Utangulizi
Baada ya maagizo kutoka Tume ya
Katiba ya kuwa kila kundi kutayarisha mapendekezo ya rasimu ya Katiba, wasanii
nao chini ya mashirikisho yao manne Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Muziki,
Shirikisho la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za ufundi waliweza kuja na mapendekezo kadhaa
ambayo waliyawasilisha katika Tume, kwa bahati mbaya hakuna kipengele chochote
cha mapendekezo hayo kilicho ingizwa katika Rasimu ya Katiba. Kwa ushirikiano,
Mashirikisho haya ya sanaa yameamua kufikisha mapendekezo yao moja kwa moja kwa
Wabunge wa Bunge la Katiba ili kuwezesha vipengele hivyo kuweko katika Katiba
yetu mpya.
Mapendekezo
1.
Kutambuliwa
kwa wasanii kama kundi maalumu katika Katiba.
Katika Rasimu ya Katika kuna
makundi maalumu kadhaa ambayo yametajwa, kama vile wakulima, wavuvi, wafugaji,
na kadhalika na hivyo kutambuliwa
kikatiba. Wasanii ni kundi kubwa katika jamii ya Kitanzania. Wasanii wapo
karibu katika kila kaya Tanzania. Wafinyanzi, wasusi, wapambaji, wanamuziki
waigizaji, mafundi mbalimbali wa ushonaji ujenzi na kadhalika, wako wengi wala
hata wao hawajitambui kama ni wasnii kutokana na mazingira waliyomo. Katika
ripoti mojawapo ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati huo
ilikuwa ni milioni 6, ni wazi kuwa idadi hiyo kwa sasa itakuwa imepanda. Katika miaka ya karibuni vijana wengi
wamekuwa wanaongezeka kujiunga na kundi hili kwani katika sanaa kumekuwa na
uwezekano wa kujipatia ajira, tena isiyokuwa na ukomo. Na hivyo sanaa kwa sasa
si utamaduni peke yake bali ni sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania. Wasanii ni
sehemu muhimu katika sekta ya Hakimiliki, takwimu za ripoti ya WIPO(World
Intellectual Property Organisation) ya mwaka 2010, kuhusu mchango wa sekta ya
hakimiliki katika uchumi wa Tanzania, inaonaonyesha kuwa sekta hii, kati ya 2007-2010 ilichangia kati ya
asilimia 3-4.6% ya gross domestic product(GDP). Na kiasi cha kati ya TSH 38.930
bilioni na 86.686 billion kilipatikana kama kipato cha walioajiriwa katika sekta
hiyo. Kati ya watu 28, 202 na 44, 331 waliajiriwa rasmi, na hiyo ilikuwa kati
ya asilimia 4.5 na 5.2% ya kundi zima la waajiriwa wa Taifa hili. Kwa kipimo
cha GDP, sekta hii ilikuwa zaidi ya sekta ya madini, ambayo wote ni mashahidi
imekuwa katika mazungumzo kila kona ya nchi. Na katika ajira sekta hii ilikuwa juu
zaidi ya sekta nyingi zikiwemo madini, usafirishaji, mawasiliano, afya na
ustawi wa jamii, maji, gesi, na hata ujenzi. Kwa mchango wa sekta hii wa 3.2%
katika GDP kwa mwaka 2009 , umeweka sekta hii kuwa bora kuliko sekta za aina
yake katika nchi kama Croatia 3%,
Singapore 2.9%, Latvia 2.9%, Lebanon 2.5%, Kenya 2.3%. Na katika mchango wa ajira
sekta hii ilikuwa juu ya Romania, Bulgaria, Lebanon, Jamaica, Colombia, Kenya
na Ukraine. Takwimu hizi hazijionyeshi katika takwimu za serikali kwa kuwa
sanaa bado inaonekana ni utamaduni tu, na thamani yake katika uchumi haitiliwi
uzito. Kutambuliwa kwa kundi hili kutawezesha kutungwa sheria na taratibu za
kuwezesha Wasanii kuongeza ajira na mapato, na Taifa kufaidika na uchumi wa raslimali hii.
2. Kutajwa kwa MilikiBunifu Intellectual Property ) katika Katiba.
Mali ziko za aina 3. Kuna mali
zinazohamishika, mali zisizohamishika na mali zitokanazo na ubunifu. Aina mbili
za kwanza zimetajwa katika katiba na ulinzi wake hujulikana na ni wa jadi.
Lakini hii aina ya tatu ya mali huwa ni ngumu kuilinda kutokana na mfumo wake
kuwa haushikiki hivyo sheria maalumu hutungwa kulinda aina hii ya mali (IP
Laws). Mali zitokanazo na ubunifu kwa sasa ndio mali zenye kipa umbele duniani.
Uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali, ugunduzi wa njia mbalimbali za kuboresha
maisha, sanaa na mengi yanayolindwa na milikibunifu, vimeweza kutoa ajira kubwa
na kutoa mchango mkubwa wa kipato kwa wagunduzi na nchi ambazo wagunduzi hao
wamekuwa wakiishi au kuzisajili kazi zao. Kama wasanii, haki zetu katika
milikibunifu zinajulikana kama Hakimiliki, lakini kama Watanzania tunaona ni
muhimu kulinda haki zote za Milikibunifu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nchi zote ambazo zimeweka taratibu
imara za kulinda Milikibunifu duniani, zimewezesha wabunifu wake kubuni mambo
ambayo yameweza kubadilisha maisha ya binadamu wengine duniani kote. Marikani
iliweka kipengele cha Ulinzi wa hakimiliki katika katiba yake tangu mwaka Agosti 1787, na kazi za wagunduzi wa
Marekani tunaziona kila wakati katika kazi za sanaa na teknolojia. Korea kusini
ilinakiri sehemu ya katiba ya Marekani kuhusu ulinzi wa Milikibunifu kuanzia
mwaka 1948, kwa wakati huu wote ni mashahidi wa bidhaa kama Samsung, Ld Daewoo,
Hyundai na kadhalika.
Milikibunifu pamoja na kulinda haki
katika kazi za sanaa ambazo picha ndogo ya mapato yake zimetajwa hapo juu,
Milikibunifu italinda haki za wabunifu wetu, tafiti za wasomi wetu, ugunduzi
mbalimbali, taratibu mbalimbali za mambo yetu ya kiasili, dawa za asili za miti
yetu, na taratibu za matumizi ya dawa hizo, na mali asili zetu nyingine nyingi
tunazozifahamu na ambazo bado hatujazifahamu .
Kuna hasara nyingi ambazo
hupatikana kama nchi haina ulinzi wa Milikibunifu, mifano michache hapa
Tanzania, ni kupoteza kwa Milikibunifu ya jina Tanzanite, ambayo licha ya kuwa
inachimbwa Tanzania tu lakini jina linamilikiwa na kampuni ya Afrika ya Kusini.
Vazi la kikoi, pamoja kuwa ni la asili ya Tanzania, milikibunifu imesajiliwa
Kenya, staili ya michoro maarufu ya Tingatinga milikibunifu yake iko Japan. Na
haya ni machache ambayo yameshitukiwa Milikibunifu ikifuatiwa vizuri ndipo
haswa ukubwa wa tatizo utakapojulikana. Kuna ulazima mkubwa wa kutaja
Milikibunifu katika katiba na kuanisha ulazima wa kulinda kuendeleza na
kwezesha wabunifu wan chi kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo
Comments