HASHIM Said ‘Igwe’ mwimbaji pekee wa kiume anayeonekana kumkimbiza kwa kasi Mzee Yussuf ‘Mfalme’ kwenye mipasho, aling’ara zaidi kwenye shoo ya kundi lake la Mashauzi Classic Modern Taarab.
Shoo hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni, jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kuhudhuriwa na zaidi ya mashabiki 250, walioonekana kufurahia vilivyo burudani ya vijana wa Mashauzi wanaotumia mtindo wa ‘Wakali wa Kujiachia’.
Aliimba nyimbo tatu kwa awamu tofauti, ambazo ni zile mbili alizorekodi yeye akiwa na kundi hilo lililo chini ya Mkurugenzi Isha Ramadhani; ‘Bonge la Bwana’ na ‘Niacheni Nimpende’ pamoja na nyingine ya kukopi iitwayo ‘Mazoea Yana Taabu’.
Mbali ya Hashim, wasanii wengine waliofunika kwenye shoo hiyo ya jana ni pamoja na waimbaji Isha mwenyewe, Zubeda Malick, Asia Mzinga, Abdulmaliki Shaaban na Sania Msomali.
Kuonekana kwa mpapasa kinanda Mgeni Kisoda kwenye shoo ya Mashauzi Classic kumeibua hali ya ‘sintofahamu’ kwa mashabiki waliokuwa na kiu ya kufahamu kama msanii huyo amejiunga rasmi na kundi hilo.
Shoo ya Mashauzi ilipoanza tu, Kisoda alionekana mara kwa mara akipanda jukwaani na kubonyeza vitufe vya kinanda kimojawapo kati ya vile viwili na kushangiliwa na baadhi ya watu wanaomhusudu.
Katika nyimbo nyingine zilizokuwa zikirindimishwa katika ukumbi wa Mango Garden, Kisoda alikuwa akipapasa kinanda kwa staili ya hisia, yaani bila kufuatisha kilivyorekodiwa awali.
Hata hivyo, mashabiki walionekana kufurahia ubunifu huo wa Kisoda ambaye tayari alishapitia bendi kadhaa kubwa, zikiwamo Jahazi Modern Taarab na African Stars ‘Twanga Pepeta’.
Baada ya shoo kumalizika, mwandishi wa habari hizi alizungumza na Meneja wa Mashauzi Classic, Ismail Sumalaga ambaye hata hivyo hakuwa tayari kuzungumzia suala la Kisoda akidai wakati wake bado.
Comments