Na Moses Gasana
Mwezi wa nne mwaka huu
wanamuziki Jay Z na Beyonce, ambao ni mume na mke wakibarikiwa kuwa na mtoto
mmoja, walifanya safari ya kwenda Cuba kwa mapumziko katika kusherehekea miaka
mitano ya ndoa yao. Safari hiyo iliibua mjadala mkubwa miongoni mwa raia wa
Marekani na watu wengine wa Ulaya, Amerika ya Kusini, Asia na Afrika.
Kilicholeta mjadala miongoni mwa
Wamarekani wenyewe kuhusu safari ya Jay Z na Beyonce ni kutokana na ukweli kuwa
kuna masharti magumu ya kisheria ili mtu aweze kuruhusiwa kwenda nchini Cuba.
Hii ni kutokana na kuwa kwa miaka 51 kisiwa cha Cuba kimekuwa chini ya vikwazo
vya kiuchumi kutoka kwa serikali ya Marekani. Mojawapo ya vikwazo hivyo ni
kwamba raia wa Marekani haruhusiwi kusafiri kwenda Cuba kama safari yake hiyo
haihusiani na masuala ya elimu, utamaduni au misaada ya kibinadamu. Sasa kwa
safari ya Jay Z na Beyonce swali ikawa ‘imekuwaje hawa wapenzi tunaona wako
Cuba kama watalii, wakati safari ya utalii hairuhusiwi?’. Hapa lazima uzingatie
kuwa utalii unaingiza fedha za kigeni katika nchi, na serikali ya Marekani
ilishaweka vikwazo vya kuhakikisha Cuba haipati fedha za kimarekani zinazoweza
kupatikana kwa njia za biashara ikiwemo utalii. Maswali yakazidi, ‘hawa wapenzi
wamewezaje kwenda kutembea Cuba? nani kawaruhusu?’
Japo ilikuja kujulikana kuwa Jay
Z na Beyonce walipata kibali kutoka serikalini cha kwenda Cuba kwa kigezo cha
safari ya kitamaduni zaidi, lakini muonekano wao kule ukaacha taswira ya
wapenzi waliokwenda kama watalii. Hii ilisababisha hata wanasiasa fulani kutoa
maoni ya kutaka ati wapenzi wale washtakiwe kwa kuvunja sheria. Kwa wengine
wengi, safari ya Jay Z na Beyonce imeongeza chachu kwenye mjadala wa kutaka vikwazo vya kiuchumi
dhidi ya Cuba viondolewe kabisa.
Hata Jay Z mwenyewe katika
kuwajibu waliopinga safari yake ile akatoa wimbo mmoja unaoitwa Open Letter (Barua ya wazi) kuwajibu
vikali na kushutumu sera ya Marekani dhidi ya Cuba. Katika mstari mmoja
anasema,
“…I’m in Cuba, I love Cubans
This communist talk is so confusing
When it’s from China, the very mic that I’m using…”
Kwa wanaojua historia ya sera ya
Marekani dhidi ya Cuba, mashairi ya Jay Z ni ngumi nzito dhidi ya uso wa
udhalimu. Inakuwaje Marekani isitake kufanya biashara na Cuba kisa eti ni nchi
ya kikomunisti na inakandamiza haki za binadamu lakini ikawa tayari kufanya
biashara na China au Vietnam ambazo ni za kikomunisti. China kila kukicha
inashutumiwa na Marekani kwa kuvunja haki za binadamu lakini biashara baina yao
zinaendelea usiku na mchana!!
Kihistoria, Marekani iliiwekea
Cuba vikwazo mwaka 1960 wakati huo rais akiwa Dwight D.Eisenhower. Hasira hii
ilitokana na kutaifishwa kwa makampuni ya kimarekani takribani 5,911 yaliyokuwa
yakifanya shughuli za kiuchumi nchini Cuba. Hiyo ilitokana na uamuzi wa Fidel
Castro baada ya kuchukua nchi, kufuata siasa za kikomunisti na kuweka misingi
mikuu ya uzalishaji mali na uchumi chini ya usimamizi wa serikali. Biashara
huria ya kibepari ikawa imepigwa konde la nguvu.
Makampuni ya kimarekani
yaliyokuwa yakifanya biashara ndani ya Cuba yalilaumiwa kwa kuvuna faida kubwa
na kuiachia Cuba kilicho kidogo.Hata Kennedy wakati akiwa mgombea urais
alilaumu sera ya Rais Eisenhower juu ya Cuba kwa kutumia nguvu na ushawishi wa
serikali kuyasaidia makampuni yale kuikamua Cuba badala ya kuhakikisha nayo
inastawi kiuchumi. Pia Kennedy alilaumu sana serikali ya Marekani kuusaidia
utawala dhalimu wa dikteta Batista. Sio ajabu basi Castro hadi leo kwa kiasi
kikubwa anamheshimu marehemu Kennedy kama rais aliyekuwa anajua vyema hali
halisi ya maisha ya wacuba, japo naye ilimbidi tu afuate hivyo hivyo kwa shingo
upande sera ya Marekani kwa Cuba.
Marekani ilichukia na kuamua
kufunga milango ya ushirikiano na Cuba. Hakuna mmarekani anaruhusiwa kufanya
biashara na serikali ya Cuba. Lengo la vikwazo hivi ikiwemo kutoruhusiwa
kusafiri kwenda Cuba ni ili kudhoofisha uchumi wa Cuba ili wananchi wake
waung’oe utawala wa Fidel Castro (Hivi sasa Castro ni mstaafu). Hata hivyo kwa
umahiri mkubwa serikali ya kimapinduzi ya Cuba ikatokea kuwa mfano wa kuigwa
dunia nzima katika ujenzi wa nchi hasa huduma za jamii.Watu wengi duniani
wanajua namna Cuba ilivyojenga uwezo katika masuala ya huduma za afya na
matibabu, elimu, miundombinu na hata uwezo wa kijeshi.
Kwa miaka mingi Cuba imekuwa
ikitoa madaktari na walimu wake bure kwenda kusaidia nchi mbalimbali ili
kujenga mifumo ya utoaji huduma za afya, matibabu na elimu. Madaktari hao hao
huenda hata huko Marekani ili kusaidia utoaji wa matibabu kwa wananchi. Kijeshi
Cuba ilizisaidia sana Angola, Msumbiji na Namibia miaka ya 1970 kutembeza
kichapo dhidi ya makaburu wa Afrika ya Kusini. Hadi leo kichapo walichotoa
wacuba dhidi ya majeshi ya Afrika Kusini mwaka 1975 nchini Angola
hakitasahulika kamwe (soma kuhusu Operation Carlota). Tanzania tunamkumbuka
mcuba Brigadier Walden (marehemu sasa) aliyeshiriki katika kuongoza vita ya
kumng’oa Idi Amin mwaka 1978-79.
Kisiwa cha Cuba kina ukubwa wa
kilometa za mraba 100,000 na idadi ya watu inayokadiriwa kuwa kama milioni 11.
Mambo mengi sana yameshatokea
katika huu mvutano mkongwe kati ya Cuba na Marekani. Mwaka 1962 almanusura vita
ya tatu ya dunia ilipuke baada ya Urusi kuweka makombora ya nyuklia kisiwani
Cuba..Katika mgogoro huo wa makombora (The Cuban Missile Crisis) Marekani ilipinga
vikali ukitilia maanani kuwa Cuba iko umbali wa kilometa 150 tu kati yake na
Marekani (Kama maili 93). Urusi ilifanya vile ili kukilinda kisiwa cha Cuba
dhidi ya uvamizi mwingine kutoka Marekani.Hapa ikumbukwe kwamba mwaka mmoja
nyuma, mwaka 1961, kulifanyika uvamizi uliosaidiwa sana na Marekani wa kutaka
kuiondoa madarakani serikali ya Fidel Castro (Playa Giron Invasion).Uvamizi ule
ulikwama baada ya kupokea kipigo kutoka kwa majeshi ya Cuba huku Castro
mwenyewe akishiriki kikamilifu katika uwanja wa mapambano kwa kuelekeza hiki na
kile hadi ushindi. Hivyo mwaka 1962 Urusi ikakubali kuziondoa meli zilizokuwa
zimebeba makombora yale ya nyuklia kutoka Cuba na ikawa mwisho wa hofu ya
kuzuka vita kubwa.
Lakini ukweli ni kwamba Cuba
iliendelea kuishi huku ikikabiliwa na uchokozi mwingi sana kutoka Marekani.
Wacuba waliokuwa wanampinga Castro ambao wanaishi Florida nchini Marekani
wameendelea kusaidiwa kwa fedha na
rasilimali zingine ili kuidhoofisha serikali ya kimapinduzi ya Cuba.
Katika mojawapo ya uchokozi huo ni majaribio lukuki ya kumuua Fidel Castro.
Katika kitabu chake kiitwacho “My Life” Fidel Castro anaulizwa na mwandishi
Ignacio Ramonet kama anajua idadi kamili ya majaribio ya kumuua. Castro
anamjibu kuwa labda siku akienda mbinguni kuonana na Mungu ndipo ataweza kujua
idadi kamili ya majaribio hayo. Hata hivyo Ignacio Ramonet anaweka idadi ya
majaribio kuwa ni 600. Kuanzia kutegeshewa sumu hadi milipuko. Tazama vile vile
filamu (documentary) iitwayo 638 Ways to
Kill Castro yenye kueleza mikakati michafu ya shirika la kijasusi la
Marekani CIA dhidi ya Castro.
Njia zingine ambazo zimekuwa
zikitumiwa na Marekani ili kuidhoofisha serikali ya Cuba ni kuruhusu wacuba
ambao wanatumia njia zisizo halali kuingia Marekani kupata upendeleo fulani na
kuruhusiwa kubaki huko. Huu mkakati umewekwa hadi katika sheria (Cuba
Adjustment Act) kiujanja ili uweze kuhamasisha wimbi la wacuba kuikimbia nchi
yao ili kuweza kutengeneza mazingira ya serikali kuondolewa. Mkakati huu mchafu
nao kama mingine umefeli kwa miaka mingi.
Mbinyo wa serikali ya Marekani
dhidi ya Cuba umekuwa ukiendelea kwa miaka 51 hadi sasa. Vikwazo hivi vya kiuchumi vimekuwa
vikilaaniwa sana na Umoja wa Mataifa kwa miaka mingi mfululizo huku Marekani
ikiziba masikio.Kwa mfano, mwaka 2006, katika kura 183 kwa 4, Umoja wa Mataifa
uliitaka Marekani kuondoa vikwazo vya kiuchumi na biashara vilivyowekwa dhidi
ya Cuba. Marekani hadi sasa haijafanya hivyo japo rais Obama anatajwa kulegeza
kidogo mbinyo huo.
Katika marais waliopita wa
Marekani Bush alitia fora zaidi kwa ubaya dhidi ya Cuba. Kama kawaida yake
alidiriki hata mwaka 2004 kuiweka Cuba katika orodha ya nchi zinazounga mkono
ugaidi na kudai kuwa ina mpango wa kutengeneza silaha za sumu za kibaiolojia.
Tukumbuke kuwa ni Bush huyu huyu aliyedai Iraq ina silaha za maangamizi ya
halaiki lakini hadi leo hakuna ushahidi wowote uliounga mkono madai hayo.Sana
sana alifanikisha lengo lake la kumuua Saddam Hussein. Lakini Bush bila shaka
ni mnafiki namba moja duniani kwani Marekani imefadhili ugaidi dhidi ya Cuba
kwa kiwango kikubwa ukiacha mbali ugaidi dhidi ya mataifa mengine ya Marekani
ya Kusini kama Guatemala na Nicaragua. Kwa taarifa zilizopo mitandaoni ugaidi
huo dhidi ya Cuba umeua zaidi ya watu 3,500 nchini Cuba na kuacha watu
takribani 2,000 wakiwa na ulemavu. Bush analijua hilo wazi. Huyo ndiye Bush na
hiyo ndiyo Marekani “mtetezi wa haki za binadamu namba moja”.
Jay Z bila shaka kwa kusukumwa
na mapenzi yake makubwa kwa falsafa za Che Guevara ameamua kuukataa uongo
mkubwa wa kihistoria wa sera ya Marekani dhidi ya Cuba. Labda kwa ufupi tu, Che
Guevara alijipatia sana sifa na kupendwa dunia nzima pale kwa kushirikiana na
Fidel Castro na wananchi wengine wa Cuba walipofanikisha vita ya msituni na
kumwondoa dikteta Batista mwaka 1959 na kuunda serikali ya kikomunisti nchini
Cuba.Baada ya hapo Che Guevara alipita nchi mbalimbali akisaidia harakati za
kimapinduzi za wanyonge hadi alipokamatwa katika mapambano nchini Bolivia na
kuuawa mwaka 1967.
Jay Z kwa wimbo wake wa Open Letter ameamua kuwapiga kwenzi wapotoshaji
wa historia. Anasema,
“…Politicians never
did shit for me
Except lie to me,
distort history…”
Hakika wamarekani kwa miaka mingi wamelishwa historia ya
uongo kuhusu mgogoro wa nchi yao na Cuba. Propaganda chafu za kudhoofisha
maendeleo ya kisiwa cha Cuba zimedumu kwa miaka mingi na sasa zimeanza kuwaudhi
vijana kama Jay Z. Hivyo bila shaka kwa ukali wa mashairi na ngoma nzito za Hip
Hop mjadala wa kutaka Cuba iondolewe vikwazo umepata nguvu na ari mpya. Hongera
Jay Z na Beyonce kwa safari yenu Cuba na Mungu awajalie safari nyingi tu za
kuadhimisha miaka mingine ya ndoa yenu.
Na Moses Gasana
Mawazo Chanya Media
0713480670
Comments