MAONI YA WACHAMBUZI KUHUSU MWENENDO WA MUZIKI WA DANSI NCHINI 1

Baadhi ya wanamuziki na wadau waliohudhuria

SIKU YA JUMAMOSI TAREHE 5/4/2014 TBC TAIFA WALIWEZA KUTAYARISHA MJADALA WA WAZI AMBAO WANAMUZIKI WA DANSI WALIKARIBISHWA KUJADILI MSTAKHABARI WA SEKTA YAO. PAMOJA NA MAONI YALIYOTOLEWA KATIKA KIPINDI HICHO, WAPENZI NA WACHAMBUZI WA TASNIA HII NAO WAMEKUWA NA MAONI MENGI KUHUSU HALI HII HAPA NI BAADHI YA MAONI 
1.     SAMPU MUSSA SAMPU aliandika hivi katika ukurasa wa Facebook
Tarehe 05/04/2014, kulikuwa na mjadala wa wazi kuhusu 'kudorora' kwa muziki wa dansi nchini. Mjadala huo ulirushwa hewani moja kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa (TBC-2). Nasikitika sana kuukosa mjadala huo muhimu, licha ya maandalizi niliyokuwa nimeyafanya.
Nilipanga (kama ningehudhuria) kuzitaja na kuziainisha sababu kuu zilizoua muziki wa dansi nchini, baadhi ni hizi hapa:
1. Wasanii wenyewe kutokuheshimu kazi yao, na kuifanya kwa mazoea, hii inapelekea:
(a) Wasanii kutunga nyimbo hovyohovyo!
(b) Kuimba hovyohovyo!
(c) Kupiga vyombo hovyohovyo!
(d) kupangilia muziki hovyohovyo!
2. Muziki wa dansi kupigwa ''bao'' na muziki wa taarabu (mipasho) na muziki wa injili! Hapa nifafanue kidogo:
Hivi sasa muziki wa taarabu unapigwa na kuchezwa kama dansi! Taarabu imeacha asili yake na sasa inapigwa na kuchezwa kama ilivyo dansi! Muhimu zaidi kulifahamu ni kwamba, taarabu inapigwa kwenye kumbi zilezile za dansi (hususani ndani ya ma-bar)!
Muziki wa injili nao hali kadhalika, umechukua vionjo karibu vyote vya dansi na sasa wanapiga dansi kamili (ukiachilia mbali ujumbe)! Hii maana yake ni kwamba, mashabiki wengi wa dansi wamekimbilia kwenye taarabu na muziki wa injili kwenye msisimuko zaidi!
MUHIMU ZAIDI: Muziki wa taarabu na ule Injili, unapata 'airtime' ya kutosha kila siku! Mathalani, taarabu wana wawakilishi (watangazaji maalum) karibu kila redio (ukiondoa redio za dini), na unapigwa kwelikweli! Kadhalika muziki wa injili, unapigwa kila siku kupitia redio zao husika!
Muziki wa dansi hauna wawakilishi kabisa katika media ukilinganisha na muziki wa taarabu na ule wa injili!
3. Studio za kiwango cha chini sana! Nifafanue kidogo hapa:
Wasanii wa Congo, wao hufanya recordings zao Ulaya na hata mauzo ya kazi zao yanaanzia hukohuko Ulaya ndiyo inakuja Afrika. Na hii ndiyo siri kubwa ya muziki wao kuwa maarufu duniani kote.
4. Kupiga muziki kila wiki! Hii inawachosha wote, wasanii na mashabiki!
5. Kutegemea gate collection. Hapa naikumbuka OMACO.
6. Muziki kupigwa sehemu moja (Bar) tena usiku tu!

 **************************************************************************
 
FREDDY MOSHA alisema……….Tathmini yangu fupi na ya kijinga kuhusu mdahalo wa Jumamosi hii: Nilibahatika kuangalia licha ya kuwa si kwa urefu wake mdahalo uliowajumuisha wanamuziki na wadau wa muziki wa dansi Tanzania uliojikita kujadili namna ya kuukwamua muziki wa dansi nchini. Kwanza nitoe hongera sana kwa waliohudhuria na pia muandaaji wa mdahalo ule na kwa ujumla wake nilifurahishwa na kilichojadiliwa kwa kuwa yote yaliyojadiliwa yalikuwa na dhima ya kujenga. Kama ningekuwepo mimi pengine mchango wangu ungejikita kwenye sehemu zifuatazo, Nafasi ya wanamuziki wenyewe, Nafasi ya wamiliki wa bendi, Vyombo vya habari na wadau wenyewe.
WANAMUZIKI WENYEWE
Wanamuziki bado wanayo nafasi kubwa tena nadiriki kusema kuwa ni nafasi kubwa kuliko zote katika kukuza na kuutanua muziki wa dansi kupitia tungo zao na kwa ujumla kazi wanazozifanya. Hata hivyo katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia tungo zisizo na mashiko za wanamuziki wetu wa dansi kiasi kwamba hata hadhira haielewi nini kisa hasa cha wimbo husika. Kwa kifupi hakuna mtiririko wa hadithi ama kisa cha wimbo husuka na badala yake wimbo unaweza kubebwa na maneno machache yasiyokuwa na maana na wakati mwingine kuibua Tafsiri sisisi zinazojielekeza kwenye matusi. Ni vizuri kwa wanamuziki wenyewe kujiuliza NATUNGA NINI na KWA WAKATI GANI na NATAKA KUELEZA NINI ili kazi zao zifanikiwe. Pia kuna baadhi ya wanamuziki ama wenyewe wanaojiita watunzi kuwa ati kuna nyimbo za kufurahisha tu bila kuelewa kuwa muziki kama Fasihi zingine ina pande kuu mbili, fani na maudhui, kwa maana ya ujumbe kwenda sanjari na ufundi unaotumika. Naweza kusema kuwa fani ma maudhui ni vitu visivyotenganishwa kabisa. Ni vizuri pia kwa watunzi kuhakikisha kuwa nyombo zao zina alama {Identity} zinazowatofautisha wenyewe ama bendi na bendi kuliko hivi sasa ambapo muziki wa bendi nyingi hasa hizi za kisasa unafanana kiasi kwamba hujui hiyo ni bendi gani na kama unapata mtangazaji muongo anakuongopea hivihivi
WAMILIKI WA BENDI
Wako baadhi ya wamiliki wa bendi nchini huamua kuingia kwenye biashara ya muziki biloa kufanya utafiti kuhusu nini kinahitajika kwenye soko la muziki ama nini kifanyike ili kulishika soko hilo. Baadhi yao huwalazimisha wanamuziki wao kupiga nyimbo kwa mitindo ambayo bila shaka si kwa matakwa ya wanamuziki wenyewe, bali hata kwa matakwa yao. Mbali na hilo mipangilio madhubuti inapaswa kuwekwa na wamiliki hao katika kukuza muziki huu kupitia makundi wanayoyamiliki.
VYOMBO VYA HABARI
Katika hili vyombo vya habari vina mchango mkubwa wa kuandika na kuripoti habari zinazohusiana na muziki wa dansi nchini. Kwa bahati mbaya siku hizi, vyombo vyetu vya habari vinazidi kuupiga teke muziki wa dansi ikilinganishwa na aina zingine za muziki kama Bongo Flavour ama Taarab. Siku hizi haishangazi kuona mwandishi wa habari ama mtangazaji akikwambia kuwa kupenda muziki wa dansi ni sawa na kupenda nyimbo za kizee. Sishangai kwa hili kwa sababu hasa ya umri kwa kuwa wengi wa watangazaji wanaofanya kazi kwenye vyombo hivi hawazidi hata miaka thelathini hali ambayo inawafanya kutojua lolote kuhusu muziki huo. Hata hao waliopo na wanaofanya vipindi vinavyohusiana na muziki huo, hawana ufahamu wa kutosha wa muziki wa dansi kiasi kwamba, wanachokitangaza ama kukiandika kupitia vyombo hivyo kinazidi kupotosha ukweli wa muziki wenyewe, jambo ambalo ni la hatari.
WADAU WA MUZIKI.
Hasa waliomo kwenye hiki kijiwe kuhakikisha kuwa tunawaambia ukweli wanamuziki waliomo humu badala ya kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa. Baadhi ya wanamuziki hawapendi kuambiwa ukweli kuwa wanaharibu ama wanachotakiwa kukifanya ni kuongeza bidii katika kazi zao na kuzifanya kuwa bora. Badala yake tunatumia muda mwingi kupeana sifa zisizo stahili, sifa ambazo kwa hakika hazijengi na badala yake zinawafanya wanamuziki kuvimba vichwa na kujiona wanajua kumbe hali ni tofauti. Hata hivyo angalizo ni kuwa lugha inayotumika kukosoa ni lazima iwe ya staha na isiyoiudhi ili kuwafanya hata wanaokosolewa kujisikia vizuri na kukubali kukosoana. Lugha za kuudhi zinasababisha mmomonyoko badala ya kujenga. Ikumbukwe pia vijiwe kama hivi husaidia kudumusha urafiki hata udugu na hivyo kusaidiana hata kwa mambo mengine yasiyo ya kimuziki. Ni hayo tu, mengine ntaandika kila nikipata wazo jipya

Comments