SURPRISE YA MWAKA......BABA YAKE NYOTA NDOGO ALIKUWA MWANAMUZIKI MTANZANIA

-->
NYOTA NDOGO

JUMA TUTU

MZEE ABDALLAH HATIBU (KATIKATI)
Nyota Ndogo  ni jina maarufu sana Afrika Mashariki, ni mwanadada mwanamuziki mwenye sauti tamu sana, kati ya vibao vyake vyote nikiri kuwa wimbo wake wa Watu na Viatu ambao ulishinda tuzo katika Tanzania Music Awards 2007, niliupenda sana, pia huyu binti ambaye amekwisha toa album kadhaa zikiwemo Chereko, Nimetoka Mbali na Mpenzi, alizaliwa 1981 na akapewa jina la Mwanaisha Abdallah.

Mwanaisha alizaliwa Mombasa  hakumaliza shule na katika kazi alizopitia ni pamoja na msaidizi wa nyumbani. Katika kuonyesha tena kuwa wanamuziki wengine muziki umo kwenye damu, baba wa binti huyu alikuwa mwanamuziki. Katika maelezo ya rasmi ya Nyota Ndogo baba yake alikuwa mwanamuziki wa bendi moja wapo Mombasa na aliitwa Abdallah Hatibu.  Blog ya www.wanamuzikiwatanzania.blogspot.com ambayo ni maarufu kwa kutafiti historia ya wanamuziki wa zamamni wa hapa nchini iliweka historia fupi ya kundi maarufu la Jamhuri Jazz Band, pamoja na picha ya mmoja wa wanamuziki wa bendi hiyo aliyeitwa Abdallah Hatibu. Mwanamuziki mahiri Profesa Abbu Omari aliyeko Japan ambaye pamoja na bendi nyingi alizopigia pia alipiga Les Wanyika, na Simba wa Nyika alikuwa na maelezo ya ziada kuhusu Mzee Abdallah Hatibu baada ya kusoma blog hiyo. Haya ndiyo aliyoyasema……Mkuu Kitime katika picha za hawa wakongwe wa Jamhuri jazz hapo katikati kuna mwanamuziki alikuwa anaitwa Abdallah Hatibu, sisi tulikuwa tunamjua kama mzee Abdallah, alikwisha fariki miaka kama mitatu iliyopita. Huyu ni baba wa wanamuziki wawili mashuhuri wa Mombasa mmoja msichana Nyota Ndogo na mvulana Juma Tutu, Mzee Abdallah alizikwa kwao Muheza baada ya kuishi Mombasa na Nairobi kwa miaka mingi, hata mimi niliwahi kuishi nae jengo moja Nairobi 1982, Mzee huyu alikuwa mkali kwa gitaa nadhani hata kushinda Michael Vicent, nadhani huenda ikawa yeye ndiye aliyemfundisha Michael kupiga gitaa, niliwahi kumuuliza kuhusu huyu Michael na akasema huyo alikuwa mtoto mdogo tu ki miziki kwake. Kwa kweli huyu mzee Abdallah alikuwa mkali sana kwa gitaa Mombasa nzima na Nairobi alijulikana. …..Abbu Omar, Tokyo,Japan

Pia kadri ya website ya Juma Tutu (JUMA TUTU) , katika familia yao walizaliwa watoto sita, waliishi sehemu ya Majengo huko Mombasa, baba yake alikuwa mpiga gitaa la solo katika bendi ya Simba wa Nyika katika Club ya Sabasaba pale Mombasa, mama yao Christine Mungala pia alikuwa muimbaji katika kwaya ya kanisani. Dada zake wawili ni wanamuziki Nyota Ndogo na Leila pia ni wanamuziki.


Comments

Anonymous said…
Mkuu Kitime,kwa kuongezea tu,huyu mzee Abdallah alikuwa akitupa story kuwa aliwahi kupiga miziki na magoa pia nadhani mbali na Jamhuri jazz alipiga muziki ktk bar moja iliyoitwa kwa Mwangoe,hii ni kulingana na mazungumzo yake,kule Mombasa alipiga bendi maarufu na kubwa sabna enzi zile iliitwa Villa Negro,Kwa kawaida MOmbasa huwa na wanamuziki wakali sana,kwa vyombo hata uimbaji,na wengi wao wanaweza kupiga miziki toka pande zote za dunia,lakini kwa mzee huyu Abdallah musicians wote wa MOmbasa,Nairobi hata ndugu zetu wakongo walimtambua kwa ukali wa gita na pia ma scales makali makali.Mimi nilikuwa nina mipango niende Mombasa siku za likizo zangu toka huku Japan, ili nnikafanye nae mzee huyu session na kuzirekoda kwa kumbukumbu zangu,kwa bahati mbaya nilipowasiliana na huayu mtoto wake mkubwa Juma,akaniambia mzee wao alishafariki,na wanashukuru urithi mkubwa aliowaachia ni miziki ambayo inawasaidia kujikimu kimaisha.Nakumbuka watoto hawa nimewahi kuwabeba sana wakiwa wadogo,nilishangaa kuona wamekuwa wanamuziki mashuhuri Kenya !!! ni habari njema sana.Tumempoteze shujaa mkuu kwa wapiga magitaa wa kitanzania.
Abbu Omar,Prof.Jnr(Mwanamuziki)Tokyo,Japan.