WANAMUZIKI WAFANYA MKUTANO


TAMUNET- Mtandao wa Wanamuziki Tanzania umefanya mkutano katika ofisi za mtandao huo, jirani na Kinondoni Mahakamani, ambao wanamuziki na viongozi wa bendi walialikwa katika kuongelea changamoto zinazoikabili tasnia hiyo. Mkutano huo ulianza kwa Mwenyekiti wa Mtandao John Kitime kutoa ripoti ya utendaji wa Mtandao huo toka ulipoanza na changamoto ambazo Mtandao umepitia.
Baadhi ya mafanikio ya Mtandao huo ni kukamilisha ripoti iliyofadhiliwa na BEST AC ambapo kwa kutumia mtaalamu kutoka Afrika ya Kusini waliweza kutengeneza ripoti iliyoitwa  Study on Artists Copyright Management& Royalties Collection and Distribution in the Tanzania Music Industry. Ripoti hii ilionyesha changamoto za ukusanyaji na ulipaji wa mirabaha kwa wanamuziki wa Tanzania. Nakala ya utafiti huu ilikwisha wasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ili kuwezesha TBC ambayo ni redio  na TV ya Taifa kuanza kulipa mirabaha kadri ya maelekezo ya sheria ya Hakimiliki na hakishiriki. Bahati mbaya mpaka sasa Wizara haija onyesha ushirikiano kwa hili.
Mtandao pia umeshiriki katika kuwasilisha kwenye Bunge la katiba mapendekezo makuu ya wasanii, i. Wasanii kutajwa  katika Katiba kama kundi maalumu kama walivyotajwa wakulima, wafugaji na wavuvi, kwa kuwa idadi ya wasnii ni kubwa sana, wanaingiza kipato kuliko wavuvi, na inaajiri watu wengi kuliko wavuvi. Pia Mtandao umeluweko katika mchakato wa kutengeneza sera ya Milikibunifu.
Mtandao ni mwananchama wa International Federation of Musicians na mwenyekiti aliwaasa wanamuziki kutumia fursa zinazotokana na uanachama wa shirika hilo.
Kikao kilamua kutengeneza kamati ya kukutana na wanamuziki katika sehemu zao za kazi ili kuongeza wanachama. Na pia kuangalia shughuli za kijamii ambazo wanamuziki wanaweza kufanya kama mchango wao kwa jamii.
Baada ya chakula cha mchana wajumbe walitawanyika

Comments