Wanamuziki kadhaa wenye heshima
katika muziki wa dansi watakuweko katika Tamasha la Gurumo 53, ambalo ni
tamasha la kustaafu muziki mwanamuziki mkongwe Muhidin Maalim Gurumo. Kati ya
wanamuziki watakao panda jukwaani ni
Komandoo Hamza Kalala, Mzee Makassy, wanamuziki nyota waliowahi kutamba
na bendi ya DDC Mlimani Park , Cosmas Chidumule, Abdallah Gama, Hussein Jumbe,
Mashaka Shaaban, Kalamazoo, Henry Mkanyia na Karama Legesu. Wengine ni Ali Yahaya na Boniface Kachala, Tshimanga Kalala Assossa,
Shaaban Lendi na Ibrahim Mwinchande. Pia wapulizaji wakongwe Majengo na King
Maluu watakuweko na wote kwa pamoja wataporomosha show kubwa Jumamosi
hii ndani ya TCC Club Chang’ombe. Wakali hao jana Alhamisi walihitimisha mazoezi ya nyimbo tano
watakazopiga katika tamasha hilo. Mazoezi hayo makali yalifanyika Amana Club
ambako kwa wiki nzima wanamuziki watakaoshiriki tamasha hilo wamekuwa
wakikutana hapo na kupiga mazoezi ya kufa mtu. Baadhi ya nyimbo zilizofanyiwa
mazoezi ni pamoja na “Selina”
utunzi wake Gurumo kwa kushirikiana na marehemu Joseph Mulenga, “Barua kutoka
kwa Mama” uliotungwa na Cosmas Chidumule na “Gama” (Tshimanga Kalala Assossa). Tamasha
la Gurumo 53 ni maalum kwa ajili ya kuhitimisha miaka 53 ya utumishi uliotukuka
katika muziki wa dansi kwa Muhidin Maalim Gurumo ambaye ametangaza rasmi
kustaafu muziki. Wasanii wengine wanaoshiriki mazoezi hayo ni Miraji Shakashia,
Hafsa Kazinja, Juma Katundu, Edo Sanga. Burudani zingine zitakazokuwepo siku
hiyo ni pamoja na bendi za Msondo Ngoma Music Band, Talent Band, na Twanga
Pepeta.
Comments