MHE. PAULYNUS RAYMOND MTENDA |
Kuna
mashirikisho manne ya sanaa nchini ambayo ni Shirikisho la muziki, Shirikisho
la Filamu, Shirikisho la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za Ufundi.
Ulipotolewa wito wa makundi maalumu kutoa mapendekezo yao katika Katiba
Mpya, Mashirikisho yalikaa kama
Kamati za katiba na kuja na mapendekezo kadhaa kwenye katiba, mapendekezo hayo
licha ya kupokelewa na Tume ya Katiba hakuna kilichoingizwa katika Rasimu ya
Katiba.
Baada ya hapa ndipo wito ukatolewa wa kupendekeza majina ya
watu watakaoingia katika Bunge la Katiba, Mashirikisho yote yalipendekeza
majina mbalimbali. Hatimae jina la Paulynus Raymond Mtenda lilirudi kama ndie
mwakilishi aliyeweza kutoka katika kundi la Watu wenye malengo yanayofanana .
Tarehe 14, February 2014 viongozi wa Mashirikisho walikutana
BASATA kumpongeza Mbunge Mteule huyu na kumkabidhi rasmi mapendekezo ambayo
yalipelekwa awali kwenye Tume ya Katiba ili aweze kuyapendekeza katika katiba
mpya.
NAIBU KATIBU MTENDAJI WA BASATA AKIMKABIDHI MBUNGE MTEULIWA MAPENDEKEZO YA MASHIRIKISHO |
Pamoja na mapendekezo hayo Shirikisho la Filamu TAFF, na
Mtandao wa Wanamuziki Tanzania (TAMUNET), pia walikuja na hoja mbili muhimu
nazo ni;
1.
Kutambuliwa kwa wasanii kama ni kundi maalumu katika
Katiba, kama yalivyoweza kutambuliwa makundi ya wakulima, wavuvi na
wafanyakazi. Sababu kubwa za kuja na hoja hii ni kutokana na ukweli
unaopatikana katika tafiti mbalimbali.
Wasanii ni wengi sana, katika ripoti ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya
wasanii nchini wakati huo ilikuwa kiasi cha milioni sita. Kwa kuwa ni maka
minane sasa imepita toka wakati wa ripoti hiyo kuna kila sababu ya kuamini kuwa
kundi hilo limekuwa kubwa zaidi. Sababu nyingine ni ukweli kuwa wasanii
wanasababisha ajira kwa kundi kubwa la watu, wakiwemo wafanyakazi wa vyombo vya
utangazaji, wafanya kazi katika biashara ya matangazo, wasambazaji, wafanya
biashara ndogondogo, (machinga) na wengine wengi waliomo katika mnyororo wa
biashara hii ikiwemo, maproducer, mameneja, mafundi mitambo, watayarishaji wa
maonyesho na kadhalika. Hivyo sanaa si utamaduni tu bali ni kazi yenye mapato
makubwa. Ripoti ya WIPO ya mwaka 2012 imeonyesha kuwa kazi zitokanazo na
Hakimiliki huingiza fedha nyingi zaidi katika uchumi wa Taifa kuliko MADINI,
jambo ambalo ni wazi wengi wanaosikia kwa mara ya kwanza hushangaa kwa kuwa
kelele za mapato ya Madini ni kubwa sana katika jamii wakati hakuna
anaelalamika kuhusu mapato kutokana nah ii raslimali ya nchi inayoitwa sanaa.
Ripoti hiyo ya WIPO pia ilionyesha kuwa sekta ya Hakimiliki inaajiri watu wengi
zaidi kuliko, sekta za Madini, gesi, maji, Ustawi wa Jamii, Afya, Usafirishaji.
Hivyo ni sekta ambayo ina umuhimu sana katika uchumi wa Taifa ikiwa italindwa inavyostahili.
2.
Hoja ya pili ilikuwa kuwekwa rasmi kipengele cha
kutambuliwa kwa MIliki Bunifu na kuhakikishiwa ulinzi na uendelezaji wa
shughuli za Milikibunifu katika Katiba. Wasanii hutegemea maendeleo yao na
uboreshaji wa kazi zao kwa kulindwa kwa Hakimiliki. Lakini ingekuwa ni uchongo
wa mawazo kudai ulinzi wa Hakimiliki peke yake. Hivyo lengo ni kupata ulinzi wa
Miliki bunifu ambayo itasababisha kulinda haki za wasanii ,wabunifu, wagunduzi,
wanasayansi na teknolojia mbalimbali. Kuna mifano kila mara hutolewa ambayo
inaonyesha nchi kadhaa ambazo wakati nchi hii inapata Uhuru, uchumi wan chi
hizo nasi ulikuwa sawa, kama vile Malasia, Thailand na korea Kusini ambazo
kutokana na ulinzi na uendelezaji
wenye mipango wa Miliki Bunifu nchi hizo zimewezesha uchumi wao kukua na kuwa katika
chumi bora duniani
Comments