendi hiyo, hata kama ataahidiwa donge nono.  Picha mbalimbali za onyesho la Msondo usiku huo hizi hapa....
Comments